Aliyekuwa Meneja wa Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza anazikwa leo katika Kijiji cha
Mulukulazo, Ngara mkoani Kagera huku familia yake ikisema haina cha
kusema kuhusu kifo hicho, bali inamwachia Mungu.
Akizungumza jana kijijini hapo,
mdogo wa marehemu, Alex Gashaza alisema familia imepokea msiba huo kwa
mshtuko mkubwa na kushangazwa na taarifa kwamba ulitokana na kujinyonga
kama inavyodaiwa.
Alisema baada ya kupokea simu kutoka Dar es Salaam kuhusu mazingira ya
kifo hicho, wameshindwa kujua sababu za kifo kwa kuwa hakuna mtu
aliyezungumza naye.
Alisema kaka yake hakuwa na tatizo lolote na wanafamilia, ndugu wala
jamaa zake wa karibu, hivyo familia haiwezi kuelezea jambo ambalo halina
ushahidi, badala yake inaacha tukio hilo mikononi mwa Mungu.
“Tumekuwa tukishirikiana naye kuendeleza familia yetu, kama unavyoona
nyumba ilipokuwa imefikia hatua ya kuezekwa, kuna mchango wake mkubwa
kifamilia,” alisema Alex.
Mwili wa Gashaza ulitarajiwa kuwasili Mulukulazo jana jioni na leo saa
4:00 asubuhi utapelekwa katika Kanisa la Anglikana katika kijiji hicho
kwa ajili ya sala na saa 6:00 mchana utaagwa kabla ya mazishi
yatakayofanyika nyumbani kwake.
Kiongozi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza mkoani
Mwanza, Mchungaji Lazaro Manjelenga ambaye pia ni baba mkwe wa mdogo wa
marehemu, alisema wana matumaini na Muumba kwa kile kilichotokea.
“Siri ya Mungu na mwanadamu wake hakuna wa kuijua, hivyo tusihukumu,”
alisema na kuongeza kuwa mazishi yatafanyika kwa mujibu wa taratibu za
Kanisa hilo.
Endelea kutembelea katemimethsela.blogspot.com hupata habari mbalimbali kama hizi kwa wakati muafaka.
0 comments:
Post a Comment