Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa
Monduli. Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa amesema hana rafiki yeyote CCM kwani yeye tayari alishapakia basi la Chadema.
Lowassa amesema ingawa aliwahi kumshauri mgombea ubunge wa jimbo la Monduli kwa tiketi ya CCM, Namelock Sokoine agombee lakini mambo yalivyobadilika alimshauri ajitoe hata hivyo alikataa na hivyo yeye sasa anamuunga mkono mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo, Julius Kalanga.
Akizungumza na wananchi wa Lokusale katika mkutano wa kampeni Lowassa alisema, "Suala la ubunge wa Monduli ni kweli nilimshawishi Namelock agombee ubunge lakini mambo yalipobadilika nilimshauri ajitoe, sasa kama CCM hainitaki kwa nini abaki, sina rafiki CCM,"alisema Lowassa na kuongeza: "Kama mtu amebaki CCM mimi nifanye nini? Alihoji Lowassa na wananchi wakijibu "Unamwachaaaaaaaa."
Huku wananchi wakishangilia Lowassa alisema amempendekeza Kalanga hivyo Namelock akubali kwa kuwa mbunge anayefaa Monduli ni Kalanga.
Aliwaambia wananchi hao wamnadi Kalanga kama Mbunge wao na wakiulizwa na mtu yeyote wamjibu kuwa Lowassa ndiye amewatuma.
"Moran mfanye kazi hiyo na pia mlinde kura. Nawapa ushauri wa bure kwamba mbunge anayefaa ni Kalanga kwa ushauri wangu mumchague na mtu asiwasumbue."
Lowassa aliwaambia wananchi hao kuwa akiingia madarakani suala la barabara litashughulikiwa kwani ndicho kitu pekee kinachowapa tabu wananchi wa Lokusale.
0 comments:
Post a Comment