Na: Ayoub Hinjo(Ayo's Mata Maestro)
Furaha ya maisha ni kufurahia kile ambacho kimekufanya ufurahi. Sio hivyo tu wakati mwingine furaha huja pale unapokamilisha jambo lililokuwa linakutatiza. Furaha hujenga upendo na uaminifu maishani.
Lomar do Nascimiento wengi wanamfahamu kwa jina la Mazinho,ndiye baba mzazi wa Thiago Alcantara na nduguye Rafinha. Mazinho alikuwa mcheza kandanda mashuhuri sana wa Brazil na timu nyingi za klabu ni mshindi wa kombe LA dunia mwaka 1994 pamoja na kina Romario. Uwepo wa vijana wake wawili waliofuta nyayo zake ni zaidi ya furaha kwake,sababu ni nadra sana kuona mtoto anarithi uwezo wa baba na kufanya kazi kama baba au zaidi ya baba.
Pep Guardiola ndiye aliyetuletea Messi kwenye ulimwengu huu wa mpira. Jicho lake na moyo ulikuwa radhi kumruhusu Ronaldinho aondoke ili kijana mdogo mwenye kipaji cha ajabu apate nafasi kwenye timu ya wakubwa. Hapo alifanikiwa kwa asilimia zote na imani yake juu ya Messi ikalipa,alishinda kila kitu kupitia Messi. Furaha ya Pep ilikamilika sababu alikamilisha shughuli yake kupitia mtu ambaye alimtengeneza.
Baada ya Messi,Pep alicheza kamari nyingine pale Barcelona, hii ilikuwa ni kumpandisha timu ya wakubwa kijana mdogo wa miaka 17 kutoka shule ya kukuza vipaji hapo Barcelona (La Masia). Kijana huyo alikuwa Thiago Alcantara,ni kipaji hasa cha mpira ambacho amerithi kutoka kwa baba yake mzazi. Maisha hayakuwa mazuri kwa Thiago sababu nafasi ambayo alikuwa akicheza kulikuwa na mseto mzuri ambao umetengenezwa kupitia Xavi na Iniesta. Thiago alishindwa kuonesha alichokuwa nacho sababu alipewa muda mdogo wa kucheza lakini hakuvunjika moyo. Alipambana kupigania nafasi kwenye timu,alionyesha uwezo alionao kila alipopata nafasi. Baada ya Guardiola kuondoka mambo hayakuwa mazuri sana kwake na nafasi ilikuwa finyu kwake lakini hakuvunjika moyo,alipambana kumshawishi kocha ampatie nafasi. Lakini mwishowe aliamua kuondoka Barcelona.
Thiago alielekea Bayern Munich,kila mtu ilimshangaza sababu alienda sehemu ambayo kuna fanana na alikotoka na kuzua maswali mengi kwa watu. Kwa kipindi kile Alcantara alihusishwa sana na Manchester United lakini aliamua kwenda Bayern Munich. Wengi walihoji kama angepata nafasi ya kucheza Bayern Munich,wakati wakijiuliza maswali hayo yote walisahau kujiuliza Thiago anaenda kucheza chini ya nani. Hilo ndio lilikuwa swali la msingi kwao pasipo kuangalia Bayern Munich kuna wachezaji wenye uwezo gani. Uwepo wa Guardiola ulikuwa ni ushawishi tosha kwa Thiago sababu ndiye mtu aliyejua thamani yake. Pep alishindwa kuficha hisia zake kwa Thiago sababu aliamini msingi wa mfumo wake ataanza kuujenga kupitia kwake. Wakati macho ya wengi yakiwa kwa kina Robben,Muller,Costa,Ribery na wengine mastaa wakubwa wanasahau ni nani ambaye anawafanya hao wameingia kwenye mfumo wa Pep pamoja na uwepo wao wa muda mrefu kwenye timu. Thiago ni shujaa asiyeimbwa(Unsung hero) na kazi yake ni kukimbiza mwizi kimya kimya. Thiago ni kama kondoo mpotevu aliyepotea kwenye malisho na kwenda sehemu yenye malisho mengi akiongozwa na mchungaji yule yule aliyemtoa kule kwenye malisho mengi zaidi. Kwa sasa nahisi Barcelona wanajutia kupoteza kipaji hiko sababu muda huu ulikuwa muafaka kwake kucheza na kufurahia maisha pale Catalunia.
Guardiola anamtumia Thiago kama silaha yake ambayo wengi wanashindwa kuifahamu. Thiago ni kama wale walenga shabaha za kulenga kwenye mauaji(Sniper) ambaye anajificha ipi asionekane.
Maisha ya Pep Guardiola ni mazuri sana pale Bayern Munich sababu ya Thiago ni kama yalivyokuwa mazuri Barcelona kwa uwepo wa Messi. Iwe wakati wa mvua au jua kali, Thiago Alcantara ndiye mwamvuli wa Guardiola kwenye vipindi hivyo vya mabadiliko. Asante sana kwa kutuletea Messi lakini asante zaidi kwa kutuletea Thiago Alcantara ambaye hatazamwi na wengi lakini ndiye shujaa wako sasa. Ni furaha tosha kwa Pep na Thiago.
0 comments:
Post a Comment