Facebook

Sunday, 17 January 2016

WAZANZIBARI MNALIJUA HILI KUHUSU MAALIM SEIF?

Na Bollen Ngetti
Kuna baadhi ya wasomaji wa maandiko yangu wameendelea kunilaani na kudai ninamshambulia Maalim Seif na huenda nina chuki binafsi na mwanasiasa huyo wa Z'bar. Wengine wameenda mbali na kudai ninatumika! Ninachojua ni kwamba unaweza kumzuia ndege asitue juu ya kichwa chako lakini kamwe huwezi kumchagulia pa kujenga kiota chake. Sina chuki na Seif, situmiki maana si hulka yangu. Tatizo ni kuwa mimi ni muumini wa dhana ya ukweli hata kama ni mchungu kama "kloriti" ya Masai nitausema tu. Kuna baadhi ya Watu Z'bar kwa sasa hawataki kabisa kuambiwa ukweli maana unawachoma hadi kwenye mfupa.

Wengine wamenitukana huku wengine wakinitisha nakadhalika. Niwaambie tu kuwa nitaacha kusema tu ninachojua ni uongo lakini ukweli ninausema hadi mwisho wa uhai wangu maana bila kuyasema mambo haya mtaendelea kuishi ndani ya boksi jeusi.

Maalim Seif hana mkosi wa kumfanya asiwe Rais wa Z'bar isipokuwa ukweli mchungu ni kwamba amekosea hesabu katika mbio za kusaka Urais toka 1995, 2000,2005,2010,2015 na sasa 2016 na sasa wakati umeshamtupa mkono. Hawezi tena. Niharakishe kusema kwamba Seif anatafunwa na mzimu wa dhambi ya kumsaliti mwalimu wake mkuu wa siasa Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi na labda hili ndilo limemfuja.

Z'bar kwa asili ya Mila, jadi na ilivyojengeka na kuaminiwa na wengi ni kuwa huwezi kumsaliti, kumdharau ama kumdhihaki mwalimu wako wa skuli, amali, madrasa, au sheikh wako wa ilmu au wa kitwanga maana kufanya hivyo ima utapungukiwa na ibra njema au hutofanikiwa katika mbio za kusaka tija au mafanikio ya maisha yako.

Wengi hatujui ama hatutaki kujua ni kwa namna gani Seif aliweza kupenya hadi leo kuwa MAALIM na kuwa mwanasiasa mashuhuri kama walivyokuwa Profesa Abdulrahman Babu au Ali Muhsin Al-Barwan.

Mzee Jumbe alifanya ujasiri wa aina yake kumteua Seif kijana kutoka Pemba kuwa Waziri wa Elimu katika wakati wa siasa za mbinde kufuatia Mapinduzi ya damu yaliyofanywa na wakulima na wakwezi ambao wengi hawakuwa na elimu lakini pia ni kufuatia kuuawa kwa Rais Amani Karume aliyepigwa risasi na Homoud Mahmoud kijana mwenye asili ya uchotara wa ki-Arabu kama Maalim Seif kutoka Pemba.

Ikumbukwe kuwa ndani ASP (sasa CC.) kulijengeka dhana iliyojenga kiongozi wa ZPPP Mohammed Shamte Hamad mwenye asili ya Pemba kulikataa pendekezo la ASP mwaka 1963 la kumtaka aunde Serikali ya mseto yenye sura ya ki-Afrika lakini hakuliafiki na kuamua kupeleka viti vyake kwa ZNP-HIZBU na kuunda ZPPP/ZNP zikiwa na asili ya Upemba kupambana ASP (weusi wa Unguja).

Ni kweli kuwa Jumbe alihitaji wasomi maana alikuwa ni msomi lakini kumchukua mwanasiasa kutoka Pemba kumfanya mtu wa karibu ulikuwa ni ujasiri maana iliaminika kuwa mtu kutoka Pemba asingeweza kuwa mtetezi wa kweli wa mapinduzi ya mwaka 1964 (rejea maadhimisho ya juzi).

Hata hivyo jumbe hakujali pamona na kwamba hata Unguja kulikuwepo na vijana wasomi lakini Jumbe alitaka kuwaunganisha Wazanzibari na kuondoa dhana ovu ya u-Pemba na u-Unguja ambao sasa Seif anashutumiwa kuufufua kwa Ari mpya. Hata sasa Seif anashutumiwa kuwa machotara wa ki-Arabu ndio wenye sauti ndani ya CUF na ndio maana chama hicho kimeota mizizi Pemba tofauti na CCM iliyopo pande zote hata hakina nguvu kubwa kwa Pemba.

Karatasi za SIRI za Rais Jumbe zilizokuwa na mikakati ya kudai Serikali 3 ziliibwa ofisini kwa Jumbe zikakutwa mezani kwa Nyerere Dodoma, NEC huku Seif akiwa msatari wa mbele kumwambia Nyerere, "Mwl ukitaka muungano uendelee kumwondoe Jumbe kwenye Urais" na hata sasa kina Seif Khatib wanasema wazi, "Seif aliwasaliti Wazanzibari kupata kiti Chao UN nk."

Miongoni mwa wasemaji wakubwa katika mkutano huo wa NEC kutaka Jumbe abanduliwe nyadhifa zake abaki kapuku alikuwa Maalim Seif kwa mategemeo ya kutwaa Urais. Hapo mwanafunI anaamua kumsulubu mwalimu wake hadharani!

Mwalimu wake aliyemfanya agile hapo juu hadi sasa anataka avuliwe nguo hadharani. Hii kwa Wazanzibari ni laana mbaya sana na ishangaze leo huyo huyo aliyekataa serikali 3 leo anasafiria nyota ya Jumbe ya Serikali 3. Tuiteje hali hii kama si unafiki na uzandiki? Seif akawa kama Petro (Biblia) alivyomkana Bwana Yesu aliyekuwa kipenzi na msaidizi wake wa karibu.

Zama za Jumbe imebebeshwa lawama nyingi kuwa Wapemba walinyimwa elimu huku Waziri wa Elimu akiwa ni Mpemba. Mdaini elimu yenu.

Leo wapambe wanaliangalia kundi la machotara kutoka Pemba wakimuunga mkono Seif lakini hawaliangalii abadan lile la Waafrika weusi titii lilipo Unguja likilinga na kujenga hofu iliyowagusa Enzi za Maalim Seif akiwa Waziri wa Elimu na usaliti alioufanya dhidi ya Mzee Jumbe.

CUF bado ina nafasi ya kumpata mgombea Urais anayeweza kuunganisha visiwa vya Pemba na Unguja na ijulikane kuwa Maalim anatafuta Urais kwa ajili ya machotara wa Pemba na si kuunganisha Wazanzibari maana historia ni mwalimu mzuri. Mkataeni Seif kwa usalama, amani na umoja wa visiwa vya Zanzibar. Nawasilisha.

BNgetti 15/01/2016

0 comments:

Post a Comment