Wakati polisi ikisema imefurahi kupata taarifa hizo na kwamba itazifanyia kazi, habari zilizopatikana jana kuhusu hali ya Nasra zimesema atafanyiwa vipimo 18 ili kubaini hali ya afya yake. Vipimo vya awali, vimebaini kuwa amevunjika mifupa ya mikono na miguu na kwamba atapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Kuhusu kaka yake, baadhi ya majirani wa nyumba aliyokuwa anaishi mama mzazi wa Nasra enzi za uhai wake walidai kuwa Mariamu alikabidhiwa watoto wawili kuwalea baada ya mama yao kufariki dunia.
Mmoja wa majirani hao, Ramadhani Mansuri alisema wakati mama mzazi wa Nasra akiishi eneo la Mjimpya alikuwa na watoto wawili akiwamo Nasoro ambaye aliachwa akiwa na umri kati ya miaka 14-15.
Vipimo
Ofisa Ustawi wa Jamii, Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu alisema taarifa alizopata kutoka kwa madaktari zinasema kuwa mtoto huyo atafanyiwa vipimo 18 ili kubaini hali ya afya yake.
Akizungumzia matokeo ya vipimo vya awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk Rita Lyamuya alisema haijafahamika sababu za kuvunjika kwa mifupa hiyo.
Dk Lyamuya alisema jana kwamba, mtoto huyo ameshafanyiwa vipimo vingine kadhaa ambavyo vinaonyesha kwamba anasumbuliwa na homa ya mapafu (pneumonia) na utapiamlo unatokana na kukosa lishe bora.
“Tulilazimika kumfanyia vipimo hivyo vya awali kwa sababu alikuwa anaonekana kama anayeugulia maumivu, kwa hiyo vipimo vingine vitaendelea kufanywa kadri tutakavyoona inahitajika,” alisema Dk Lyamuya.
Alisema kipimo cha X- Ray ndicho kilichoonyesha kuvunjika kwa mifupa yake ya miguu na mikono na kwamba hali hiyo ndiyo inayosababisha ashindwe kusimama na kutembea.
“Wakati anafikishwa hapa hospitalini alikuwa amebanwa na kifua na alikuwa anashindwa kupumua vizuri. Ilitulazimu kumwekea mashine ya oksijeni ili imsaidie kupumua, lakini sasa hali yake inaendelea vizuri na tayari tumeondoa mashine, anaendelea na matibabu mengine,” alisema.
Mbali na tiba, Nasra pia alifanyiwa usafi wa mwili wake ambao ulikuwa mchafu kutokana na kutoogeshwa kwa muda mrefu na sasa inaelezwa kuwa yuko kwenye hali ya kuridhisha na wasamaria wema wameanza kujitokeza kumpa misaada ya nguo na chakula.
0 comments:
Post a Comment