Facebook

Sunday 4 May 2014

Nigeria wafanya msako mkali Abuja


Mashambulio NIgeria
Majeshi ya usalama ya Nigeria yamewakamata watu kadha katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja kufuatia mashambulio ya mabomu ya hivi karibuni, zikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Uchumi wa Dunia mjini humo.
Wengi wwaliokamatwa wanasemekana kuwa raia wa kigeni, lakini hakuna taarifa zaidi za kina zilizotolewa.
Maafisa wameagiza kufungwa shule na ofisi za serikali wakati wa mkutano huo, ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na marais wa Rwanda, Senegal na Kenya pamoja na waziri mkuu wa China Li Keqiang.
Serikali iko katika shinikizo kubwa la kukabiliana na kusambaa kwa ghasia nchini Nigeria.
Mlipuko wa Alhamisi uliua watu 19, wiki mbili baada ya mlipuko eneo la karibu na hapo kuua watu 75.
Hakuna kikundi kilichodai kuhusika na mashambulio hayo, lakini wapiganaji wa Kiislam wa kundi la Boko Haram wanatuhumiwa kuhusika na matukio hayo.
Rais Goodluck Jonathan akitembelea eneo lililoshambuliwa mjini Abuja
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Nigeria amesema waliokamatwa Jumamosi wanahojiwa na wametoa "taarifa muhimu."
Boko Haram pia wanaaminika kuhusika na utekaji wa zaidi ya wanafunzi wa kike 200 kutoka shule yao katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria zaidi ya wiki mbili zilizopita.
Rais Goodluck Jonathan anatarajiwa kulihutubia taifa Jumapili baada ya kukosolewa kwake namna anavyowashughulikia wapiganaji wa Kiislam.
Jumamosi serikali ya Marekani iliwaonya raia kuhusu kuwepo mpango wa kushambuliwa kwa moja ya hoteli za Sheraton karibu na Lagos, mji mkuu wa kibiashara wa Nigeria.

0 comments:

Post a Comment