Jina la Zari hivi sasa limekuwa jina maarufu katika masikio ya Watanzania,
Afrika Mashariki na kwingineko hasa baada ya mwanadada huyo
mfanyabiashara na mwanamuziki wa Uganda kuwa na urafiki na Mwanamuziki
wa Bongo Fleva, Nassib Abdul maarufu kwa jina la usanii Diamond Platnum.
Kwenye mitandao ya kijamii kama Tweeter, Facebook, Instagram na hata
Whatsapp lazima utakutana na jina Zari akiunganishwa na Diamond na
wengine wataunganisha na Wema Sepetu aliyewahi kuwa mpenzi wa Diamond.
Uhusiano kati ya Zari na Diamond umezua gumzo kila eneo Tanzania na
Afrika Mashariki huku wakifananishwa na mastaa wa nje kama vile Kanye
West na Kim Kardashian kwa namna wanavyofuatana wakati wote huku Diamond
akionesha kila aina ya mbwembwe za kumjali mrembo huyo kutoka Kampala,
Uganda.
Uhusiano wa Zari na Diamond umewafanya kuandamana kila sehemu hivi sasa.
Wawili hao walianza kuonekana kuwa na ukaribu wa mahusiano tangu
Diamond alipokwenda Afrika Kusini kwenye Tuzo za Channel O ambapo
Diamond aliibuka na ushindi wa Tuzo tatu.
Baada ya Tuzo hizo, Zari alimualika Diamond kushiriki katika ‘pati’
maarufu ambayo mwanadada huyo huandaa kila mwaka nchini Uganda ambapo
mwaka huu ilijulikana kama All White Ciroc Party.
Wawili hao baada ya sherehe hiyo, walifuatana ambapo Zari alimsindikiza
Diamond nchini Rwanda na Burundi alipokwenda kutoa burudani nchini humo,
na picha kusambazwa katika mitandao ya kijamii na kuwafanya wawili hao
kuwa gumzo hivi sasa katika mitandao Tanzania na Afrika Mashariki. Je,
Zari ni nani hasa? Zarina Hassan Tlale.
Maarufu kama Zari ni Mganda anayeishi Afrika Kusini. Mrembo huyo ni
mwanamuziki na mfanyabiashara. Ni mwanamke aliyefanikiwa na anayependa
kuishi maisha ya kifahari. Anamiliki magari ya kifahari na yenye gharama
kubwa kama Lamborghini Gallardo, BMW- 2006, Chrysler-2008, Audi Q7-2010
na Ranger Rover Sports .
Mwanadada huyo ni binti wa Halima Sultan Hassan na Nasur Hassan akiwa na
asili ya damu mchanganyiko ikiwa ni pamoja na ya Kihindi , Toro,
Somalia na Burundi kutoka mji wa Jinja, Uganda. Babu mzaa mama yake
anatoka India na bibi yake ni kutoka Uganda. Babu yake mzaa baba ni
kutoka Somalia na bibi yake mzaa baba anatoka Burundi.
Zari maarufu kama The Bosslady aliwahi kuolewa na mwanamume
anayejulikana kwa jina la Ivan na kubarikiwa watoto watatu wa kiume
Pinto, Didy na Quincy na anamiliki kampuni tatu. Mwanadada huyu
alizaliwa Septemba 23, 1980. Zari amekulia katika mji wa Jinja katika
nchi ya Afrika Mashariki inayojulikana kama Uganda.
Zari alisoma shule ya msingi, kisha kwenda Shule ya Sekondari ya
Wasichana ya Jinja ambapo alisoma kwa bidii kutimiza ndoto zake. Baada
ya kumaliza elimu ya sekondari, mwanadada huyo alihamia katika mji mkuu
wa nchi hiyo, Kampala ambapo alikuwa akitoa burudani ya muziki katika
maeneo ya starehe kabla ya kuhamia mjini London, Uingereza na kusomea
Stashahada ya masuala ya urembo (cosmetology).
Historia yake kimuziki inaonesha Zari alianza kuimba akiwa na umri mdogo
wakati akisoma shule ya msingi ambapo alikuwa akitoa burudani katika
matamasha ya muziki yaliyokuwa yanaandaliwa na wafanyakazi wa shule,
wakati wa hafla za mwishoni mwa mwaka na katika mashindano mengine ya
jumuiya akiwakilisha shule yake.
Ingawa amekulia katika familia ya Kiislamu yenye wasichana sita na
wavulana wawili, Zari hakuacha mapenzi yake kwenye muziki. Alianza
muziki akiwa na umri mdogo na albamu yake ina nyimbo kali kama ‘Toloba’
na ‘Hotter Than Them’. Watu waliomvutia katika muziki ni Wasanii wa
Marekani Arethal Franklin na Whitney Houston wakati akiwa sekondari.
Afrika waliomvutia akapenda muziki ni wanamuziki wa Afrika Kusini Brenda
Fassie, Miriam Makeba, Lucky Dube na Malkia wa Muziki Afrika Kusini,
Yvone Chaka Chaka. Alipojiunga na sekondari alijiunga na makundi ya
dansi, drama na muziki jambo ambalo lilimsaidia kuchaguliwa kwa miaka
miwili mfululizo la Muigizaji Bora.
Baada ya miaka miwili ya kufanya vizuri katika majukwaa na matamasha ya
shule, alipumzika na kuhama kutoka Uganda kwenda London, Uingereza na
kuendelea na masomo yake lakini bado mapenzi yake kwa muziki yakiwa
mawazoni mwake. Zari kwa msaada wa familia, mashabiki na marafiki wa-
naopenda mtindo wa muziki wake na kuamini anaweza aliamua kuchukua hatua
mwaka 2007 wa kurekodi singo yake ya kwanza inayoitwa Oliwange (ikiwa
na maana wewe ni wangu) .
Mwaka 2008 Zari alishinda Tuzo ya Channel O ya Video Bora ya Muziki ya
Msanii Bora Afrika Mshariki. Hafla ya tuzo hizo ilifanyika Johannesburg,
Afrika Kusini. Tangu hapo Zari ameendelea kutoa nyimbo zaidi za
kuvutia, huku akitiwa moyo na mashabiki wake wakati huo.
Mwaka 2009 alipata Tuzo inayojulikana kama Diva ya mwaka katika
kipengele cha Diaspora tangu hapo aliendelea kutengeneza muziki. Zari
hivi sasa anaishi Afrika Kusini ambapo anamiliki maduka makubwa ya
vipodozi na shule ya elimu ya juu mjini Pretoria wakati akiendelea
kujijenga kimuziki.
Inaelezwa kuwa Zari na aliyekuwa mumewe Ivan wanamiliki Shule ya
Brooklyn City ambayo ina kampasi sita Afrika Kusini, huku kila moja
ikiwa na wanafunzi kati ya 800 hadi 2,100. Wanafunzi hao hupewa vyeti
vya taifa wanapomaliza mwaka. Vile vile Zari amejenga hosteli iliyopo
barabara ya Sir Apollo Kaggwa, Kampala na anamiliki nyumba kadhaa katika
mji huo hasa eneo la Munyonyo, pamoja na duka kubwa la nguo Afrika
Kusini.
Ingawa muziki wake haujafanya vizuri kama wanamuziki wengine wa Uganda
akiwemo Jose Chameleone, Bebe Cool, Bobi Wine na Ragga Dee, Zari amekuwa
akifurahia kwa mafanikio zaidi kwenye biashara na kutokana na hilo
anasema lazima arudishe kwa jamii na hivyo kuamua kusaidia vituo na
taasisi kadhaa zinazohitaji misaada kama Katalemwa Cheshire Home, Sanyu
Babies’ Home pamoja na Gereza la Luzira.
Mfano mwaka 2013 kutokana na moyo wake wa kusaidia, kwa kutimiza hilo
baada ya sherehe zake anazozifanya kila mwisho wa mwaka aliamua
kutembelea Kituo cha Watoto Yatima cha M-Lisada kilichopo Nsambya siku
moja kabla ya Sikukuu ya Krismasi, akifuatana na watoto wake Pinto, Didy
na Quincy.
Alitoa zawadi maalum kwa watoto hao, ambapo Zari alishiriki kuandaa
chakula cha Krismasi na kisha baadaye kutoa msaada wa vitu vyenye kama
vile taulo za wanawake, sukari, biskuti, mchele na matoke. Mbali na
masuala mengine yote, kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, watu wengi nchini
Uganda wanakubaliana kuwa Zari ndio Mwanamke Mrembo zaidi nchini humo.
“Sitafuti umaarufu, wenyewe umaarufu ndio hunifuata,” aliwahi Zari
kusema kupitia mtandao wa Red Pepper akikanusha habari za baadhi ya watu
wanaodai kuwa anatafuta umaarufu kwa nguvu.
Habari zake kuandikwa katika mitandao ya kijamii pamoja na shughuli zake
za uhisani zimesababisha wengi kudai kuwa anataka tu umaarufu,
kujulikana na kuzungumziwa kila wakati.Hata hivyo akijibu madai hayo,
Zari alisema umaarufu unamtafuta yeye na sio kwamba yeye anautafuta.
0 comments:
Post a Comment