Sakata la lililojitokeza la mrembo
wa Taifa wa mwaka huu 'Redd's Miss
Tanzania 2014', Sitti Mtemvu
kudaiwa kudanganya umri, limeingia
katika sura mpya baada ya Baraza la
Sanaa Tanzania (Basata) kueleza
kuwa litamvua taji hilo endapo
itabainika kweli alichakachua umri
wake.
Katibu Mkuu wa Basata, Geoffrey
Mwingereza, aliliambia NIPASHE jana
kuwa baraza hilo linasubiri
uchunguzi ukamilike na endapo
watabaini kuna udanganyifu
ulifanyika hawatakuwa na la kufanya
zaidi ya kumvua taji.
Wakati Mwingereza akieleza hayo,
viongozi wa Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo
wanatarajia kukutana leo jijini Dar
es Salaam kwa ajili ya kujadili
sakata hilo la Sitti.
Akizungumza na NIPASHE jana, Naibu
Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia,
alisema serikali imesikia taarifa
za mkanganyiko kuhusiana na mrembo
huyo hivyo imeamua kuitisha kikao
ili kuanza kulifanyia kazi.
Nkamia alisema kamwe serikali
haiwezi kukaa kimya pale ambapo
jina la nchi linatajwa vibaya.
"Siwezi kukuambia hatua gani
zitachukuliwa, ila kesho (leo)
tutakuwa na kikao, serikali haiwezi
kukaa kimya, kuna vyombo vyake
vinalifanyia kazi," alisema Naibu
Waziri huyo.
Aliongeza kuwa yeye alikuwa nje ya
Dar es Salaam, lakini tayari kuna
maelekezo aliyoyatoa na yameanza
kufanyiwa kazi na wizara hiyo.
Siku moja baada ya Sitti kutangazwa
mshindi wa taji hilo, taarifa za
mrembo huyo kuhusu umri wake
zilianza kusambaa kwenye mitandao
ya kijamii zikionyesha kuwa ana
miaka 25, hivyo hana sifa za
kushiriki shindano hilo hapa
nchini.
Nakala ya hati ya kusafiria ya
mrembo huyo ambayo ilitolewa
Februari 15, 2007 na muda wake wa
kumaliza kutumika ukiwa ni Februari
14, 2017 yenye namba AB 202696
inaonesha Sitti ambaye pia
anashikilia taji la Kitongoji cha
Chang'ombe na Kanda ya Temeke,
alizaliwa Mei 31, 1989.Pia taarifa
nyingine zinazoone sha mrembo huyo
ana miaka 25 ni zilizokuwa kwenye
Taasisi ya Explore Talent, ikimtaja
kwamba anaishi Dallas, Texas, urefu
wake ni 5'8, umbo lake ni la kati,
asili yake ni Mwafrika na rangi ya
macho yake ni kahawia.
Juzi, Kamati ya Miss Tanzania
iliyoko chini ya Mratibu wa
shindano hilo, Hashim Lundenga,
ilisema kuwa Sitti amezaliwa Mei
31, 1991 katika wilaya ya Temeke
jijini kwa mujibu wa cheti chake
cha kuzaliwa alichokionesha.
Lundenga alionesha cheti cha
kuzaliwa cha Sitti ambacho
kimetolewa na Wakala wa Usajili,
Ufilisi na Udhamini (RITA) Septemba
9, mwaka huu kikiwa na namba
1000580309 na kikimtaja baba yake
ni Abbas Mtemvu Zuberi (Mbunge-
Temeke) wakati mama ni Mariam
Nassor Juma (Diwani- Temeke).
Hata hivyo, Lundenga alisema kuwa
kamati yake inaendelea na uchunguzi
kuhusiana na taarifa hizo na endapo
watabaini kuwepo na udanganyifu
watamchukulia hatua mrembo huyo kwa
kushirikiana na Basata.
Pia Lundenga na Sitti, walikanusha
taarifa za mrembo kuwa kuwa na
mtoto na kusema kwamba mwenye
uthibitisho wa jambo hilo anatakiwa
aliwasilishe kwa kamati ili hatua
zichukuliwe.
Sitti aliibuka kidedea katika
shindano la urembo la taifa
lililofanyika usiku wa Jumamosi ya
Oktoba 11 kwenye Ukumbi wa Mlimani
City jijini na kuwashinda washiriki
wenzake 29 waliokuwa wanawania taji
hilo.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment