Facebook

Wednesday, 8 October 2014

OKWI,MOSSOTI NA KALAMU YA FRIEDRICH VON WIESER

 
              Adam Smith ndie gwiji la maswala ya uchumi kuwai kutokea Duniani.Kanuni na nadharia nyingi za uchumi zimetoka kwenye kichwa cha Adam Smith.Ukiacha Adam Smith maJabali mengine ya uchumi kuwai kutokea Duniani  ni Karl Max na  John M.Keynes. John M. Keynes,Karl Max na Adam Smith kwenye uchumi ni kama pele , Maradona na Messi  kwenye soka.Ni wachumi bora kuwai kutokea Duniani.
              Pamoja na Ubora waliokua nao Karl Max na Adam Smith bado walishindwa kutueleza ni jinsi gani mtu atafanya maamuzi magumu na maamuzi hayo yasimletee matokeo hasi.Pamoja na Dunia kumuhesabu kuwa ni miongoni mwa watu 100 muhimu kwenye karne ya 20 bado Keyness alishindwa kusaidia  wafanyabiashara wadogo wadogo jinsi ya kufanya uchaguzi sahihi kati ya vitu viwili muhimu.Unaweza ukafanya jambo dogo litakalowagusa watu wengi na Dunia ikakukumbuka daima.Mwaka 1914 Friedrich Von Wieser aligundua kanuni ya uchumi  aliyoiita ”Opportunity Cost”(gharama nafasi). Ukiwa na vitu viwili muhimu,ukachagua kimoja na kupoteza kimoja,hiko kimoja ulichokichagua ndio gharama nafasi (Opportunity Cost) ya kingine ulichokipoteza.Kiufupi kanuni  ya ”Opportunity Cost” inasaidia kufanya maamuzi magumu ukiwa na mahitaji ya vitu viwili muhimu na inabidi kwa wakati huo uchague kimoja huku ukikubali kupoteza kingine. Huyo ndio Friedrich Von Wieser kanuni yake ya “Opportunity Cost” ikamshawishi rais wa Australia wa wakati huo Count Heinrich Von Clam Martinic amteue kuwa waziri wa maswala ya fedha hiyo ni miaka mitatu tangu kugundua principle pendwa ya “opportunity cost”
         

   Wiki kama tatu zimepita tangu simba iamue kumrudisha mshambuliaji  Emmanuel Okwi.Emmanuel Okwi kipenzi cha washabiki na viongozi wa simba.Viongozi na washabiki wa simba walikua wakiumia sana wakimuona Okwi amevalia uzi wa njano na kijani.Viongozi wa simba wakaamua kufanya kila njia kumrudisha kipenzi chao Okwi.Ilikua ngumu kwa simba kwasababu kuu mbili.Kwanza OKwi alikua ana Mkataba wa Utata na Yanga lakini Ugumu zaidi ukaja kwa simba wenyewe ambao walikua wameshafikisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni ambao ni mahitaji ya kanuni ya shirikisho la mpira wa miguu Tanzania.Hapo ndipo Akili za Kaburu,Aveva na Hans pope zilipokua zinawasha.Hapo ndipo viongozi hao walikuwa wakifanya maamuzi huku wakikumbuka hekima za  mtunzi maarufu wa vitabu marekani Alfred A. Montapert. Alfred A. Montapert aliwai kusema  
“kila binadamu ana uhuru wa kuchagua,chaguo hilo ndio linaamua matokeo hakuna binadamu aliyewai au atakayewai kukimbia matokeo ya chaguo alolifanya”
 .Okwi sawa wanamtaka lakini nani atoke ili okwi acheze?.Hapo lazima uumize kichwa ili ufanye maamuzi sahihi.Kwizera na Kiongera wao ndio kwanza walikua wamesajiliwa hawa wawili wakawa salama.Shida ikabaki kwa Tambwe,Mossoti na Owino.Tambwe kwa upande wake alikua ametoka kuwa mfungaji bora wa ligi kuu Vodacom msimu ulioisha,hiyo ikawa pona yake kuenguliwa.wakabaki Owino na Mossoti,Hapa walitumia akili sahihi ilitumika kumtoa kafara Mussoti na Kumbakiza Owino kwani owino ndio roho ya beki ya simba.
             Tatizo lililopo Mossoti ni beki na okwi ni mshambuliaji.Ni wachezaji wawili tofauti uwanjani.Kazi ya Mossoti Okwi hawezi kuifanya na Kazi ya Okwi  Mossoti haiwezi.Ilo bado likawa tatizo kubwa kwa simba.Mpaka sasa wameshacheza mechi 2 na katika hizo mechi 2 wametoa sare mechi hizo zote mbili.Wamefunga mabao matatu na kufungwa magoli matatu.Na huo ukawa muda sahihi wa wachambuzi wa mpira Tanzania kuanza kuhoji  maamuzi ya simba kumtoa kafara mossoti na kumrudisha okwi kundini.Ukiangalia mabao mawili waliofungwa simba  yalitokana na uzembe wa mabeki.Wachambuzi wakaanza kuwa na mashaka na kuachwa kwa mossoti,wengi wanaamini makosa wanayofanya mabeki wa simba angekuepo mossoti yasingefanyika.Nakumbuka mtu mmoja tukiwa uwanja wa taifa wakati Danny Mrwanda anafunga goli akanifuata na kuniambia “unaona,simba wameamua kubaki uchi baada ya kuuza suruali waliyokua nayo na kununua shati”
              Lakini mimi bado naamini viongozi wa simba walisoma vizuri maandishi yaliyoandikwa na kalamu ya Friedrich Von Wieser kuhusu  kanuni yake ya “Opportunity Cost” .Ukiangalia simba ikicheza bado utaona ilimuhitaji okwi zaidi ya inavyomuhitaji mossoti.Okwi  kwa simba ni kama Messi kwa Barcelona au Ronaldo kwa Real Madrid.Hakuna goli la simba lililofungwa msimu hii pasipo msaada wa Emmanuel okwi ila lipo goli simba  wamefungwa  hata angekuwepo Mossoti wangefungwa tu.Okwi ndio moyo wa simba.ndie Mchezaji pekee wa simba anayeweza kuamua matokeo uwanjani.Wachezaji wa aina ya okwi ndio wale waingereza wanawaita” Match Winner”.Unafikiri ni timu gani Duniani isiyehitaji mchezaji anayeamua matokeo?.Unafikiri ibrahimovich atakataa Barcelona wakimwambia awape Cahil ili yeye apewe messi?.
           Kinachowagharimu simba ni kwa mabeki wao  wawili  chipukizi mugeveke na Isihaka kukosa udhoefu wa ligi.Isihaka na Mugeveke ni mabeki wazuri ila hawajiamini. Wakizoea ligi  naamini watakua miongoni  mwa mabeki bora  Tanzania na pia wanamsimbazi watamsahau mossoti.Kwenye swala la kati ya mossoti na okwi nani alikua muhimu msimbazi bado nipo pamoja na viongozi wa Simba,Hapa nawapa pongezi kwa kutumia vizuri kanuni ya ”Opportunity cost”  ambayo ilitungwa na hekima ya kalamu ya Friedrich Von Wieser.
 

                                   Allen kaijage
                              kaijagejr@gmail.com
                                   0655106767

0 comments:

Post a Comment