UTAFITI mbalimbali uliokwishafanywa unaonyesha kuwa magonjwa mengi ya
saratani (cancer) yanatokana na vyakula tunavyokula kila siku katika
maisha yetu. Katika siku za hivi karibuni, ongezeko la magonjwa haya
limekuwa kubwa kwa sababau vyakula vinavyosababisha magonjwa hayo,
ndivyo vinavyoliwa sana kuliko vile vinavyozuia.
Wiki iliyopita tuliwaorodheshea baadhi ya vyakula vinavyoaminika
kusaidia kuzuia magonjwa ya kansa ambapo wiki hii tunawaletea orodha ya
vyakula vinavyoaminika kuongoza kwa kuwa chanzo cha magonjwa hayo
hatari:
VYAKULA VYA KUKAANGA
Vyakula vingi vinavyotayarishwa kwa kukaangwa kwenye mafuta yenye moto
mkali huwa na madhara kiafya na miongoni ma madhara hayo ni pamoja na
kusababisha kansa ya kwenye mfuko wa uzazi. Vyakula hivyo ni pamoja na
chips na vyakula vingine vinavyopikwa kwa kukaangwa kwenye mafuta.
VYAKULA VYENYE CHUMVI NYINGI
Vyakula vyenye chumvi nyingi vimebainika navyo kusababisha kansa. Vile
vile inaelezwa kuwa chumvi huwa kama chakula kwa bakteria wa kansa
tumboni. Kansa ya tumbo inadaiwa kuua watu wengi nchini Japan kutokana
na jamii hiyo kupenda sana vyakula vyenye chumvi nyingi. Miongoni mwa
vyakula vyenye chumvi nyingi ni vile vya kusindika, kama vile nyama za
makopo, maharage, n.k
SUKARI
Matumizi mabaya ya sukari yanaelezwa kusababisha kansa. Kama tujuavyo,
kuna aina mbalimbali za sukari lakini sukari hatari zaidi ni zile
zinazowekwa kwenye vinywaji mbalimbali, zikiwemo soda, juisi za ladha ya
matunda ambazo huwa na kiwango kingi cha ‘fructose’ ambayo inaelezwa
kusababisha saratani ya kongosho.
Vile vile sukari kwa ujumla wake hairuhusiwi kutumiwa na mtu ambaye
tayari amegundulika kuwa na kansa kwa sababu chakula cha chembechembe za
saratani mara nyingi huwa ni sukari. Kwa matumizi mengine ya kawaida,
sukari inatakiwa kutumiwa kwa kiwango kidogo sana katika vinywaji au
vyakula tunavyotumia, tofauti na baadhai ya watu wanavyoweka sukari
nyingi ili kupata utamu zaidi.
NYAMA ILIYOIVA SANA
Upikaji wa nyama kwa muda mrefu na kwenye moto mkali (high
temperatures) husababisha aina fulani ya kemikali inayojulikana
kitaalamu kama ‘heterocyclic aromatic amines’. Utafiti wa hivi karibuni
uliofanywa na Chuo Kikuu cha Utah (University of Utah), umeonesha kwamba
watu wanaopenda kula nyama zilizoiva sana, wako hatarini zaidi kupatwa
na saratani ya njia ya haja kubwa (Rectal Cancer). Hivyo inashauriwa
unapopika nyama, usipike kwenye moto mkali na kuiva kupita kiasi.
POMBE
Unywaji wa pombe kupita kiasi nao unaelezwa kusababisha aina nyingi ya
saratani, kwa wake kwa waume. Aina ya saratani zinazodaiwa kusababishwa
na pombe ni pamoja na satarani ya mdomo, ini, utumbo na koromeo, ambazo
ndizo zinazoua watu wengi hivi sasa nchini Marekani.
NYAMA NA MAFUTA
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, umegundua
kwamba watu wanaopenda kula nyama kila siku wako hatarini kupatwa na
saratani ya utumbo kuliko wale wanaokula mara moja moja. Pia baadhi ya
mafuta ya wanyama na yale yanayowekwa kwenye ‘baga’ au ‘cheese’ huweza
kusababisha kansa.
Vile vile ulaji wa vyakula vilivyotengenezwa kwa kuchanganya na nyama
zilizosindikwa au kuhifadhiwa kwa matumizi ya muda mrefu husababisha
saratani pia. Vyakula hivyo ni pamoja na ‘soseji’ ambazo hupendwa na
watu wengi. Pia mikate ya nyama ‘hot dogs’ nayo ni chanzo cha magonjwa
ya saratani.
VYAKULA VYA UNGA MWEUPE
Vyakula vyote vinavyopikwa kutokana na unga uliokobolewa na kuondolewa
virutubisho vyake vyote na kuwa mweupe, vinaelezwa kuchangia magonjwa ya
saratani kwa kiasi kikubwa. Vyakula hivyo ni pamoja na ‘donati’
(doughnuts), maandazi, mkate mweupe, n.k
Mwisho, licha ya kuepuka ulaji wa vyakula vilivyotajwa hapo juu,
unatakiwa kuzingatia ulaji wa vyakula asilia vitokanavyo na mimea, mboga
za majani na matunda kwa wingi kila siku. Utaona kwamba adui mkubwa wa
afya zetu ni vyakula vyote vya kusindika na vile vya kutengenezwa
viwandani au vile ambavyo wakati wa utayarisjaji wake huondolewa
virutubisho vyake vya asili.
0 comments:
Post a Comment