Mgombea ubunge wa Jimbo la Kijitoupele kupitia Chama Cha ACT-Wazalendo, Zaitun Ali Khamis akihutubia mkutano wa kampeni kwenye Uwanja wa Kwamabata mkoani Mjini Magharibi, Zanzibar jana. Picha na Anthony Siame
Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo juzi kimehitimisha siku 10 za awamu ya kwanza kwa kutembelea mikoa minane ya Tanzania Bara, huku wakisisitiza kaulimbiu yao ya utu, uzalendo na uadilifu.
Mkoa wa kwanza ulikuwa ni Kigoma, mara baada ya kuzindua kampeni za udiwani na urais katika Viwanja vya Zakhem Mbagala, jijini Dar es Salaam huku kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe akiwa kivutio kwa wafuasi wa chama hicho.
Katika mkoa wa Kigoma walifanya mikutano kwenye majimbo matano, huku Zitto akiwahutubiwa wananchi wa Jimbo la Kigoma Mjini eneo la kiwanja cha Kawawa Ujiji. Katika mkutano huo Zitto alirudia kauli yake ya kuwataka wagombea ubunge wa chama hicho kipya, kujiandaa kwenda bungeni.
Hata hivyo, baada ya kuhutubia mkutano huo kiongozi huyo hakuweza kuambatana na mgombea urais kwenye ziara za kampeni, badala yake alirudi Dar es Salaam kwa shughuli maalumu za kichama.
Hatua hiyo ilisababisha mgombea urais, Anna Mghwira kuendelea kujinadi mwenyewe akiwa na mgombea mwenza wake, Hamad Yusuph Mussa, ambapo msafara wao mara kadhaa ulikumbana na kadhia ya kusimamishwa na wananchi wakitaka kumuona Zitto.
Mara ya kwanza msafara huo ulisimamishwa na wananchi wa Kijiji cha Bugaga, Kasulu Vijijini wakitaka kuonana na Zitto, hali iliyomlazimu Mghwira kushuka na kuwaeleza wakazi hao kuwa kiongozi huyo yupo pamoja nao, lakini kwa wakati huo alibanwa na majukumu ya chama.
“Zitto yupo ila ana majukumu ya kikazi na hapa siyo eneo rasmi la mkutano ,“ alisema Mghwira hata hivyo wakazi hao hawakuridhishwa na kauli hiyo, na kuamua kuchungulia kila dirisha la magari yaliyokuwa kwenye msafara huo ili wamuone Zitto.
Hali hiyo pia ilijitokeza katika mikoa ya Tabora na Rukwa, ambapo wakazi wa mikoa hiyo nao walishindwa kujizuia na kuamua kusimamisha msafara wa Mghwira wakitaka kumuona Zitto, na ilimlazimu mgombea urais kufafanua kwa nini Zitto hakuungana nao kwenye ziara hiyo. Hata hivyo, wananchi walionekana kutoridhishwa na majibu hayo na kuendelea kunung’unika.
Kubadili staili ya kampeni
ACT-Wazalendo kwenye baadhi ya maeneo waliyopita waliwaponda Chadema, lakini hali ilikuwa tofauti kwenye maeneo ambayo Chadema ina nguvu ambapo Mghwira alibadili ‘makombora’ na kuyaelekeza kwa CCM, akisema mwaka huu ni wakati wa vyama vya upinzani kukamata dola na kuipumzisha CCM, kwa kuwa kimeshindwa kuwatumikia Watanzania ipasavyo kwa zaidi ya miaka 50.
Lakini hali ilikuwa tofauti katika Jimbo jipya la Malinyi mkoani Morogoro, ambapo mmoja wa viongozi wa chama hicho alipomtaja kwa ubaya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, hali ilibadilika, ambapo baadhi ya wananachi waliohudhuria mkutano huo walisikika wakisema; “Huyu mzungumzaji anataka kutuudhi ni bora azungumzie sera za chama chake kuliko kumzungumzia kiongozi wetu mtarajiwa.”
Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza ni kutokuwa na ratiba ya mikutano mkoani Morogoro na kulazimika kurejea Dar es Salaam baada ya mkutano wa Malinyi.
katika ziara hiyo ya awamu ya kwanza hali iliyozua sintoafahamu kwenye mkoa wa Morogoro kwani mgombea huyo hakuwa na ratiba ya kufanya kampeni kwenye mkoa huku taratibu zikionyesha Lowassa ndiye aliyekuwa na kibali cha kufanya mkutano.
Hata hivyo, Mghwira alifanikiwa kufanya mkutano kwenye Jimbo la Malinyi lakini alishindwa katika Jimbo la Morogoro Vijijini kwa maelezo kuwa wagombea wawili hawawezi kufanya kampeni mkoa mmoja.
Hali iliyoawalazimu kuelekea Mkoa wa Pwani kufanya mkutano mmoja kisha kurudi Dar es Salaam kujipanga upya kwa awamu ya pili ziara yao inazotarajiwa kuanza kwenye mikoa ya Kaskazini tofauti na ratiba za awali iliyokuwa ikionyesha Septemba 18 watakuwa mkoani Shinyanga lakini wapo Dar es Salaam.
mwisho
CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment