Msemo mmoja kutoka kwenye maandiko matakatifu au wakati mwingine hata mitaani unasema kila mwanaume atakula kwa jasho lake. Ndio,ni kweli kila mbuzi atakula kutokana na urefu wa kamba yake na kila mtu anavuna kile alichokipanda. Mara nyingi tunashuhudia wazee wastaafu wa mashirika fulani ya Serikali au binafsi wakipokea mafao yao ya kazi waliyofanya kipindi cha nyuma.
Bastian Schweisteiger sasa ana miaka 31 ni miaka ambayo ni mara chache sana kumuona mtu wa miaka ya kariba hiyo kutoka ligi moja ngumu na kwenda ligi nyingine ambayo ina ugumu zaidi. Bastian ametoka ligi kuu ya Ujerumani akiwa ameshinda kila kitu ambacho kila mchezaji anapenda kushinda. Miaka 17 aliyokaa Bayern Munich alivuna kila taji na katika timu ya taifa ni mshindi wa kombe la dunia. Maisha yanataka nini zaidi ya hapo tena!!? Hakuna ila kwa Schweisteiger anaona bado nguvu ya kupambana na hamu ya kuendelea kuwa mshindi bado anayo.
Ametoka Ujerumani na kwenda moja kwa moja Uingereza ambako ligi yake ni ngumu na ina ushindani kila wiki. Kwa umri alionao wengi walidhani atashindwa kuendana na kasi ya ligi hiyo lakini babu huyo amekomaa na kuwafunga midomo waliyombeza. Ligi bado haijachanganya sana lakini Bastian ameonekana kuimudu vyema. Uwepo wa Schweisteiger kwenye kikosi cha Manchester United ni taswira tosha kuwa United hawafaidiki na uwepo wake ndani ya uwanja tu bali hata nje ya uwanja.
MWALIMU NA KIONGOZI
Kuna wachezaji wengi vijana wanapenda kuwa kama Schweisteiger na wanajifunza kupitia yeye. Bastian amekuwa mwalimu na kiongozi awapo ndani ya uwanja,kwa uzoefu wake anatoa mchango kwa wachezaji wengine ndani ya timu hasa kwa chipukizi. Amekuwa muhamasishaji na mpambanaji muda wote. Ni mchezaji anayejua mbinu mbalimbali za ushindi kwa timu yake,na pia ni mchezaji ambaye hana makuu ndani au nje ya uwanja. Mchango wake kwenye timu ni zaidi ya kupiga pasi sahihi nyingi au kuhangaika ndani ya uwanja,mchango wa Bastian kwenye timu unatokea pale timu inaposhindwa kujua cha kufanya na yeye hutoa ushauri na kurekebisha makosa machache kabla ya kocha hajafanya hivyo.
Bastian ni darasa tosha kwa wengine. Bastian ni silaha tosha ya kuumizia wengine ndani na nje ya uwanja. Upambanaji wake unatoa fursa ya wachezaji wengine kupambana ni kitu ambacho akiwezekani kumuona mtu mzima anapambana kwaajili ya timu halafu chipukizi ashindwe kufanya hivyo.
Schweisteiger alistahili kwenda timu ambayo haina presha ili afaidi matunda yake aliyovuna akiwa Bayern Munich sababu kwa umri wake ili kuwa vyema angeenda kuvuna mamilioni ya pesa Marekani au mashariki ya mbali. Kiu yake ya kuendelea kupambana na kushinda ndiyo iliyompeleka Manchester United,tumeshuhudia baadhi ya wachezaji wakishindwa kuendana na kasi ya Uingereza mfano Di Maria, Falcao,Kagawa na wengine wengi hao wote kiumri ni chini ya Bastian Schweisteiger lakini walikata tamaa mapema na hawakuwa na kiu ya kupambana ili kupata mafanikio kwenye timu waliyopo.
Mafao ya pensheni anayopata United alitakiwa ayapate Bayern Munich sababu pale ndipo alipofanya kazi kwa miaka mingi lakini mafao hayo yanaleta faida zaidi kwa United ambayo inahitaji muda zaidi ili irudi kwenye fomu kama zamani.
0 comments:
Post a Comment