Wananchi wa Jimbo la Muleba Kusini wakizungusha mikono wakiashiria kutaka mabadiliko walipokuwa kwenye Uwanja wa Fatuma, Muleba ulipofanyika mkutano wa kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, mkoani Kagera jana. Picha na Edwin Mjwahuz
Kagera. Mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa amesema ili kupata ushindi Oktoba 25, anahitaji kupata ushindi wa mabao matatu bila, akimaanisha Ukawa ipate rais, wabunge na madiwani.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Fatuma wilayani Muleba na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi, Lowassa alisema wakimpatia ushindi huo atapata watu wa kufanya nao kazi na kuwaletea wananchi maendeleo.
Lowassa ambaye alifanya mikutano mingine Karagwe, Kyerwa na Kamachumu, alirejea ahadi zake za ajira kwa vijana, elimu bure na iliyo bora, kilimo cha kisasa na kuanzisha benki ya mamantilie, bodaboda na wamachinga.
“Nitaziheshimu ahadi zangu na sitakuwa kama wengine wanaoahidi na kushindwa kutekeleza,” alisema Lowassa ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu.
“Siamini umati huu, nimepita maeneo mengi hali ni hivi hivi Mungu anipe nini kwa hali hii, hivi nina haja ya kuomba kura? alihoji na kuongeza:
“Naomba kura kwa kila Mtanzania mwenye nia njema, nataka kuwa rais kwa sababu nina uwezo wa kufanya hivyo na nimechoshwa na umaskini. Naomba kura tusaidiane kupambana na umaskini uliodumu kwa miaka mingi,” alisema. Huku akishangiliwa na wananchi alisema; “Tanzania ni taifa lenye uwezo, haliwezi kuacha rasilimali zake zikaenda kwa wageni tu. Nataka magoli matatu ili niweze kufanya kazi kwa uhakika.”
Akifafanua kauli hiyo, Lowassa alisema wananchi wanampenda na wanajitokeza kwa wingi katika mikutano yake ya kampeni, kuwaomba wahakikishe kuwa wanawachagua madiwani na wabunge wa Ukawa ili kukamilisha kile alichokiita, “magoli matatu”.
“Uwezo wa kuwaondoa wananchi katika umaskini ninao. Nikiwa rais, elimu itakuwa bure na bora na masilahi ya walimu yataboreshwa. Itakuwa mwisho kwa wanafunzi kukaa chini na nitaboresha kilimo na kuondoa ushuru wa mazao,” alisema.
Lowassa ambaye leo ataendelea na mikutano ya kampeni mkoani hapa, alisema Serikali yake itazalisha ajira za kutosha kwa vijana na kuanzisha benki kwa ajili ya maskini, hasa makundi ya waendesha bodaboda, mamantilie na machinga.
Wakati Lowassa akieleza hayo, waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye alikumbushia suala la Akaunti ya Tegeta Escrow, lililosababisha mgombea ubunge wa jimbo la Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka kujiuzulu uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mapema mwaka huu.
Sumaye alisema Tibaijuka alipewa mgawo wa mabilioni na akatamka kuwa Sh10 milioni ni hela ya mboga, kauli aliyosema si rafiki na umaskini wa Watanzania.
Kauli za Wananchi
Haji Buberwa mkazi wa Nshamba alisema, “Wanasema Dk Magufuli (mgombea urais CCM) ni mwadilifu lakini mbona ametuumiza. Amebomoa nyumba zetu mpaka sasa watu hawajalipwa fidia. Huyu hajawa rais lakini akisimama jukwaani anasema ‘ole wenu’, kama anakamia watu kiasi hiki akiwa rais itakuwaje?”
Helena Simon mkazi wa kijiji cha Kabale aliliambia gazeti hili kuwa tangu aanze kuishi Muleba, miaka tisa iliyopita hakuwahi kuona umati mkubwa wa watu kama wa jana ukihudhuriwa mkutano wa kampeni.
“Ahadi yake ya elimu bure ndiyo iliyonikuna kuliko zote, kutokana na watoto wetu kupata shida ikiwa ni pamoja na kukaa chini na michango kuwa mingi, kwa kweli kama akifanikisha hilo atakuwa rais wa maskini kama anavyosema,” alisema Helena. Denis Mutayoba mkazi wa Lubya alisema, “Pale alipozungumzia ajira kwa vijana na bodaboda ndiyo amenichanganya kabisa. Huyu mtu ni mchapakazi atatusaidia.”
Sumaye alisema ili chama kiendelee kuwa madarakani ni lazima kihakikishe kuwa kinatekeleza yale kilichowaahidi wananchi, lakini CCM imeshindwa kuleta mabadiliko, inang’ang’ania madaraka.
Wenje
Mgombea ubunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje alisema, “Nilichojifunza baada ya Lowassa kuhamia Chadema ni kuwa si vyema kukubali watu wazuie ndoto yako. Lowassa alikuwa na ndoto na nyinyi wananchi nawaomba mumchague kwani ataweza kutuvusha.”
Alisema, “Wakileta fedha zao zichukueni tu halafu siku ya kupiga kura mnaichagua Ukawa na kuachana na hao CCM. Eti Dk Magufuli anashangaa nchi haina dawa si akamuulize Rais Kikwete (Jakaya).
0 comments:
Post a Comment