Moshi. Wagombea udiwani wa Chadema katika kata 16 za Jimbo la Vunjo lililopo mkoani Kilimanjaro, wametangaza kutomuunga mkono mgombea ubunge wa jimbo hilo wa NCCR Mageuzi ambacho ni kati ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia.
Madiwani hao wametoa msimamo huo mbele ya Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo, baada ya jitihada za kuwatuliza kugonga mwamba, hivyo kuongeza orodha ya maeneo ambayo vyama vya Ukawa havijakubaliana hadi sasa.
Wakati hali hiyo ikiendelea Vunjo, mgawanyo wa jimbo la Itilima mkoani Simiyu baina ya Chadema na CUF umevunja mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa Chadema uliokuwa uzinduliwe na Mke wa mgombea urais wa chama hicho, Edward Lowassa, Regina Lowassa kama ilivyoripotiwa katika ukurasa wa 31 wa gazeti hili.
Katika tukio jingine mkutano wa mgombea mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji wilayani Nzega ulioripotiwa katika ukurasa wa 14 wa gazeti hili, ulivurugwa baada ya wagombea wa CUF na Chadema kugongana.
Tukio la Vunjo
Kutokana na mvutano uliopo, Ndesamburo alikutana na wagombea udiwani wa Chadema kwa faragha jana asubuhi lakini taarifa zilieleza wako tayari kumfanyia kampeni Lowassa lakini siyo Mbatia.
Ndesamburo alipotafutwa na Mwananchi jana, alithibitisha kuwapo kwa hali hiyo na kuongeza kuwa anamtafuta Mbatia ili kujadiliana na namna ya kushughulikia suala hilo.
Mbatia alipoulizwa, awali alisema aulizwe Meneja wake wa kampeni, Hemed Msabaha, baadaye alisema,“Nilishasema kamati tendaji za jimbo za Chadema na NCCR-Mageuzi zikae ziangalie vigezo vilivyosainiwa na makatibu wakuu wa Ukawa na kama vitaonyesha Chadema ndiyo inastahili kusimamisha madiwani kwenye kata zote 16 miye sina tatizo.”
Msabaha alisema katika waraka wa makubaliano ya ndani ya Ukawa uliosainiwa Agosti 13, mwaka huu, kulitolewa vigezo vitatu ambavyo ni matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, chama chenye diwani kipewe nafasi na chama kilichofanya vizuri uchaguzi wa Serikali za mitaa 2014.
“Uchaguzi wa Serikali za mitaa NCCR-Mageuzi tulifanya vizuri katika vitongoji na vijiji vya kata 10 dhidi ya kata mbili za Chadema, Kwa hiyo kata 14 zilikuwa hazina mgogoro,” alisema.
Msabaha alifafanua kuwa kwa kigezo hicho cha uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2014, NCCR-Mageuzi ilipewa kata 10 na Chadema mbili lakini kukawa na ubishani katika kata mbili. Hata hivyo, alisema baadaye Chadema waligeuka na kwenda na agenda mpya kwamba vyama hivyo vigawane sawa kata hizo
Wakizungumza na waandishi wa habari wagombea hao walidai kuchukizwa na hatua ya NCCR-Mageuzi kukiuka makubaliano ya kuachiana viti vya udiwani.
CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment