Facebook

Sunday, 1 March 2015

Wagonjwa wa Akili Hosptali ya Mirembe Watoroka



Wagonjwa wa akili katika Hospitali ya Mirembe iliyoko mkoani Dodoma wametoroka katika wodi zao baada ya kutokea mgomo wa wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi ya Mass inayolinda hospitalini hapo.
Mmoja wa wafanyakazi katika hospitali hiyo (jina linahifadhiwa) amesema kuwa leo asubuhi wagonjwa hao walitoroka katika wodi zao walizokuwa wamelazwa baada ya kutokea mgomo wa wafanyakazi wa kampuni ya ulinzi inayolinda hospitalini hapo.

Amesema jana asubuhi wafanyakazi hao waligoma kufanya kazi kutokana na kutolipwa mishahara yao kwa muda wa miezi mitatu na hivyo kukosekana kwa ulinzi wa kutosha kulikopelekea wagomjwa hao kutoroka.
“Ni kweli wagonjwa walitoroka baada ya walinzi wanaolinda hapa kugoma na jeshi la polisi lilifanikiwa kuwakamata na kuwarudisha tena wodini kwa sababu wengine walikuwa wameshaanza kurudi nyumbani kwao kwa miguu na wakati wanatoka Iringa,” alisema mfanyakazi huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa madai kuwa yeye siyo msemaji wa hospitali hiyo.

Hata hivyo amesema idadi kamili ya wagonjwa waliotoroka haijafahamika mpaka watakapokusanyika wakati wa kula ili waweze kuchukuliwa idadi yao kamili ya waliopo na wasiokuwepo.
Awali mganga mkuu wa Hospitali ya Mirembe Dk, Elasmus Mndeme alisema kuwa hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa ndiyo walikuwa wanafuatilia kwa ukaribu ili kujua ni wagonjwa wangapi waliokuwa wametoroka.
Kwa upande wake meneja wa kampuni ya ulinzi ya Mass Fredrick Masaka amesema mgomo wa wafanyakazi wake unatokana na kutolipwa na Hospitali hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu sasa ambapo katika kipindi chote hicho kampuni hiyo imeshindwa kuwalipa wafanyakazi wake mishahara.

Hata hivyo habari kutoka katika hospitali hiyo zinasema kuwa kutokana na tukio hilo kampuni hiyo ya ulinzi ya Mass imevunjiwa mkataba wake wa kulinda hospitali hiyo na badala yake imeingia mkataba na kampuni myingine ya ulinzi ya Embassy.
Awali habari zilizagaa mjini hapa kuwa madaktari katika Hospitali ya Mirembe wamegoma na hivyo kusababisha wagonjwa wa akili kuzagaa mjini habari ambazo hakuwa na ukweli wowote kwani waliokuwa wamegoma walikuwa ni walinzi wa hospitali hiyo.

0 comments:

Post a Comment