Vurugu zimezuka jana asubuhi katika
makao makuu ya jeshi la Polisi jijini Dar es
Salaam nchini Tanzania, muda mfupi baada
ya Mwenyekiti taifa wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo – Chadema,
Freeman Mbowe, kuwasili kwa ajili ya
mahojiano.
Mbowe aliitwa na polisi kwa ajili ya kutoa
maelezo kuhusiana na kauli aliyoitoa hivi
karibuni ambapo kiongozi huyo
alinukuliwa akihamasisha maandamano ya
wafuasi wa chama chake kupinga
kuendelea kwa vikao vya bunge maalumu
la katiba.
Awali vurugu hizo zilihusisha wafuasi wa
Chadema na askari wa kutuliza ghasia FFU,
lakini ghafla zikabadilika na kuwa kati ya
polisi na waandishi wa habari, hatua
iliyotokana na polisi kuanza kuwapiga
waandishi na kuwafukuza kwa kutumia
mbwa maalumu, kitendo ambacho
kimelalamikiwa na waandishi na hali
ilikuwa kama hivi.
Tukio la kupigwa kwa waandishi wa
habari, limetokea siku moja baada ya
Makamu wa Rais Dkt Mohammed Gharib
Bilal, kuvitaka vyombo vya ulinzi na
usalama likiwemo jeshi la polisi, kufanya
kazi kwa ushirikiano na wanahabari,
kutokana na pande zote mbili kuwa na
jukumu moja kuu la kuwatumikia
Watanzania.
Awali, askari wenye silaha waliwazuia
kuingia ndani ya ofisi za makao makuu ya
polisi, wabunge kadhaa wa Chadema,
akiwemo Mbunge wa Iringa Mjini
Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa
Iramba Mashariki Tundu Lissu, Mbunge wa
Ubungo John Mnyika na mwenzake wa
jimbo la Ilemela Ezekiah Wenje.
Hatua hiyo ilizusha majibizano baina ya
pande hizo ambapo wafuasi wa Chadema
walikuwa waking'ang'ania wabunge wao
waingie ndani kwa madai kuwa baadhi ya
wabunge hao wana nyadhifa muhimu ndani
ya chama na kwamba ingekuwa vema
waingie na kufahamu anachohojiwa
Mwenyekiti wao.
0 comments:
Post a Comment