Jinsi Kampuni ya Pan Africa Power Ltd
(PAP) ilivyoichukua Independent Power
Tanzania Ltd (IPTL) bure na kujichotea
Dola za Marekani 128 milioni kutoka Benki
Kuu ya Tanzania (BoT)
1. Muhtasari
KWA miaka ishirini sasa, wanasiasa
waandamizi na maofisa wa serikali,
makampuni ya nje na mawakala
wameipindishapindisha Sera ya Nishati ya
Tanzania na kupata faida kubwa kutokana na
shughuli za ushirikiano wa Sekta Binafsi na
Sekta ya Umma (PPP) walizounda.
Katika eneo hili, PPP mbili zinaonekana zaidi,
ile ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL)
na Richmond/Dowans. Tofauti ni kwamba,
wakati kashfa ya Richmond/Dowans ilifikia
kulazimisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri
Mkuu, Edward Lowassa (Februari 2008),
hakuna ambaye amechukuliwa hatua kuhusu
IPTL –ambao ni mradi wenye hasara kubwa
zaidi na umekuwa ukitengeneza umeme wa
bei mbaya ya kinyama kwa zaidi ya muongo
mmoja.
Mada hii bainifu inaelezea ilikotoka IPTL na
kuchukuliwa kwake ‘kisheria’ hivi karibuni na
Pan-Africa Power Tanzania Ltd (PAP). Ni
hadithi tahadharishi ya jinsi mahusiano kati
ya dola na sekta binafsi yanavyoweza
kutumika kwa manufaa ya wachache kwa
kuumiza walio wengi, kuleta hasara zenye
athari pana katika uchumi na uwezo wa
kuendesha uchumi kwa jumla.
Wahusika wawili muhimu wa IPTL ni James
Rugemalira wa VIP Engineering and
Management (VIPEM), Harbinder Singh Sethi
wa PAP na mlolongo wa makampuni mengine
ambayo yana rekodi chafu nchini Kenya.
Matokeo ya kashfa hiyo ni kuwa Sethi sasa
'anamiliki' mtambo wa kufua umeme wa
megawati 100 ambao hajawekeza hata thumni
na Rugemalira ametia mfukoni kiasi cha dola
milioni 75 (Shilingi bilioni 123 kwa viwango
vya sasa) kutokana na hisa zake asilimia 30
katika kampuni ambayo hajawekeza hata senti
tano.
Mada hii inafananua jinsi kati yao, na kwa
ushiriki wa viongozi wa Tanzania na maofisa
wa serikali, watu hao wawili walijichotea
kutoka BoT zaidi ya dola milioni mia moja
ishirini na nane za Marekani sawa na shilingi
za Tanzania bilioni mia mbili.
Kiwango hiki cha fedha kinaweza kujenga
barabara ya lami kilometa 217 kutoka Itigi
(Singida) mpaka Tabora Mjini. Kwa namna
nyingine, fedha hizi zingeweza kujenga
kipande cha barabara cha Ndundu – Somanga
cha kilometa sitini mara tatu na chenji
kubakia.
Kipande hiki kinalalamikiwa sana na wananchi
wa mikoa ya Kusini yenye utajiri wa gesi na
Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kabisa
kukimaliza lakini imeweza kujenga bomba la
gesi kutoka mikoa hiyo kuelekea Dar es
Salaam!
Mada hii bainifu inafafanua vianzio
nilivyovitoa katika makala ya hivi karibuni,
iliyochapishwa kwenye magazeti ya hapa
Tanzania; The Citizen kwa lugha ya
Kiingereza na Raia Mwema[1] na magazeti
ya Tanzania Daima na Mwananchi kwa
Kiswahili.
Katika makala hiyo nilihoji madai yasiyo ya
kawaida ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Frederick Werema, ambayo baadaye
yalirudiwarudiwa na wengine, kuwa fedha
iliyokuwa kwenye akaunti ya Escrow ya Tegeta
'Si fedha ya umma.' kwa vile vitabu vya
TANESCO vinaonyesha fedha ya escrow kuwa
ni akiba.
Nilisisitiza kuwa hapakuwa na amri ya
Mahakama Kuu kuhusiana na kutolewa fedha
ya escrow ilipwe kwa wadai, uongo mwingine
uliorudiwa na maofisa kadhaa waandamizi,
kama ambavyo unayakinishwa hapa chini.
Tatu, nilidai kuwa kuchukuliwa kwa asilimia
70 ya hisa za Mechmar kutoka IPTL na PAP,
dili linalohusisha kampuni isiyoeleweka ya
Paperlink na visiwa vya Virgin (British Virgin
Island) vya Uingereza, pia ilikuwa uporaji.
Hizi na hoja nyingine nilizotoa katika makala
zinaelezewa kwa kirefu zaidi hapa.
Mwaka 2009, Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Mashirika ya Umma, ambayo nilikuwa
Mwenyekiti wake wakati huo, ilitoa agizo kwa
Benki Kuu isitoe fedha katika akaunti hiyo ya
Tegeta escrow. Katika nafasi yangu ya
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha za
Serikali, hapo Machi 20 mwaka huu
nilimwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu
kufanya Ukaguzi Maalum wa kina wa akaunti
ya escrow ya Tegeta kwa nia ya kupata
undani wa jinsi ambavyo wamiliki wa IPTL na
PAP walifaulu kuiingia na kuchukua zaidi ya
nusu ya fedha zilizokuwamo humo.
Ukaguzi huo utajumuisha tathmini ya uhalali
wa PAP kuchukua hisa za IPTL kutoka
Mechmar na VIP Engineering.
Mada hii imegawanyika sehemu tatu. Sehemu
ya kwanza inatoa muhtasari wa ilikoanzia
IPTL na shughuli zake katika miaka ya 1990
hadi sasa. Tunajaribu kuonyesha jinsi uporaji
wa hivi karibuni wa akaunti ya escrow una
mizizi yake katika kuingiza sekta ya Nishati
katika mfumo wa soko katika miaka ya 1990,
ambako angalau mhusika mmoja muhimu
(Rugemalira) ni muhimu kwa muda wote huo.
Sehemu ya pili inaelezea habari za akaunti ya
escrow ya Tegeta na mikakati ya washiriki
wakuu waliohusika. Tunajaribu kuonyesha
jinsi wanasiasa kadhaa na majaji walivyotoa
udhamini wa wizi wa mchana kweupe wa
Benki Kuu.
Sehemu ya tatu inajadili matokeo ya uporaji
huo, na rushwa ya jumla katika sekta ya
nishati, kwa uchumi, watumiaji wa umeme,
serikali na wafadhili. Tutafikia tamati kwa
kuangalia masuala ambayo hayajatatuliwa
ambayo yatahitaji kuangaliwa ili mkasa wa
IPTL ufungwe kabisa. Kiambatanisho 1
kinatoa vianzio vya mada hii. Kiambatanisho
2 kinaorodhesha rejea za vyombo vya habari
na mitandao.
Sehemu ya Kwanza:
Kufikia IPTL na Pan-Africa Power (Ona
Kiambatanisho 1: 1994-..)
(2)
"Kama huu ni mfano wa ushirikiano wa nchi
za Kusini, basi ukoloni ulikuwa afadhali."
----------- Julius Nyerere
Mchango wa IPTL kwa Sera ya Nishati nchini
na ufanisi wake tangu 2004 umekuwa kwa
jumla ni hasi. IPTL ilihujumu juhudi za
serikali kupunguza utegemezi katika vianzio
vya maji na mafuta kwa kutumia utajiri wa
gesi asilia nchini. IPTL ilianzia katika
majadiliano ya ngazi za juu kati ya wanasiasa
wa Tanzania na Malaysia mapema miaka ya
1990. Waziri Mkuu Mahathir Muhammad
alipigia debe biashara za Malaysia katika
Afrika, ikiwemo Tanzania, kama njia ya
kuendeleza ushirikiano wa nchi za Kusini, na
kutatua utegemezi kwa nchi za Magharibi.
Hivyo IPTL mapema ilipewa kipaumbele na
serikali, hivyo kuweka kando kuendelezwa
kwa mitambo ya kutumia gesi.
Mnamo mwezi Mei 1997, benki za Bumiputra
na Sime (Singapore) ziliikopesha kampuni ya
Malaysia ya Mechmar zaidi ya dola milioni
100 za Marekani kujenga mtambo wa IPTL
eneo la Tegeta, Kaskazini ya Dar es Salaam.
Baada ya hapo, benki ya Bamiputra ilitangaza
mkopo huo kuwa hauna tija. Mnamo Agosti
2005, benki ya Standard Chartered ya Hong
Kong (SCB-HK) ilinunua deni hilo, lenye
thamani ya dola milioni 125; kwa dola 74
milioni. (3)
Kampuni ya Finland ya Wartsila ilijenga na
kuendesha mtambo wa IPTL ambao una vinu
10 vya ukubwa wa kati, vinavyotumia dizeli
kufua umeme wa megawati 100.
Ukizingatia kwamba IPTL inazalisha chini ya
asilimia kumi ya umeme wote unaozalishwa
hapa nchini, imepata tuhuma kubwa na
inazostahili mahakamani katika kipindi cha
miongo miwili iliyopita.
Mgongano wa muda mrefu kuhusu gharama
za ujenzi wa mtambo - na hivyo bei ambayo
Shirika la Umeme nchini (TANESCO)
inahitajiwa kulipa kwa umeme wake -
ilichelewesha kwa muda mrefu kuzinduliwa
kwa IPTL.
Badala ya kufua umeme kupunguza upungufu
uliokuwa unazidi wa umeme nchini, IPTL
ilitumia miaka ya 1997 hadi 2001 ikilumbana
na TANESCO, ikiwa ni pamoja na kufikishana
katika vyombo vya kimataifa vya usuluhishi
mwaka 1998. Mnamo Februari 2001, Kituo
cha Kimataifa cha Kutatua Migogoro ya
Uwekezaji (ICSID) kilifikia tamati kuwa IPTL
ilikuwa imejiongezea thamani yake kwa dola
milioni 23.5, hivyo kulazimisha upunguzaji
wa malipo ya uwezo wa mitambo (capacity
charges) ambayo TANESCO inahitajiwa
kimkataba kulipa kwa umeme wa IPTL.
IPTL mwishowe ikazinduliwa Januari 2002,
karibu miaka minane tangu kampuni hiyo
imeundwa, Lakini chini ya mwezi mmoja
baadaye mwenye hisa chache za IPTL, VIP
Engineering and Management (VIPEM)
iliwasilisha madai mahakamani kuwa kampuni
hiyo ivunjwe, kwa msingi kuwa VIP haijapata
asilimia 30 ya hisa za IPTL. Hadi 2013,VIP
ilikuwa inajaribu kufunga IPTL dhidi ya
upinzani wa Mechmar Bhd, kampuni yenye
hisa nyingi zaidi ya Malaysia (asilimia 70)
ikiwa ni 'mshirika' wa VIP.
Rugemalira, mmoja wa ‘vigogo’ wa IPTL, ana
tabia ya kutoa madai ya kipuuzi dhidi ya
washirika na washindani wake kibiashara.
Kutokana na nafasi yake muhimu katika
mkasa wa IPTL katika miaka 20 iliyopita, ana
bahati hakuwahi kumulikwa kwa karibu na
vyombo huru vya habari, ambavyo kwa
kawaida vinajitahidi kuonyesha rushwa katika
ngazi za juu inayohusisha wawekezaji kutoka
nje.
Ukinzani kuhusu IPTL katika miongo mmoja
uliopita ulilenga gharama kubwa za umeme
wa IPTL, kuwekwa kando kwa mradi wa
umeme wa Songas wakati IPTL ilipotokea na
uhusika wa wanasiasa wa ngazi za juu
kusukuma dili hilo –wakipinga ushauri wa
kitaalamu na upinzani wa TANESCO na
maofisa wa ngazi za juu serikalini.
Benki ya Dunia - iliyotoa fedha nyingi zaidi
kwa mradi wa Songas - pia iliikosoa IPTL,
kama lilivyofanya Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF), na Umoja wa Ulaya (EU) na
baadhi ya nchi wafadhili.
Kwa mujibu wa Gratwick na Eberhard
(2006:46), mwaka 2005, malipo kwa IPTL na
Songas yalifikia kiasi cha kushangaza cha
theluthi mbili ya mapato yote ya TANESCO.
(4) Kuharibu zaidi, mwaka uliofuata:
"..........wakuu serikalini, walifanya mzaha
uleule wa IPTL. Walitoa tenda ya kufua
umeme wa haraka kwa kampuni hewa (ya
mfukoni), Richmond Ltd, na kuiacha nchi
'gizani' kwa zaidi ya miezi mitatu na
kugharimu taifa mamilioni ya dola za
Marekani zilizoibwa na kuparaganyika kwa
uchumi (Brewin 2011). (5)
Mnamo mwaka 2005, benki ya Standard
Chartered (Hong Kong) *SCB) ilinunua deni la
IPTL wa dola milioni 74 kutoka kwa kampuni
wakala wa madeni ya ngazi ya pili wa
Malaysia iitwayo Donahatra,, ambako benki
ya Bumiputra ilikuwa imeliweka kama amana
isiyo na tija. Kuanzia 2005 hadi sasa, SCB-HK
ilijaribu bila mafanikio kupata jawabu la
mivurugano ya kisheria ya IPTL ili kuendeleza
mtambo bila matatizo na kulipa deni lake.
Walihujumiwa na VIP na PAP, ambao
walitafuta njia ya kuchukua mtambo huo bila
kulipa chochote ikiwa bado katika hatua ya
kufilisiwa.
Hapo Agosti 2007, serikali ilisimamisha
ulipaji wa gharama za uwezo wa kuzalisha
kwa IPTL kuhusiana na thamani ya mtambo
kwa gharama halisi za ujenzi. TANESCO ilidai
kugundua baada ya muda kuwa VIP ilikuwa
imeweka tu kiasi mfano cha hisa (sehemu ya
mtaji) katika mradi (sehemu ya hisa
inatumika katika kufikia malipo ya uwezo wa
mtambo). Hivyo TANESCO ikaona kuwa
ilikuwa ikilipa zaidi ya jinsi inavyotakiwa
kulipa.
Licha ya kuwa dhamira ya kubadilisha
mtambo wa IPTL kutoka mafuta kwenda gesi
ulipendekezwa tangu mwanzo, ulishindikana
kutekelezwa, hivyo kulazimisha gharama
zisizo za lazima kwa uchumi kwa kuagiza
dizeli hiyo nje na kwa watumiaji kwa umeme
ghali (angalia Timeline Desemba 28, 2009).
Songas inadai kuwa imeiokolea nchi
mamilioni ya dola za Marekani ambazo
zingetumika kununulia mafuta kutoka nje.
Licha ya kuwa kuwekeza katika matumizi ya
gesi kungepunguza gharama na kuongeza
faida kwa IPTL, kuagiza mafuta kunatoa
mwanya wa watu kujipatia fedha kwa
udanganyifu, kwa wahusika katika sekta ya
umma na sekta binafsi (angalia Timeline
Agosti 8, 2012). Makisio ya kiasi ambacho
ingegharimu kubadili mtambo wa IPTL kutoka
diseli kwenda gesi inatofautiana, ila tarakimu
ya dola milioni 20 za Marekani linatajwa
mara kwa mara. Kubadilisha kungeiokolea
TANESCO kiasi kinachokisiwa kufikia dola
milioni 840 katika uagizaji wa mafuta kwa
miaka 20 ijayo.
Kati ya miradi muhimu ya ubia wa sekta
binafsi na umma kwenye sekta ya Nishati,
IPTL na Richmond zinajitokeza kama makosa
ya gharama kubwa ambayo nchi ingefaidika
kutokuwa nayo. Lakini wakati Richmond
ilitwaa kichwa cha Lowassa, hakuna ambaye
amebanwa kuhusiana na hasara zilizotokana
na kashfa ya muda mrefu ya IPTL. Sehemu ya
pili inaangalia jinsi kati yao Harbinder na
Rugemalira walivyolitapeli taifa zaidi ya dola
milioni 128 (na zinaongezeka hadi dola
milioni 250).
Sehemu ya 2: 'Kununuliwa' kwa IPTL na
wizi wa akaunti ya escrow ya Tegeta
Akaunti ya escrow ya Tegeta iliundwa baada
ya TANESCO kuacha kulipia uwezo wa
mitambo ya IPTL mnamo 2006. Jinsi fedha
katika akaunti ya escrow ya Tegeta
zilipongezeka, ndivyo shauku ilivyozidi
miongoni mwa kundi fulani la
wafanyabiashara kuichukua kampuni hiyo
yenye migogoro, akiwemo Sethi. Akiwa
anajulikana kama mwekezaji kutoka Kenya
katika vyombo vya habari, Bw. Sethi kwa
yakini ni mzaliwa wa Iringa, mwaka 1958
(ona Kisanduku 1). Hapa tunaelezea jinsi
Sethi alivyochukua hisa kwanza za Mechmar
na halafu zile za VIP Engineering.
Hisa asilimia 70 za Mechmar
Kuhamishwa kwa hisa kutoka Mechmar
kwenda kampuni ya Piperlink ltd na halafu
PAP ilikuwa ni wizi mtupu. Ni kwa njia gani
ambako PAP ilichukua hisa za Mechmar katika
IPTL mwaka 2010 wakati Mechmar ikiwa
inafilisiwa? Sheria za nchi zote ulimwenguni
haziruhusu jambo hilo kutokea kwani ni
marufuku hisa za kampuni iliyo chini ya
muflisi kuuzwa au kufanyiwa biashara yeyote.
Au, kama wengine wanavyoamini,
wakurugenzi wa Mechmar waliwazidi akili
wasimamizi wa Malaysia, ikiwa ni pamoja na
Mahakama Kuu, na kufaulu kuuza hisa zao?
Anachoeleza Harbinder ni kuwa Mechmar
kwanza iliuza hisa zake katika IPTL kwa
kampuni kificho inayoitwa Piper Link,
ambayo ilizihifadhi, kwa sababu moja au
nyingine, huko British Virgin Islands vya
Uingereza.
Wapokeaji wa dhamana za Mechmar walidai
kuwa Mkurugenzi wa Mechmar, Datuk
Baharuden bin Abdul Majid alikiuka Amri ya
Mahakama ya Oktoba 4, 2010 kwa kuipotosha
Mahakama kwa kuingia makubaliano ya
kununua hisa (kwa dola milioni sita za
Marekani) na hao Piper Link Investments
mnamo Septemba 9, 2010. Wapokeaji
(waliokuwa wanaifilisi Mechmar) walifaulu
kupata hati ya Mahakama Kuu ya BVI (visiwa
hivyo) kuitisha vyeti vya uuzaji huo wa hisa
kwa msingi kuwa ulikuwa kinyume cha sheria.
Vyeti hivyo vya hisa vilifikishwa na muuzaji
kwa Mahakama Kuu ya BVI. (6) Hivyo ni kwa
njia gani Piper Link ilifaulu kuuza hisa zake
kwa PAP wakati ushahidi unaonyesha kuwa
wakurugenzi wa kampuni hiyo walikuwa
wamezuiliwa kukamilisha mpango huo
mnamo Aprili 2011? Ni hati zipi ambazo
wamiliki wa PAP walifikisha Wizara ya Nishati
na Madini kuthibitisha umiliki wa IPTL? Kwa
mujibu wa Sheria ya Fedha 2012, kifungu cha
29 wizara inatakiwa kuruhusu uuzaji baada ya
kukpokea cheti cha kuthibitisha kuwa
mahitaji yote ya kodi yametimizwa kutoka
Mamlaka ya Kodi Tanzania. Hati zinaonyesha
kuwa Pipelink ilinunua hisa za Mechmar kwa
shilingi milioni sita na baadaye kuuza hisa
hizo kwa PAP kwa dola 300,000. Kampuni
zote mbili, Mechmar na PiperLink zililipa
kodi ya ongezeko la mtaji siku hiyo hiyo
katika tawi la CRDB la Azikiwe mnamo
Desemba 5, 2013, siku moja baada ya Benki
Kuu kuachia fedha za akaunti ya escrow kwa
PAP.
Hisa asilimia 30 za VIPEM : Jawabu la
kitendawili cha IPTL kufungwa lilitengenezwa
na Harbinder na Rugemalira, kwa PAP
kununua hisa za VIP asilimia 30 za IPTL kwa
dola milioni 75 baada ya VIP kuondoa madai
ya mwaka 2002 katika Mahakama Kuu
kufunga kampuni hiyo. (Kiambatanishi 1).
Kuporwa kwa akaunti ya escrow: Katika
barua yenye tarehe ya Novemba 28, 2013
(isiyo na namba ya rejea) IPTL inaiomba
Benki Kuu kuhamisha dola milioni 22 na
shilingi bilioni nane kutoka katika akaunti ya
escrow kwendaa akaunti za PAP "kama
uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ya
Septemba 5, 2013 unavyoagiza."
Maofisa wa serikali na PAP wanasema kuwa
hukumu ya Septemba 2013 ya Jaji Utamwa J,
iliambatana na amri ya kuondoa fedha katika
akaunti ya escrow. Kwa jambo hilo,
mwandishi wa habari wa gazeti la Daily News
aliripoti matukio hayo kwa usahihi:
" ....Mnamo Septemba 5, 2013,, Jaji wa
Mahakama Kuu John Utamwa alimwamuru
Kabidhi Wasii Mkuu (mfilisi wa muda wa IPTL)
kutoa usimamizi wa shughuli zote za
kampuni, ikiwa ni pamoja na mtambo wa
umeme, kwa PAP." (7)
Hakuna mahali akaunti hiyo ya escrow
ilipotajwa. Kufuatilia hukumu ya Jaji Utamwa
ya Septemba 5, mapema mwezi Oktoba 2013,
maofisa wa TANESCO na IPTL walikutana
katika hoteli ya Kunduchi Beach. (8) Minute
za mkutano huo zinasomeka kwa uchache:
"..Mahakama Kuu imemwamuru Mfilisi wa
Muda kutoa mali zote za IPTL ikiwa ni pamoja
na mtambo ya umeme wa IPTL na amana
zinazopokelewa za akaunti ya escrow ya
Tegeta kwa Pan Africa Power Solutions (T)
Limited." (9)
Lakini ukisoma kwa uangalifu unaona kuwa
hapakuwa na amri katika hukumu hiyo kutoa
amana hizo 'zinazopokelewa.' Tofauti hii
haikuonekana au ilipuuzwa na wanasheria
katika Benki Kuu na Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Kama amri muhimu kama
hiyo ingetolewa, si ni wazi kuwa mwandishi
Faustine Kapama, ambaye kwa kawaida
anaandika inachosema VIPEM kuhusu suala la
IPTL, angeiandika katika habari yake
iliyonukuliwa hapo juu? Hoja isiyo sahihi
kuwa akaunti ya escrow iliamriwa kufungwa
na Mahakama Kuu ilichukuliwa na
Mwanasheria Mkuu na Gavana wa Benki Kuu,
Benno Ndulu.
Katika barua kutoka kwa Werema, ya tarehe 2
Oktoba 2013 kwa Katibu Mkuu, Hazina, Dk.
Servacius Likwelile, Mwanasheria Mkuu haoni
sababu yoyote kwanini Benki Kuu isihamishe
fedha za akaunti ya escrow kwa PAP na
Serikali isionekane kuyumba katika kutekeleza
"kile ambacho mahakama iliamua." (10)
Mnamo Septemba 10, 2013, E.S. Maswi,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini
alimwandikia Bw. Sethi katika nafasi yake
kama Mwenyekiti na Ofisa Mtendaji Mkuu wa
IPTL, kuwa, 'kufuatia mashauriano kati ya
TANESCO na ninyi" hakuwa na kipingamizi
kutia saini makubaliano ya kutoa fedha za
akaunti ya escrow ya Tegeta (ona Timeline,
Kiambatanisho 1). Hata hivyo mkutano
unaotajwa ulikuwa wa kawaida tu kati ya
maofisa wa ngazi za chini wa TANESCO bila
kuwepo watendaji wakuu wa VIP au PAP
wakihudhuria.
Hapa chini tunatoa wasifu wa wahusika
wakuu wawili wa VIP na PAP. Historia zao
wote wawili zinaonyesha kuwa walikuwa na
uwezo wa kubuni mkakati wa kuitoa IPTL
kutoka mikononi mwa mpokeaji wake rasmi
nchini Malaysia, kununua hisa za Mechmar
kwa kupitia dalali feki, kupata umiliki kamili
wa IPTL kwa kupitia ujanja wa kisheria,, na
mwishowe kudaka fedha ya akaunti ya escrow
kwa msaada wa maofisa wa serikali.
Kisanduku cha 1: Harbinder Singh Sethi ni
nani?
Harbinder Singh Sethi ni mmoja wa
wawekezaji vijana wenye asili ya Kiasia ambao
walitajirika miaka ya 1980 wakati Rais Daniel
arap Moi wa Kenya alipoanza kutengeneza
himaya yake binafsi ya biashara na majengo.
Akitajwa katika magazeti kama
mfanyabiashara wa Kenya na tajiri mkubwa,
Sethi alizaliwa na kulelewa Iringa, katika
Nyanda za Juu Kusini. Katika umri wa miaka
20 na ziada kidogo, Sethi na kaka zake wawili
Nota Singh na Manjit Singh walisajili kampuni
ya Ruaha Concrete Co. Ltd (Novemba 1977),
wote watatu wakitoa anuani ya S.L.P. 498
Iringa kama anuani yao.
Katika miaka ya 1980, Singh alihamia Nairobi
ambako alianza kuwa mbeba mifuko wa
mwanae wa kwanza Rais Daniel arap Moi,
Gideon. Anasemekana pia kuwa alikuwa rafiki
wa karibu wa Nicholas Biwott, mwanasiasa
na mfanyabiashara tajiri na mtu wa karibu wa
Moi.
Akiwa nao anasemekana kumiliki sehemu ya
mtambo ulioleta zogo wa megawati 47 wa
Westmont mjini Mombasa, akiwa na Mukesh
Gohil, Kamlesh Pattni, Bw. Gichuru,
Mkurugenzi Mtendaji wa KPLC, Bw. Mutitu,
Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Gideon
Moi (Oktoba 1997).
Uchunguzi wa Kroll ulionyesha kuwa Gideon
anamiliki mali kadhaa nchini Afrika Kusini..
Inaelezwa zipo mali zake ambazo
zimeandikishwa kwa kutumia jina la
Harbinder Singh Sethi. Mtanzania huyo wa
Iringa anaelezwa kuwa na mali 74
zilizooreshwa chini ya "mashirika
yaliyofungwa," ambayo yote yameandikishwa
kwa jina la Sethi.
Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Mashirika nchini
Kenya (1997) inataja kandarasi iliyotolewa
kinyume cha utaratibu na kampuni ya serikali
Kenya Pipeline Company kwa Ruaha Concrete
Ltd kujenga barabara ya kilomita tisa kufikia
mtamboni, ambako kulikuwa na
ucheleweshaji, kuongezeka kwa gharama, na
utekelezaji hafifu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu,
"Ruaha imesajiliwa katika kundi la wapaka
rangi na wajenzi wa barabara za ndani katika
mashamba makubwa."
Mhandisi msimamizi A.S. Kitololo alijiuzulu
baada ya kukataa kutia saini kuwa kazi
iliyozembewa imekamilika. Gharama ya mradi
wote ilipanda kutoka Ksh 197 milioni mnamoi
Februari 1995 hadi zaidi ya Ksh510 milioni
mwezi Juni 1998, ambako mradi huo
hatimaye ulikamilika.
Katika ukaguzi, barabara iligundulika kuwa
imejengwa kwa kiwango cha chini. Ripoti
ilitoa rai kuwa Ruaha Concrete iwekwe
kwenye orodha ya makampuni yasiyotakiwa
na ipelelezwe.
Kampuni nyingine ya Sethi, Pan African
Builders and Contractors, (PABCO), iliingia
mkataba na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
wa Kenya, kujenga nyumba, maghorofa ya
kupangisha na eneo la maduka Kitisuru jijini
Nairobi ambako NSSF ina nyumba za
kupangisha, kwa gharama ya Ksh2bilioni.
Tarehe iliyopangwa kumalizika ilikuwa Mei
2000, Mradi huo ulicheleweshwa baadaye na
kupunguzwa ukubwa wake kufikia
Ksh82.2milioni. Akikabidhi mradi huo,
malipo hayo hayakukamilishwa, na PABCO
ikaishtaki NSSF mahakamani kutaka ilipwe
Ksh1.3billioni.
Mnamo Agosti 31, 2010 Mahakama Kuu ilitoa
hukumu kuipa haki PABCO kulipwa
Ksh668milioni, pamoja na gharama na riba ya
fedha hizo. PABCO mwishowe ikakubali
kuishia katika malipo ya Ksh590milioni.
PABCO ikashindwa kulipa kwa wakati
unaohitajiwa kwa Mamlaka ya Kodi nchini
Kenya kodi ya kiasi cha Ksh260milioni.
Kutokana na biashara zake zenye giza, Kamati
ya Bunge ya Uwekezaji wa Umma (PIC)
ikamweka Sethi katika fungu la watu
wasioaminika, ikitoa rai asipewe kandarasi za
ujenzi kokote nchini. Kukamilisha picha,
kama mkurugenzi wa Hydrotanz Ltd, Sethi
pia ana hisa katika utafutaji wa mafuta na
gesi katika uwekezaji wa pamoja na Adhulink
Group, kampuni ambayo imetwaa kitalu cha
mafuta na gesi Mnazi Bay, kisiwa cha
Songosongo. Hydrotanz ipo kiwanja na. 887
mtaa wa Mrikau, Masaki jijini Dar es Salaam,
anuani moja na PAP.
Hivi karibuni, Sethi ameibuka na kuanza
kutoa misaada mbalimbali kwa jamii kama
sehemu ya uwajibikaji kijamii wa IPTL/PAP
kwa kutoa michango kadhaa: Sh. 11milioni
kwa SACCOS ya kundi la kwaya ya kanisani la
Kanisa la Mtakatifu Rita Wakashia lililoko
Kimara, Sh10 milioni kwa ujenzi wa kituo cha
polisi cha Mbweni-Malindi, Sh14.5milioni
kusaidia ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Petro
jijini na Sh.20 milioni kwa ajili ya Chama cha
Mchezo wa Riadha nchini (AT) kusaidia
kufanyika kwa mashindano ya riadha ya taifa.
(Jumla ya uchangiaji kwa uwajibikaji kijamii ni
sh.55.5milioni).
Kwa kificho pia, Sethi amekuwa akifadhili
baadhi ya vyama vya siasa nchini ili
kuhakikisha kwamba vinakaa kimya bila
kuhoji uporaji uliofanyika. Uchunguzi wa kina
wa matumizi ya vyama vyote vya siasa nchini
ukifanyika kwa kulinganisha na ‘forensic
investigation’ inayofanywa na TAKUKURU
utaweza kuibua kiasi cha fedha ambacho Bw.
Seth ametoa kwa vyama tajwa. Baadhi ya
viongozi wa vyama hivi ni marafiki wa Seth
wa muda mrefu.
Kianzio: Makubaliano ya wanahisa wa Ruaha
Concrete 1977, Ripoti ya Kroll (vipande),,
Taarifa ya Mkaguzi Mkuu (Mashirika) kuhusu
hesabu za Kenya Pipeline Company kwa
mwaka wa fedha ulioishia Juni 30. 1997
(ukurasa wa 75-78), "Masahihisho' ya NSSF
ya Kenya kuhusu taarifa za magazeti, Aprili 3,
2012; HYDROTANZ LIMITED, TANZANIA.
Ona rejea (Kiambatanisho 2) kwa viashiria
vya dili feki za kibiashara za Dethi nchini
Kenya, nafasi yake kama mbeba mikoba wa
Gideon Moi na uhusiano wake wa kibiashara
na Biwott na Pattni, na kuingia kwa
Hydrotanz yake katika utafutaji wa gesi.
Rais Moi aliwatumia Waasia nchini Kenya
kama washirika wake wakati akiwaingiza watu
wa kabila lake la wa-Kalenjin katika kina cha
mamlaka za kiuchumi na kisiasa. Wa-Kalenjin
waliingia katika miradi ya pamoja na wafanya
biashara wa Kiasia ambao mara nyingi
walikuwa wakipelekwa mbele kwa niaba ya
wa-Kalenjin ambao walikuwa wameupata
utajiri.
Waliofaulu zaidi walitumia dola kupata
kandarasi katika sekta ya umma kwa
kushirikiana na watu wa kabila la Kalenjin
waliokuwa wanamzunguka Rais Moi.
Licha ya kuwa Mtanzania kwa kuzaliwa,
Harbinder alikuwa mmoja wa wafaidika
wakuu wa ulaji rushwa rasmi wa enzi za Rais
Moi.
Kisanduku 2:
James Rugemalira ni nani?
James Burchard Rugemalira ndiye mhusika
mkuu wa Tanzania katika mkasa wa muda
mrefu wa IPTL. Akijiita kuwa ni mtaalamu
huru, mshauri wa kimataifa na 'mzalendo
mkubwa,' Rugemalira ni mwajiriwa wa zamani
wa Benki Kuu ambaye alistaafu mapema na
kusomea biashara katika Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam ambako alipata shahada daraja la
kwanza licha ya kuwa hakuwa mwanafunzi
mwenye kipaji kinachoonekana.
Katika nafasi yake kama Mkurugenzi wa
VIPEM Ltd, alikuwa mtu muhimu katika
kuwezesha mradi wa IPTL kuharakishwa
katika mikondo tofauti ya utawala nchini - na
hasa kwa vile ulikuwa ni mradi wa haraka.
Migongano ya kisheria ilizuia mradi huo
kuzinduliwa hadi miaka saba baada ya
makubaliano ya msingi (MoU) kutiwa saini.
Miradi anayoshiriki ubia (Tritel, IPTL) na
uwakala wa usambazaji (Windhoek, Heineken)
mapema au baadaye huishia mahakamani.
Mahakama za Tanzania zimesaidia kumbadili
Rugemalira kuwa mmoja wa matajiri
wakubwa sana hapa nchini. Wakati
Rugemalira anapopeleka madai katika
mahakama za hapa nchini dhidi ya wabia
wake wa miradi ya ubia au washindani wake
kibiashara, kesi zinafunguliwa dhidi yake na
washirika wake katika mabaraza ya usuluhishi
ya kimataifa. Kesi ya mwaka 2002 katika
Kituo cha Usuluhishi wa Migogoro ya
Uwekezaji (ICSID) ilitokana na jaribio la
kihuni la IPTL kutunisha gharama za mradi
huo wa umeme wa dharura.
Mkakati wake umekuwa kupeperusha bendera
ya kitaifa na kuhoji uhalali wa washiriki
kutoka nje katika kutatua madai tofauti, iwe
ni makampuni, wanasheria, mahakama, akidai
kuwa sheria za Tanzania ndizo peke yake
zinaweza kutumika katika masuala hayo.
Licha ya kuwa mshirika wa kutafuta haki
katika mabaraza ya usuluhishi ya kimataifa
hapo awali, mafanikio yake ya kuiparamia
akaunti ya escrow ilihitaji kwanza hatua ya
kupuuza kilichoamuliwa na ICSID.
Licha ya kuwa maamuzi ya hivi karibuni ya
mahakama nchini yameinua maslahi yake,
kwa zaidi ya miaka kumi alishindwa kuifikisha
IPTL kufungwa ili aweze kupata asilimia 30
yake ya hisa.
Kama ametia mfukoni dola milioni 75
alizokuwa anadai. basi huko kungoja
kumekuwa na faida ya kutosha, kwani
muongo mmoja uliopita angeambulia sana
sana dola milioni 30. 'Akihojiwa' juu ya dili
ya IPTL, Rugemalira alinukuliwa akisema
"Inahitajika Watanzania wenzangu wanione
kuwa ni mzalendo mkubwa kwa sababu
mkataba huo ulilenga zaidi maslahi ya taifa.
Nilikuwa nastahili kupata dola milioni 600
lakini nimepata dola milioni 75 ambayo ni
vijisenti tu.."
Chanzo: Cooksey 2003, Citizen Reporter
2014c, allafrica.com/
stories/2013/02281263.html, Daily News
Reporter, 17 March 2014. Ona rejea na
Kiambatanisho 2.
Baadhi ya Watanzania wasingeshangaa kama
'peanuts' zilizotajwa katika habari ya
Kiingereza ni sawa kabisa na alichosema kwa
Kiswahili, kuwa ni 'vijisenti' (kama
ilivyotafsiriwa hapa).
Mwezi Septemba 2008, upinzani ulianza
kuitaka serikali kununua mtambo wa Dowans
wa megawati 100 kupunguza makali ya
kukatika kwa umeme,, lakini serikali ikasita
kufanya hivyio, ikisema kuwa hainunui
mitambo wala bidhaa ambazo
zimekwishatumika.
Kama serikali ingenunua mtambo wa Dowans.
IPTL ingekuwa imeondolewa katika biashara
kwa sababu ya urahisi wa kumudu umeme wa
Dowans unaotokana na injini zinazotumia
gesi, na hadi sasa IPTL inafua umeme
kutumia mafuta mazito yanayoagizwa kutoka
nje, licha ya karibu miongo miwili ya ahadi
ya kubadilisha mtambo wa awali kuwa na njia
mbili, ya mafuta na ya gesi.
Kwanini ubadilishaji huo haukuwahi kufanywa
wakati ilikuwa wazi kuwa kwa maslahi ya
umma kubadilishwa kungewezesha kubana
malipo ya matumizi ya umeme kwa mtumiaji
wa kawaida na serikali inafichua tatizo kubwa
la kuweza kufanya kitu kwa pamoja, ambayo
ina athari ya kuzuia utekelezaji kimantiki wa
sera.
Hivi inavuka mpaka kusisitiza kuwa umeme
wa ghali mno wa mitambo isiyo na mshindani
ya IPTL ulikuwa unalindwa katika ngazi za juu
kabisa? Kama IPTL ilileta zogo lote hilo,
kwanini TANESCO iliendelea kuingiza
mamilioni ya dola za Marekani katika akaunti
ya escrow wakati ikiwa hailipi madeni
mengine mengi tu? Nani atakayelipia
ubadilishaji wa mtambo huo? Tutaacha hili na
masuala mengine yanayofanana nalo kwa
majadiliano.
Hadi sasa, VIP imekuwa ndiyo mfaidika mkuu
wa uporaji wa Benki Kuu, Kama Rugemalira
analipwa kikamilifu, atapata dola milioni 75
za Marekani kati ya dola milioni 122, au kiasi
cha asilimia 60 ya kiwango kilichotolewa
katika akaunti hiyo hadi sasa.
Lakini inasemekana bado kuna kiasi cha dola
za Marekani 128milioni zilizobaki katika
akaunti ya escrow ambazo Harbinder
anatazamia kuingiza mikono yake hapo punde
na siyo baadaye kidogo. Isitoshe, PAP,
ambayo dili zake za kitapeli zimempa
Harbinder mtambo wa IPTL bure, anakuwa
katika nafasi ya kuendelea kuvuna kodi za
pango (capacity charges shilingi bilioni 3.8
kila mwezi za kutumia mtambo huo) kama
IPTL itaendelea kuruhusiwa kuwa katika
shughuli zake kama kawaida, chini ya mfumo
uliopo hivi sasa kisiasa.
PAP imeelezea nia yake ya kuongeza uzalishaji
wa umeme wa IPTL mara tano, kubadilisha
kutumia gesi, na kupunguza bei ya umeme
hadi kufikia senti za Marekani sita hadi nane
kwa uniti moja.
Kwa sasa, wanadai kufua umeme katika
kiwango cha juu, wakitumia dizeli ya ghali,
huku wakipata malipo ya uwezo wa mtambo
yasiyofahamika kutoka TANESCO.
1. Matokeo: ubepari wenye vielelezo vya
Kitanzania
".......Hivyo, wananchi ndiyo walikuwa
walipaji wa bei ya mwisho. Hakuna umeme na
uzalishaji mali ni mdogo, giza totoro usiku na
gharama kubwa za uzalishaji wakati watu
binafsi na makampuni wakigharamia kununua
jenereta na mafuta kwa kuwasha taa na
kuzalisha." (11)
Ufanisi huu duni wa sekta ya umeme, ikiwa ni
pamoja na kujirudiarudia kwa makato
makubwa ya umeme kwa miaka 20 iliyopita,
na madeni makubwa ya TANESCO, ambayo
yanachukua sehemu si ndogo ya pato la taifa
kwa jumla, ni matokeo ya moja kwa moja ya
kashfa za IPTL na Richmond, pamoja na
udhaifu na rushwa katika utendaji wa kazi
TANESCO. (12) Hapa tunatoa rejea ya athari
za kashfa ya IPTL kwa washikadau muhimu.
Vyama vya siasa:
Kufichuliwa kwa tuhuma hizi kuhusu IPTL
kutazidi kuvuruga imani ya wananchi kwa
utawala wa Rais Jakaya Kikwete katika
kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa 2015.
Imani hiyo inaweza kuanguka kabisa kama
Sethi na Rugemalira wataruhusiwa kufurahia
uporaji wao wa mchana kweupe.
Tunatumaini na tunaamini kuwa wanasiasa wa
vyama vyote watahamasisha kusaidia
kuwafikisha waliotekeleza kashfa ya IPTL/PAP
mbele ya sheria mara watakapokuwa
wamepata vielelezo vinavyohitajika.
Kwa wakati huu, Rugemalira na Sethi bado
wanatamba na kutishia watu, kama
ilivyoonekana kwa vitendo vyao vya kupeleka
magazeti na wanasiasa mahakamani (mnamo
Julai 13, 2014 IPTL na PAP walimshitaki
mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila kwa
kuwaharibia sifa, wakitaka sh. bilioni 310
kama fidia).
Ni wakati sasa kwa vyama vya upinzani na
wapenda jema miongoni mwa wale walioko
katika chama tawala kuchukua msimamo wa
kimaadili dhidi ya uhalifu huu wa kiuchumi
uliofanywa na IPTL, PAP na wahalifu wenzao.
Watumiaji umeme wa majumbani:
Chini ya Mtanzania mmoja kati ya 50 anapata
umeme kutoka gridi, na weengi zaidi hukaa
maeneo ya mijini. Jumla ya kaya milioni 7.2
zinasemekana hazina umeme, hasa vijijini.
(13).
Bila uwazi zaidi na uwajibikaji katika sekta ya
umeme, watumaji wa nyumbani watazamie
mengine kama hayo katika miaka ijayo.
Biashara na uchumi:
Kwa mujibu wa OECD (2013), ukuaji wa
uchumi unaanza kupita uwezo wa uzalishaji
umeme:
"...........Kukua kwa wastani kwa uzalishaji
umeme (ambako kulikuwa asilimia 4.2 tu kwa
muongo uliopita) kunatofautiana na asilimia
7.1 ya wastani wa ukuaji wa uchumi na
asilimia 8 hadi 13 ya kukua kwa mahitaji ya
nishati kwa mwaka.'
Umeme usio na uhakika unavuruga biashara
za kila ukubwa. Kwa mfano, mwaka 2002,
kampuni ya Tanga Cement ilidai kupoteza kati
ya Sh80 milioni na Sh400 milioni kwa mwezi
kutokana na kukatwa kwa umeme. (14) Tafiti
za kimataifa mara kwa mara zinataja
kutokuwepo umeme wa kuaminika kama
kikwazo cha kupatikana faida katika biashara
nchini.
Kielelezo cha 1 kinataarifu juu ya maoni ua
wafanyabiashara kuhusu udhaifu katika
mazingira ya kufanya biashara nchini.
Kielelezo 1: Udhaifu wa mazingira ya biashara
nchini, 2008-2012
.......... Kimsingi mchoro unaonyesha
wasiwasi kuhusu umeme ukibaki tatizo la
kwanza kwa wafanyabiashara, ambako
halikubadilika katika nafasi yake kwa kipindi
chote cha takwimu hiyo. Maeneo mengine ya
wasiwasi yalikuwa yakipanda na kushuka, kwa
mfano hali ya barabara, upatikanaji wa maji,
usimamizi kodi, viwango vya kodi, fedha
(mikopo) na hata rushwa. Upatikanaji wa
umeme ulikuwa ndiyo udhaifu mkubwa
uliotajwa na wafanyabiashara kutoka 2008
hadi 2012.
Fedha za Umma na Bajeti:
Ripoti hii imedhihirisha matokeo mabaya ya
usimamizi mbovu wa sera katika sekta ya
umeme kwa bajeti ya Tanzania. Katika ripoti
ya nchi kuhusu Tanzania, Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF) linasema:
"Licha ya kuongezeka kwa asilimia 40 kwa bei
za umeme mnamo Januari 2012, nakisi ya
ulipaji wa TANESCO kwa wanaowapa huduma
ilifikia kiasi cha kukisia cha dola za Marekani
252milioni (takriban asilimia moja ya pato la
taifa) hadi kufikia mwisho wa Oktoba 2012.
( Ukurasa wa 5). Kuvurugika zaidi kwa hali ya
kifedha ya TANESCO kutafikia mwishowe
kuwa ni mzigo kwa bajeti na kunaweza
kusababisha makato ya nguvu ya umeme,
hivyo kuweza kuvuruga matumaini ya kukua
kwa uchumi." (ukurasa wa 6) (15).
Hasara ya Shirika la TANESCO kwa mwaka
sasa imefikia shilingi bilioni 300 mwaka 2013
kutoka hasara ya shilingi bilioni 5 mwaka
2011. Hasara yote hili anayeilipia ni
Mtanzania masikini kupitia bei kubwa ya
umeme na kodi lukuki anazolundikiwa kila
kukicha kwenye kila bidhaa anayotumia.
Kichangiaji kimojawapo muhimu katika
kuongezeka kwa pengo la bajeti nchini na
kukopa kwa dharura ni utawala mbaya na
rushwa katika sekta ya nishati.
Wafadhili:
Mara ya mwisho fedha za aina hiyo
zilipoporwa kutoka Benki Kuu ilikuwa ni
Akaunti ya fedha za mikopo ya kigeni (EPA)
iliyochelewa uliofanyika kabla na baada
kidogo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005
ambao uliingiza utawala uliopo madarakani
sasa.
Jibu la wafadhili kwa wizi huo wa wazi
lilikuwa wazi na la kusisitiza: serikali iajiri
kampuni binafsi ya uhasibu kuchunguza suala
hilo na kuwapeleka wahusika mahakamani. La
kwanza lilifikiwa, hata kama si la pili.
Hivi sasa, ni Balozi wa Uingereza peke yake
ndiye amezungumza hadharani kuhusu kashfa
iliyojitokeza - ambayo kimsingi ni mbaya
zaidi kuliko ile ya EPA katika athari zake
zitokanazo - na akasemwa vibaya bungeni kwa
sababu hiyo, kama inayoelezwa katika
Kiambatanisho 1 (Mei 7, 2014).
Mfadhili ambaye yuko karibu zaidi na suala
hili ni Benki ya Dunia, ambayo imetoa fedha
mara kadhaa kuitoa gizani kifedha TANESCO
hadi sasa, na sasa inatoa fedha kwa ajili ya
kuigawa TANESCO kuwa sehemu tatu
zinazojitegemea. Hapo mwezi Machi mwaka
huu, Benki ya Dunia iliidhinisha:
"Mkopo wa IDA wa dola za Marekani milioni
100 kwa ajili ya shughuli za sera ya pili ya
maendeleo ya sekta ya umeme na gesi,
ambayo itaisaidia Tanzania kuboresha
uthabiti kifedha wa sekta ya umeme, na
kuinua ushirikiano sekta ya umma na binafsi
kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme," (16)
Mkopo huu unaendeleza jadi ambako
wafadhili wanaitupia kamba TANESCO
kujiokoa badala ya kuhitaji kufumuliwa kabisa
kwa mpangilio wa ushirikiano wa sekta ya
umma na binafsi uliopo sasa ili kuwezesha
misaada hapo baadaye.
Kama mashirika ya maendeleo yatapuuzia
athari za kashfa hii kwa progamu
wanazosimamia, basi watapoteza sifa kama
wadau halisi wa kupiga rushwa na kuendeleza
utawala bora mbele ya macho ya jamii na
kuongeza kuungwa mkono kwa wale
wanaoona mashirika ya maendeleo ni sehemu
ya tatizo. Benki ya Maendeleo ya Afrika
yenyewe imeendelea kumwaga fedha kwenye
shimo lisilojaa la TANESCO.
Vyombo vya habari, asasi za jamii:
Tusingekuwa tunajadili undani wa kashfa hii
yenye utata mwingi hivi sasa kama magazeti
ya Nation Group, The Citizen na Mwananchi
yasingekuwa yameitoa habari hiyo mwezi
Machi.
Mara baada ya habari hiyo kutokea, PAP na
IPTL ziliyapeleka magazeti hayo mahakamani
zikidai kuwa makala hizo zililenga kutoa picha
kuwa IPTL na PAP ni 'matapeli, wahalifu,
wanaohusika na dili chafu zenye nia ya
kupata fedha kwa udanganyifu na ni watu wa
maadili hafifu."
Tunadhani kuwa maelezo haya yamepimwa
vyema. Iwapo uhamishwaji wa umiliki kutoka
Mechmar kwenda PAP ulikuwa ni kibadhirifu
(fraudulent), hakuna neno bora zaidi la
kuwaelezea PAP na makuwadi zaidi ya wao
kuwa ni waporaji, wanyonyaji na matapeli
waliokubuhu.
Rugemalira na Sethi wanaweza kujitambulisha
bila kupingwa kama wazalendo na wawekezaji
halisi, wakiwa wamepania kufanya jambo
linalofaa kwa jamii, wakati ni wasanifu wa
tatizo tulilo nalo la umeme, inaonyesha ni
kiasi gani vyombo vya habari na asasi za
jamii nchini ni dhaifu katika kutoa habari za
ulaji rushwa mkubwa.
Hivi hakuna hata mmoja kati ya waandishi
wetu wa habari aliyehangaika ku-'Google'
Harbinder Singh Sethi kudhihirisha kuwa
haiba yake nchini Kenya ni ya msukaji, tapeli
aliyekubuhu? Unatafuta bila mafanikio kwa
makala au tahariri katika moja ya magazeti
yetu ambayo angalau inahoji nafasi ya Bw.
Rugemalira na alichofanya katika ujanja wote
huu? Kwa miaka mingi, gazeti la serikali la
Daily News, limekuwa likitoa anachoeleza
Rugemalira katika suala la IPTL.
Na ziko wapi asasi za kijamii zinazochukua
suala hilo katika mwelekeo wa 'kupinga
rushwa' au kufuatilia 'utawala bora'?
Kwenda mbele:
Ili kufanikiwa, mikakati hatarishi ya Sethi na
Rugemalira inahitaji ushiriki wa dhati au wa
kujitolea miongoni mwa wanasiasa
waandamizi, maofisa wa serikali, majaji na
vyombo vya habari. (17) Watuhumiwa wakuu
walioko mstari wa mbele ni pamoja na wale
ambao, tangu The Citizen na Mwananchi
waanze kuelezea habari ya IPTL/PAP,
wametetea kiliochofanyika au kuwasema
wakinzani wake kwa nguvu. Nje ya
Rugemalira na Sethi, orodha hiyo ni pamoja
na:
* Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema,
ambaye anadai akaunti ya escrow siyo fedha
za umma, na kuitaka Hazina kutokusitasita
kuhusu kutoa fedha ya akaunti ya escrow.
Anatuhumiwa kuiagiza Mamlaka ya Kodi
kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
katika malipo ya uwezo wa mtambo.
* Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo ambaye alidai bungeni
kuwa wabunge wa upinzani wamehongwa
kuinua suala la IPTL. (Wangehitaji vipi
kuhongwa ili kuibuka na habari tamu kama
hiyo?)
* Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen
Masele, ambaye alimtuhumu balozi wa
Uingereza kuwataka wafadhili na mashirika
yasiyo ya kiserikali kuchukua msimamo
kuhusu kashfa iliyoanza kujitokeza.
* Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliachim Maswi, ambaye alisema
taarifa wanazotumia wabunge wa upinzani
kuhoji uhalali wa kutolewa fedha za akaunti
ya escrow 'siyo sahihi.' Alidai kuwa benki ya
Standard Chartered ya Hong Kong siyo
mhusika katika tofauti za IPTL na TANESCO.
Alikuwa mtekelezaji mkuu wa kuhakikisha
kuwa fedha za escrow zinaondolewa Benki
Kuu.
* Utawala wa TANESCO, ambao hadi sasa
haujatoa ukinzani wowote kuhusu
kuondolewa kwa maamuzi ya ICSID kuwa
upande wake na uporaji wa akaunti ya
escrow,ambao kiasi fulani kilitakiwa
kurudishwa TANESCO ambayo iko taabani
kifedha.
Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno
Ndulu, ambaye alichukua tahadhari kubwa
kuzuia lawama kwa Benki Kuu kuhusiana
na madai yoyote ya ziada kuhusu IPTL
baada ya kufungwa kwa akaunti ya escrow
ila akashindwa kueleza kwanini hakuhoji
kuondolewa fedha za akaunti kwa kurejea
uamuzi wa usuluhishi wa ICSID na uamuzi
wake (Februari 2014) unaounga mkono
dai la TANESCO kuwa walilipa kupita kiasi
kinachohitajiwa kwa uwezo wa mtambo
wa IPTL.
* Mfumo wa Mahakama: Mahakama nchini
zinatoka katika mkasa wa IPTL zikiwa na
haiba ya sura mchanganyiko, Licha ya kuzuia
kwa miaka mingi juhudi za kila maara za
kuifunga kampuni hiyo, tangu alipoteuliwa
Mfilisi wa Muda, Rugemalira anaonekana
kuweza kuitumia Mahakama Kuu atakavyo.
Hivi Jaji Utamwa ana lipi la kusema kuhusu
utumiaji mbaya na PAP wa hukumu yake ya
mwezi Septemba kupora akaunti ya escrow?
Pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(PCCB) hivi sasa inaichunguza PAP/IPTL kwa
kuombwa na Waziri Mkuu (baada ya agizo la
PAC la tarehe 20 Machi 2014, kwa nia ya
kutoa tathmini kama kilichofanyika katika
mada hii ni rushwa.
Katika wakati uliopita, PCCB iliwakingia
lawama wanasiasa waandamizi, licha ya kuwa
kulikuwa na ushahidi mkubwa wa kuwaingiza
hatiani (18) Kama PCCB inataka kuinua
mwonekano wake katika jamii itafanya
uchunguzi wa kina ya kilichojiri katika suala
hili kabla ya kufikia mahitimisho yoyote.
Maswali kadhaa ambayo hayajajibiwa:
Hivi imekuaje kwa mtambo wa kati wa kufua
umeme ulete mgogoro mkubwa kisheria na
katika vyombo vya habari kwa karibu miongo
miwili na ukaruhusiwa kuvuruga vipaumbele
vya uzalishaji umeme nchini?
Hivi imekuaje mradi huu uchangie kutokea
kwa hasara kubwa kwa sekta ya umma na
binafsi? Mradi huu ni kielelezo kimojawapo
cha utawala mbovu katika sekta ya nishati
hapa nchini.
Kama mkasa wa muda mrefu wa IPTL haufikii
tamati yake hivi karibuni, upotevu wa kasi wa
fedha za umma (na za wafadhili) utaendelea,
kuvuruga zaidi udhaifu wa ushindani wa
uchumi wa Tanzania. Tunahitimisha na
maswali kadhaa ambayo hayajajibiwa:
* Kwanini TANESCO iliilipa IPTL kwa muda
mrefu hivyo bila kuhoji malipo ya uwezo wa
mtambo?
* Ni kwa muda gani mtambo wa IPTL ulikuwa
haufanyi kazi, na ni wakati gani ulipoanza
tena? Nani alilipia matengenezo yake wakati
ukiwa haufanyi kazi?
* Ni wapi uhusiano wa Rugemalira na
Harbinder ulipoanzia?
* IPTL ilikuwa inafanya nini na mapato yake,
ni sehemu gani ya deni lake ililipwa?
* Ni fedha gani au hisa zilizobadilishwa kati
ya PAP na Mechmar/Piper Link? Nani
anamiliki Paper Link kama siyo Harbinder
Singh Sethi? Nani anammiliki mwanahisa
mwingine wa PAP anayeitwa Simba Trust?
* Ni fedha kiasi gani imebaki katika akaunti
ya escrow, kama ipo?
* IPTL inafanya kazi? Nani anaimiliki? Hali
yake ya fedha ikoje? Inapata fedha za
uendeshaji wa mtambo hivi sasa? Ni kiasi
gani? Nini kimekubaliwa na
TANESCO? REJEA
1. Zitto Kabwe, 2014 "Akaunti ya escrow ya
Tegeta ni fedha za umma," The Citizen, Dar es
Salaam, Juni 29,
2. Kipande hiki kinatoa muhtasari wa Cooksey
(2002) kuhusu suala hilo katika chapisho
Afrika Kusini, "The Ugly Malaysians?" n.k.
katika Institute for Black Research, Durban
3. Punguzo hilo la dola milioni 51 za
Marekani linaelezea thamani halisi ya sasa ya
deni hilo na uhatarishi uliopo katika kununua
dhamana ya tija duni. Hadi sasa, SCB-HK
haijalipwa chochote kutoka IPTL.
4. Gratwick, Katherine Nawaal na Anton
Ebehard (2008), "Kifo cha mfumo wa kawaida
wa urekebishaji wa sekta ya umeme na
kuzuka kwa masoko mchanganyiko ya
umeme," katika jarida la Energy Policy, 36
(10): uk. 3948-3960
5. Degani, Michael "Umeme wa Dharura:
Muda, Maadili na Umeme katika Tanzania
baada ya Ujamaa," na Brewin, David
"Rushwa, waliochelewa..." katika jarida la
Tanzania Affairs 99: uk 15-19
6. Barua na viambatanisho kutoka kwa Lim
Litt na Andrew Heng, wafilisi rasmi wa
Mechmar, kwa Zitto Kabwe, Mwenyekiti,
Kamati ya Hesabu za Serikali, Machi 28, 2014
7. Faustine Kapama 2014, "PAP yaanza
mipango ya kupunguza gharama za umeme,"
Daily News, Aprili 5
8. Walikuwa: John Kabadi, Meneja
Mwandamizi, Mipango/Mikakati, Heromini
Shirima, PDEO (?), na Stella Rweikiza, Ofisa
Mkuu Sheria (wote wa TANESCO) na Joseph
Makandege, Mwanasheria wa Kampuni, na XX
(wote wa IPTL). Tarehe halisi ya mkutano huo
haiko wazi katika minuti za mkutano huo.
9. Minuti za mkutano wa maofisa wa
TANESCO na IPTL, Hoteli ya Kunduchi Beach,
October 2013 (uk. 1-2)
10. Barua namba ya rejea GCC/E.80/6/65
(mkazo umeongezewa)
11. OECD 2013, Mapitio ya Sera za
Uwekezaji, Tanzania, Agosti 6, uk, 101
12. Wakati wa kuandika mada hii, Mkurugenzi
Mtendaji wa zamani wa TANESCO alikuwa
mahakamani, akikabiliwa na mashtaka ya
kuingiza kampuni ya mkewe katika kashfa ya
manunuzi. TANESCO pia inahusika na kashfa
ya ununuzi wa mafuta ambayo inaihusisha
IPTL (ona maelezo).
13. TANESCO ina kiasi cha watumiaji wa
umeme 900,000, ambao asilimia 80 wanaishi
mijini.
14. George Sembony 2012, "Wafanyabiashara
wamechoshwa na kukatika umeme," Citizen,
Desemba 28
15. IMF 2013, Ripoti ya nchi, Tanzania, uk. 6
16. Lazaro 2014 (Kiambatanisho 1 Machi 21,
2014)
17. Kwamba hawa ni wengi inathibitishwa na
jinsi maofisa wa vyeo vya juu wanavyoingia
na kutoka kwa haraka wakati Sethi akiwa
katika anga zake kwenye hoteli ya Sea C liff,
ambako anakaa mara kwa mara anapokuwa
jijini Dar es Salaam.
Zitto Kabwe, Mb
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC)
0 comments:
Post a Comment