Zaidi ya miongo sabini baada ya kuanza
uhusiano wa kimapenzi, Vivian Boyack na
Alice "Nonie" Dubes wamefunga ndoa.
Boyack, 91, na Dubes, 90, walifunga ndoa
rasmi Jumamosi iliyopita, limeripoti gazeti la
Quad City Times.
"Sherehe hii ilikuwa ifanyike siku nyingi
sana," amesema mchungaji Linda Hunsaker
wakati akifungisha ndoa hiyo iliyohudhuriwa
na marafiki wachache na baadhi ya
wanafamilia wa maharusi.
Wawili hao walikutana katika mji waliokulia
wa Yale, Iowa, nchini Marekani. Baadaye
walihamia mji wa Davenport mwaka 1947,
Boyack akifanya kazi ya ualimu, huku Dubes
akifanya shughuli za kihasibu.
Dubes amesema wameishi maisha mazuri
pamoja, katika miaka yote hiyo na wameweza
kutembelea majimbo yote 50 ya Marekani, na
ya Canada, na pia kutembelea Uingereza
mara mbili.
"Tumekuwa na wakati mzuri," amesema
Dubes.
Boyack amesema inahitaji mapenzi ya dhati
na kujituma kuweza kuendeleza penzi kwa
miaka 72.
Rafiki wao wa muda mrefu Jerry Yeast, 73,
amesema alikutana nao zamani wakati
akifanya kazi nyumbani kwao akiwa kijana
mdogo.
"Nimewafahamu wanawake hawa maisha
yangu yote, na ninakwambia, ni wa kipekee,"
Yeast amesema.
Jimbo la Iowa lilianza kuruhusu ndoa za
wapenzi wa jinsia moja mwaka 2009.
Wanawake hao wamesema hawajachelewa
kuanza ukurasa mpya katika maisha yao.
0 comments:
Post a Comment