Safari ya mbunge wa zamani wa Kigoma
Kaskazini kwa tiketi ya Chadema,
Zitto Kabwe kurejea bungeni imeanza
rasmi baada ya kiongozi huyo wa
chama kipya cha ACT-Wazalendo
kuchukua fomu za kuwania kuongoza
jimbo la Kigoma Mjini.
Uamuzi huo wa kulitaka jimbo hilo
unathibitisha kauli zake ambazo
amekuwa akizitoa kwa muda mrefu kuwa
hatarudi tena Kigoma Kaskazini kwa
kuwa alishawatimizia kila kitu na
haoni sababu za kuwawakilisha tena
wananchi wa eneo hilo.
Kauli yake iliibua ubashiri kuwa
Zitto anataka kubadilishana jimbo na
mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter
Serukamba, uvumi ambao aliukanusha
akisema hadhani kama CCM inaweza
kupata jimbo Kigoma.
Zitto, ambaye alijiondoa Chadema
baada ya kukiuka katiba kwa kufungua
mashtaka dhidi ya chama hicho,
hakufanya mbwembwe wakati akienda
kuchukua fomu kwenye ofisi za ACT
Ujiji jana, badala yake aliita
viongozi wa kata na matawi bila ya
kutaarifu vyombo vya habari.
“Nimeamua kugombea ubunge wa Kigoma
Mjini ili niwatumikie ndugu zangu
ambao wamekuwa wakipata tabu katika
kupigania haki zao za msingi ambazo
walistahili kuzipata kama ilivyo
katika mikoa mingine,” alisema Zitto
alipoongea na mwandishi wa Mwananchi
kwa simu.
“Nitakapokuwa mbunge wa Kigoma Mjini
nitahakikisha barabara za mitaani
zinapitika katika kipindi chote cha
mwaka, nitahakikisha watu wanaacha
tabia ya kulima mashamba katikati ya
mitaa na makazi, lakini
nitahakikisha kila mmoja anajiunga
na mifuko ya kijamii ili kujiwekea
akiba ya uzeeni pamoja na kupata
huduma ya matibabu, elimu na
nyinginezo zinazopatikana kwa
kutumia mifuko hiyo.”
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Kamati
ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), alisema bonde la Mto Luiche
bado halijatumika ipasavyo kuzalisha
chakula kwa wingi.
“Nakusudia kuibana Serikali ijenge
skimu ya umwagiliaji maji ili
wakulima walime kilimo cha mpunga
kwa mwaka mzima bila kupumzika,
jambo ambalo litainua uchumi wa
wakulima na kuongeza chakula hapa
Kigoma,” alisema.
Kuhusu umeme wa gridi ya Taifa,
Zitto alisema lazima upatikane ili
kusaidia jitihada ya ujenzi wa
viwanda vya kusindika mazao ya uvuvi
na kilimo kwa kuwa hivi sasa mji wa
Kigoma Ujiji unategemea umeme wa
jenereta ambao hauwezi kuendesha
shughuli za viwanda, hali
inayochangia mkoa kuendelea kuwa
masikini licha ya kuzungukwa na
rasilimali nyingi.
Katibu wa ACT wa Jimbo la Kigoma
Mjini, Azizi Ally alisema Zitto
alichukua fomu hiyo jana kwa malipo
ya Sh100,000 mbele ya viongozi 72 wa
kata na matawi kutoka jimboni humo.
“Kwa hali ya sasa Kigoma Mjini
inahitaji kupata mbunge anayeweza
kufuatilia mambo kwa kina ili kuleta
maendeleo ya wananchi baadala ya
yule anayekwenda bungeni kujifunza,”
alisema Ally.
“Watu wanakabiliwa na kero
mbalimbali kama ubovu wa barabara za
mitaani, uhaba wa umeme wa uhakika
unaoweza kuendesha viwanda vikubwa
na vidogo, pamoja na wengi kufanya
kilimo cha kujikimu zaidi.“
Zitto alitofautiana na uongozi wa
juu wa Chadema uliomtuhumu kuwa
alikuwa amefanya uasi na kwamba
alishaanzisha chama kingine akiwa
ndani ya chama hicho kikuu cha
upinzani na kusababisha avuliwe
nyadhifa zote, ikiwamo ya unaibu
katibu mkuu.
Hata hivyo, wakati Chadema
ikijiandaa kumjadili na pengine
kumvua uanachama, Zitto alifungua
kesi akitaka mahakama imuamuru
katibu mkuu wa Chadema ampe nyaraka
za mwenendo wa vikao vilivyomvua
madaraka na kuomba amri ya kuzuia
vikao hivyo visimjadili.
Katika hukumu ya kesi hiyo, mahakama
ilitupilia mbali hoja zake, uamuzi
uliotafsiriwa kuwa umefungua njia ya
kutimuliwa kwake kwa kitendo cha
kufungua kesi mahakamani kinyume cha
katiba.
Mkazi wa Gungu mjini Kigoma, Zuberi
Mrisho alisema ujio za Zitto
kugombea Ubunge wa jimbo hilo
utaamsha ari ya wananchi
kujiandikisha kwa wingi katika
Daftari la Wapigakura na kujitokeza
kupiga kura tofauti na chaguzi
zilizopita.
“Mwaka 2010 Vijana wengi hatukupiga
kura hapa kwa sababu tulikosa imani
na baadhi ya wagombea wa nafasi
mbalimbali, lakini kwa ujio wa Zitto
sasa nina hakika wengi tutajitokeza
kupiga kura ili tupate viongozi
makini kwa maslahi ya mji wetu,’
alisema Mrisho.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment