Uzinduzi wa kipindi cha 'Big Brother Africa' umeahirishwa kwa muda baada ya moto mkali kuzuka katika jengo linalotumika kama studio za kuendeshea kipindi hicho jijini Johannesburg.
Kipindi hicho, kilichokuwa kianze siku ya Jumapili, sasa kimeahirishwa, wakati watayarishaji wakitafuta jengo mbadala.
Hakuna aliyeumia katika tukio hilo, na sababu
hasa za chanzo cha moto hazijajulikana, huku uchunguzi ukiendelea.
Washiriki kutoka nchi 14 walitarajiwa kushiriki katika makala haya ya
tisa. Kipindi hicho kingefanyika kwa siku 91 kabla ya mshindi mpya
kutajwa, kuchukua taji kutoka kwa mshindi wa mwaka jana, Dilish Matthews
kutoka Namibia. Mshindi wa mwaka huu atapewa zawadi ya dola 300,000,
sawa na alizochukua mshindi wa mwaka jana.
Watayarishaji wa kipindi
hicho Endemol na M-Net wamesema juhudi za kutafuta studio na nyumba
nyingine itakuwa ngumu katika kipindi kifupi kutokana na "miundombinu ya
hali ya juu ya kiufundi" ambayo, "haiwezi kupatikana mara moja".
Kipindi hicho tayari kilipata 'kwikwi' baada washiriki kutoka Ghana
kukabiliwa na matatizo ya kupata visa na hivyo raia wa Ghana wanaoishi
Afrika Kusini kuchukua nafasi zao.
Ushiriki wa Rwanda, kwa mara ya
kwanza, pamoja na Sierra Leone ulilazimika pia kutofanyika. Kipindi hiki
kilikuwa kioneshwe barani Afrika kupitia televisheni za satellite. Big
Brother Africa kimekuwa kipindi maarufu tangu kilipoanza mwaka 2003, na
kimetoa washindi kutoka Tanzania, Angola, Nigeria, Namibia, Zimbabwe na
Afrika Kusini. Mshindi wa kwanza, Cherise Makubale, (Pichani) alitokea
nchini Zambia.
0 comments:
Post a Comment