Facebook

Wednesday, 13 May 2015

ARSENE WENGER NA HADITHI YA UNYWELE WA MFALME MVI.

"Mbinu hufuata mwendo". Kama mbinu zako ni mbovu basi na mwendo wako utakuwa mbovu, ila kama mbinu zako ni nzuri basi na mwendo utakuwa mzuri.
Huu msemo unanikumbusha hadithi moja ya mfalme wa zamani , ambaye aliwaaminisha wananchi wake kupitia mbinu yake isemayo " Mwenye mvi kichwa kizima , ndiye anastahili kukalia kiti cha Ufalme" , Na kwenye nchi yake yeye peke yake ndiye alikuwa na mvi kichwa kizima. Na katika kutilia mkazo wa mbinu yake alitangaza wazi siku moja ikitokea Mfalme akawa na unywele hata mmoja mweusi basi huyo hatastahili kuendelea kuwepo kwenye kiti cha Ufalme wa nchi hiyo.
Mbinu yake ilikuja kuonekana mbovu na dhaifu siku ambayo mke mdogo wa Mfalme ambaye alikuwa ametengwa kisa ya kuzaa mtoto mlemavu wa Macho. Mke huyo alipata wasaa wa kuwa na Mfalme Siku Moja , ndipo alipogundua kuwa Mfalme ana Unywele Mmoja mweusi . Ndipo alipoenda kwenye baraza la wazee kuwaambia na baraza lilifanya jitihada na kudhihirisha ukweli , na huo ndiyo ukawa mwisho wa utawala wa Mfalme mvi. Na yule Mama alimtoa Nje mtoto wake mwenye ulemavu wa macho, aliyekuwa na Mvi pia kichwa kizima na alimpeleka kwenye baraza la wazee , na yule mtoto aliapishwa kuwa Mfalme.
Kwa kipindi hiki tulichopo sasa hivi, bodi ya Arsenal na Arsene Wenger sitosita kuwafananisha na Mbinu za Mfalme Mvi.

Mwaka 1999 ndiyo mwaka ambao Arsenal walianza mpango wa kujenga Uwanja Mpya wa kisasa, tena mkubwa kuzidi ule wa Awali ( HIGHBURY) Uliokuwa na uwezo wa kubeba watu 38,500 . Mpango wa kujenga Uwanja mkubwa wenye uwezo wa kubeba watu Elfu 60+ Lilikuwa jambo jema kwa klabu na Mashabiki wa Arsenal.Mpango huu ulienda Sambamba na Kuifanya Arsenal kuwa Timu yenye Uchumi mkubwa Duniani.
Mipango hii ilienda sambamba na Sera mpya za usajili.
Timu ilitakiwa kusajili wachezaji vijana .
Hii Sera ilizalisha watu kama kina Johan Djourou, Gael Clichy, Nicklas Bendtner.

Hii sera ilikuwa nzuri sana ila ilikuwa na mapungufu mengi. Mapungufu haya ndiyo yaliifanya Arsenal kwenda miaka mingi bila ya kuchua kombe , na ndiyo maana nikafananisha sera hii na sera ya Mfalme Mvi.

KIVIPI SERA HII ILIKUWA SABABU YA UKAME WA ARSENAL?

1: Uwiano mbaya wa umri wa wachezaji.  Safari ya Ukame wa Arsenal ilianza mwaka 1999!!.  Wakati bodi ikipitisha sera za kujenga uwanja mpya, sera ya kuifanya Timu kuwa na Uchumi mkubwa, kwa kubebwa na Sera kuu ya kusajili vijana wachanga kwa kutumia kiasi kidogo cha Fedha, na kwa kutegemea Academy.Lakini sera hii ya kusajili vijana ilichelewa sana kuanza kutekelezwa, Mwaka 2004 ndipo sera ilianza kutumika rasmi. Hii ndiyo iliwagharimu sana Arsenal, Kama Sera hii ingeanza mwaka 1999 &.2000 kungekuwa na wachezaji waliokomaa ambao wangechukuwa nafasi ya kile kikosi cha dhahabu 2004. Kumsajili mchezaji wa miaka 16 na unategemea huyo mchezaji azibe pengo la kina Patrick Vieira akiwa na miaka 18 . Vipi kama ungemsajili 2000 akiwa na miaka 16? Mwaka 2006 angekuwa na miaka 22 huyu tayari angekuwa ameshafika hatua ya ukomavu .Na kuwa na njaa ya mafanikio na kwenye umri wa miaka 22 mchezaji huwa amefikia hatua ya ushindani na siyo ya kujifunza

Ndiyo maana kile kizazi kichanga kilichosajiliwa 2004-2006 Kina Alex Song, Theo Walcot, Abou Diaby, Carlos Vela, Johan Djourou, Gael Clichy, Nicklas Bendtner hakikuweza kufuata nyayo za mafanikio za wakubwa wao kina Henry.Kwa sababu kilikuwa na mambo mengi ya kujifunza kuliko kushindana.

2: Wakati kina Vieira, Gilberto Silva na Flamini wanaondoka hakukuwa na watu wa kuziba nafasi hizo mpaka pale ilipochukuwa muda mrefu kumpata Song.
Sawa Sera ya Timu ilikuwa kusajili vijana kuepukana na gharama za klabu lakini kulikuwa na ugumu gani kwa Arsene Wenger kusajili mchezaji wa nafasi hiyo muhimu?

3: Kuna mchango mkubwa sana kwa Ryan Giggs, Paul Scholes kumalizia maisha yao ya kisoka pale Manchester United. Hii iliwafanya kuwa kioo kwa wachezaji Vijana, ambao walipagana zaidi kufikia mafanikio makubwa. Hii ilikosekana kwa Arsenal.Hakukuwepo na kina Vieira, Henry , Pires, Bergkamp, Martin Keown ambao wangekuwa kioo kwa vijana wachanga ili kupitia wao kungewafanya wachezaji vijana kupigana zaidi ili kufikia Mafanikio Makubwa.

Kwa hadithi hii ya Bodi ya Arsenal na Arsene Wenger naifananisha sana na hadithi ya unywele wa Mfalme mvi.Arsene Wenger hakuona Unywele wake mweusi, ndiyo maana sera yake ya mara ya kwanza yakuwaleta vijana wakina Thierry Henry, Patrick Vieira, Nicolas Anelka, Kolo Toure, Fredrik Ljungberg.Aliamini sera hiyo hiyo itatumika kwa kina Walcot , Carlos Vera bila kuwatengenezea mazingira mazuri ya mafanikio.Ndipo wakina Mourinho walikuja na kuchukuwa Kiti cha Arsene Wenger.

Ahsanteni.

Written by: Martin Kiyumbi 0657 7710 77

Edited by : Ngod

0 comments:

Post a Comment