JUMAMOSI jioni, John Terry aliwaongoza mabeki wa Chelsea kukabiliana na mchezaji mnene na mwenye nguvu zaidi duniani, Saheed Adebayo Akinfenwa ambaye umbo lake linaleta kichekesho kikubwa kwa mashabiki wa soka.
Chelsea ilishinda mabao 3-2 wakati huu ikijiandaa
na michuano mbalimbali msimu ujao, lakini walilazimika kukabiliana na
Akinfenwa ambaye alikuwa katika ubora wake.
Hadi wakati anatolewa uwanjani dakika ya 60,
Chelsea ilikuwa imekufa 2-0 huku Akinfenwa akimuhenyesha Terry na
wenzake. Hata hivyo baadaye walifunga mabao matatu ya haraka haraka
yaliyobadili matokeo ya mechi wakati Akinfenwa akiwa nje ya uwanja.
Licha ya umbo lake kubwa, Akinfenwa aliyezaliwa
jijini London Mei 10, 1982 anadaiwa kuwa na kilo 86 tu lakini ana uwezo
wa kubeba uzito wa kilo 180 ambazo ni mara mbili na uzito wake.
Tayari Fifa wamempitisha kama mchezaji mwenye
nguvu zaidi duniani huku wakimuingiza katika Video zao za michezo ya
kompyuta huku umbo lake likionekana kuwa kivutio kwa mashabiki wengi
duniani.
Mlinzi wa klabu ya Vale iliyo daraja la kwanza
England ambaye alicheza timu moja na Akinfenwa Northampton, Dan Jones
anaeleza kwamba ni kujisumbua tu kujaribu kutumia nguvu kumkaba mchezaji
huyo.
“Soka lake halibadiliki tangu tulipokuwa
Northampton. Anapenda kuuficha mpira miguuni na inajionyesha wazi kwamba
hana mpango wa kukimbia nao. Anapenda kukaa na mpira mguuni huku
akiwasukuma walinzi kwa nguvu zake.” Anasema Jones.
“Hauwezi kushindana naye kwa nguvu kwa sababu
utaishia kumfanyia rafu au atakutupa tu. Inabidi utumie akili sana
wakati wa kumkaba. Inabidi usitumie nguvu nyingi sana kumkaba.”
“Wakati mwingine akipata mpira tunamuachia tu na
kuangalia anachotaka kufanya kwa sababu tunajua hawezi kukimbia, yeye
huwa anaaangalia watu wanaofungua nafasi tu.” Anasema Jones.
Akinfenwa amedai kwamba hajawahi kucheza katika
Ligi Kuu ya England kwa sababu makocha wamekuwa wakiliogopa umbo lake na
kudhani kwamba atakuwa mzigo tu uwanjani kitu ambacho sio cha kweli.
“Nadhani naweza kutisha Ligi Kuu. Nadhani niko
sawa na Didier Drogba tu. Sijacheza madaraja ya juu kwa sababu kuna
mtazamo fulani wa jinsi ambavyo mwanasoka anapaswa kuwa na mimi
sionekani kuwa hivyo,” anasema Akinfenwa.
“Sitaki kuonekana mjinga lakini nimefunga zaidi ya
mabao 150 katika mechi 300. Waulize walinzi au makocha wa timu pinzani
watakwambia jinsi nilivyo balaa.” Anasema staa huyo.
0 comments:
Post a Comment