Monday, 28 July 2014
"UKAWA rudini bungeni katiba haiandikwi Kibanda maiti wala Ubungo...."- Wassira
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na Sera),
Stephen Wassira ameshauri wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba wanaojiita Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), kurejea bungeni na kama
maoni yao ni ya wananchi, wasubiri wakati wa
kura za maoni.
Aidha, Wasira pia amemtaka msemaji wa Ukawa,
Tundu Lissu kuwaomba radhi mashehe na
maaskofu ambao ni wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba, kwa kudai ni wanachama wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wamekuwa
wakihongwa chakula, chai na fedha katika
nyumba za viongozi.
Alitoa maoni hayo jana kwenye mdahalo wa
Tanzania Tuitakayo uliolenga kuangalia ‘Nani
anataka kuwazuia Watanzania kupata Katiba
Mpya,” akiwa sambamba na wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba na
Lissu.
Alisema kama Ukawa wanaungwa mkono na
wananchi, ni vyema watumie nafasi hiyo kurejea
bungeni na kujadili rasimu ndani ya Bunge na
baadaye wasubiri wananchi waamue.
“Kama wanachokiamini Ukawa kuwa wako
pamoja na wananchi, kwanini wanakwenda kwa
wananchi kabla hawajamaliza kazi. Warejee
bungeni tujadiliane na kumaliza kazi halafu
wakatushitaki kwa wananchi, tuone Ukawa
watapata ngapi… kwanini tuandikie mate na
wino upo?”
Aliongeza: “Kama ni muundo wa serikali mbili au
tatu utajulikana bungeni.”
Wasira alisema Ukawa wanatakiwa kujua kuwa
sheria inataka Katiba kuandikwa ndani ya Bunge
na si sehemu nyingine na kushindwa kufanya
hivyo ni kukwamisha mchakato huo ambao
umefikia hatua ya tatu.
Alisema watu waliokataa kurudi bungeni ndio
wanaowazuia Watanzania kupata Katiba mpya
sababu Katiba haiwezi kuandikwa nje ya Bunge.
“Wanaokataa kwenda bungeni ndio wavurugaji,
Katiba haiwezi kuandikwa Kibanda Maiti au
Ubungo, inaandikwa ndani ya Bunge Maalumu.”
Awali, Lisu alisema kati ya wajumbe 201
walioteuliwa na Rais kama wajumbe wa Bunge,
169 ni wanachama wa CCM wakiwamo mashehe
na maaskofu na wamekuwa wakihongwa katika
nyumba za mawaziri.
Katika hatua nyingine, Wasira amewataka
wanasiasa kuacha kusemea wananchi masuala
ya mchakato wa Katiba kwa kuweka mawazo
yao na kuwa CCM haipingi mawazo ya
wananchi.
“Wanasiasa kutoka vyama vya upinzani wanadai
kuwa tunapinga mawazo ya wananchi kama
yaliyowekwa kwenye rasimu ya Katiba, lakini
wamekuwa wakiweka mawazo yao kwa kisingizio
kuwa ni mawazo ya wananchi."
Naye Profesa Lipumba, alisema rasimu inapaswa
kuboreshwa na kujadiliwa kulingana na rasimu
ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Taifa ya
Mabadiliko ya Katiba na kutuhumu CCM kuwa
ndio wanaovuruga mchakato kwa kutaka
kupitisha mfumo wa serikali mbili.
Kwa upande wa Lissu alidai kuwa machakato wa
Katiba umekuwa ukiendeshwa kwa kupendelea
wajumbe wengi wa CCM.
Imeandaliwa na.......
Mdau wa BantuTz
0 comments:
Post a Comment