Facebook

Tuesday, 26 August 2014

Watuhumiwa wa Ugaidi wachafua hali ya hewa kortini.


KIONGOZI wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI),Sheikh Farid Hadi Ahmed (43), ametoa
shutuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi akidai kuwa limewafanyia ukatili kwa kuwapiga, hali inayowafanya baadhi yao wajisaidie damu.

 
Sheikh Farid alitoa madai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa, wakati kesi ya tuhuma za ugaidi inayowakabili ilipokuwa ikitajwa.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Njike,alidai kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa,upelelezi haujakamilika na wanaomba hati ya kuwachukua washtakiwa saba, akiwamo Sheikh Farid kwa ajili ya mahojiano.


Hakimu Riwa alikubali maombi hayo na kuahirisha kesi hadi Septemba 3, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Hali hiyo ilisababisha washtakiwa kuomba kutoa maelezo yao.
 

“Mheshimiwa wametuomba kwenda kutuhoji tena, mara ya kwanza tulipohojiwa, polisi hawakutumia ustaarabu wala ubinadamu, ni ushenzi na ukatili, walituhoji uchi wa mnyama na kutupiga."
 

“Kiongozi Mkuu wa Uamsho, Sheikh Mselem Ally Mselem, mwenye heshima, mfasiri wa Kur’ani, alinihadithia alipohojiwa walimfanya nini, tumepigwa na hatukutibiwa, magereza wamejitahidi, lakini hawana nyenzo za matibabu."

“Watu wameumizwa vibaya, mengine hayasemeki, wanajisaidia haja ndogo damu wiki moja hadi mbili, tunaomba tufanyiwe uchunguzi wa afya zetu, ipo siku mahakamani italetwa maiti."
 

“Tumekamatwa sababu hatutaki Muungano,hiyo ndiyo kesi ya msingi, tunawaambia ukweli katika mihadhara na watu wanatuamini, tunaomba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iletwe mahakamani tuijadili,” alidai Sheikh Farid.

Mshtakiwa wa 12, Salum Alli Salum, aliomba mahakama imwite daktari ili aweze kufanyiwa uchunguzi wa afya yake kwani ameingiliwa kijinai kwa nguvu.
 

“Mheshimiwa tunalazimishwa kutoa maelezo wanayoyataka wao, wanatuingilia kinyume cha maumbile, wanaingiza majiti, chupa,
wengine wanavuja nyuma, kama unaweza hakimu twende faragha nikakuonyeshe."


“Askari ameniingilia kisha akaniingiza jiti mpaka likakatika, kungekuwa na sehemu ningekuonyesha, Jeshi la Polisi la kwanza
kuvunja sheria, waliofanya madhila haya wanawatukanisha Watanganyika na kufanya waonekane wabaya,”
alidai mshtakiwa huyo.


Baada ya washtakiwa hao kutoa malalamiko yao, mahakama iliwaahidi washtakiwa hao waende wakahojiwe na muda wote watakuwa katika mazingira salama.Sheikh Faridi na wenzake 19 wanashtakiwa kwamba kati ya Januari 2013 na Juni 2014 maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikula njama ya kutenda kosa la kuingiza watu nchini kufanya ugaidi.
 

Shtaka la pili linawakabili washtakiwa wote, wakidaiwa kuwa katika kipindi hicho walikubaliana kumuingiza Sadick Absaloum na Farah Omary nchini ili kushiriki kutenda makosa ya ugaidi.
Katika shtaka la tatu linalomkabili Sheikh Farid, anadaiwa kati ya Januari 2013 na Juni 2014 maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, huku akijua ni kosa,alimuingiza nchini Sadick na Farah kufanya ugaidi.

 
Sheikh Farid pia anadaiwa kuwahifadhi Sadick na Farah, huku akijua watu hao walitenda vitendo vya kigaidi.Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Jamal Swalehe, Nassoro Abdallah, Hassan Suleiman, Anthari Ahmed, Mohammed Yusuph, Abdallah
Hassani, Hussein Ally na Juma Juma.
Wengine ni Saidi Ally, Hamisi Salum, Saidi Amour Salum, Abubakar Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Amir, Rashid Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Nassoro na Said Sharifu.

 
Wakati huohuo, kesi nyingine ya ugaidi inayomkabili Kiongozi Mkuu wa JUMIKI, Sheikh Mselem Ali Mselem na mwenzake, Abdallah Said Ali, imeahirishwa hadi Septemba 3, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa kwa sababu Sheikh Mselem hakuwapo


                                       Katemi Methsela
                                           

0 comments:

Post a Comment