Serikali imeanza kuingiza nchini vifaa
vya kuwabaini watu wanaohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa homa kali ya
ebola ambavyo vitawekwa kwenye viwanja vya ndege pamoja na baadhi ya
maeneo ya mipakani.
Jana Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk Steven Kebwe alikabidhi mashine nne za kuwapima abiria
wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege bila kuwagusa. Vifaa hivyo
vinabaini mtu kuwa na dalili za ebola kutokana na joto lake na abiria
wanapimwa kwa kumulikwa machoni na kwenye masikio.
Kwa kuanzia mashine hizo ambazo ni mfano
wa kamera zitapelekwa kwenye viwanja vya ndege vya Mwanza,
Kilimanjaro, Zanzibar na Dar es Salaam. Maeneo hayo kwa mujibu wa naibu
waziri huyo ndiyo yanapokea wagonjwa wengi kutoka nje ya nchi.
Dk Kebwe pia aliagiza shehena ya mashine
zingine zitakazoingizwa nchini kuanzia leo zipelekwe kwenye viwanja
vingine vya Mtwara, Kigoma na maeneo ya mipakani kuhakikisha kuwa kila
abiria anayetoka nje ya nchi anapimwa dalili za ugonjwa huo hatari.
Pia aliagiza wanadiplomasia na viongozi
wa kitaifa wanaotoka nje ya nchi ambako wanakwenda kuhudhuria mikutano
mbalimbali pia wapimwe kwani ugonjwa hauchagui cheo wala fedha na hadhi
aliyo nayo mtu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa
(MSD), Cosmas Mwaifwani alisema jana kuwa wamenunua mashine hizo nne
kutoka Afrika Kusini, lakini zimetengenezwa nchini Marekani kwa kiasi
cha Sh milioni 16.
Alisema katika kipindi hiki ambacho kuna
mlipuko wa ugonjwa wa ebola huko Afrika Magharibi, upatikanaji wa vifaa
hivyo ni adimu na haiwezekani kupata mashine zote kwa msambazaji mmoja,
hivyo akasema leo ziwawasili mashine nyingine mbili kutoka Ubelgiji.
Mkurugenzi wa Manunuzi wa MSD, Heri
Mchunga alisema mashine hizo kitaalamu zinajulikana kama thermo scanners
ni mashine za mkononi na kila abiria atakayeshuka uwanja wa ndege
atapimwa kwenye macho au masikio bila kugusana.
0 comments:
Post a Comment