Mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano
Ronaldo ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa
Uefa, na kuwapiku kipa wa Bayern Munich,
Manuel Neuer na Arjen Robben.
Ronaldo, 29, kutoka Ureno alipachika mabao
17 na kuisaidia Real Madrid kunyakua Kombe
la Klabu Bingwa Ulaya - Uefa Champions
League- msimu uliopita.
"Nimefurahi sana, kwa hiyo lazima
niwashukuru wachezaji wenzangu kwa sababu
bila timu, tuzo binafsi ni vigumu kuzipata."
Amesema Ronaldo.
Ronaldo aliwazidi Neuer na Robben katika
kura zilizopigwa na jopo la waandishi wa
habari 54.
Neuer, 28, aliisaidia Ujerumani kushinda
Kombe la Dunia, huku Robben, 30, akifunga
magoli 21 ya Bayern na matatu kwa timu ya
taifa ya Uholanzi iliyofika nusu fainali Brazil.
Ronaldo alifunga mabao matatu - hat-trick -
wakati Ureno ilipoichapa Sweden katika
mchezo wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia,
ingawa hakuweza kuwika Brazil, kwani Ureno
ilitolewa katika ngazi ya makundi.
Hata hivyo, kiwango chake katika ngazi ya
klabu kiliweza kushawishi jopo lililopiga kura,
ambalo lilitakiwa kuchagua mshindi kati ya
watatu hao baada ya mchujo kutoka
wachezaji 10.
0 comments:
Post a Comment