Facebook

Monday, 25 August 2014

Watu wawili wafariki kwa Ebola DRC




Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imesema watu wawili wamekufa kutokana na ugonjwa wa Ebola, uliolipuka kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Hao ni wagonjwa wa kwanza wa Ebola kuripotiwa nje ya Afrika Magharibi tangu kuzuka kwa ugonjwa huo huko, ingawaje haijaeleweka wazi kama vifo vya watu hao vinahusiana na mlipuko wa Ebola katika nchi za Afrika Magharibi.
Mpaka sasa watu 1,427 wamekufa kutokana na maambukizo ya virusi vya Ebola.
Shirika la Afya Duniani, WHO limesema kasi na kiwango cha milipuko hiyo hakijawahi kutokea hapo kabla.
Watu wanaokadiriwa kufikia 2,615 Afrika Magharibi wameambukizwa ugonjwa wa Ebola tangu uzuke mwezi Machi mwaka huu.

Kirusi cha Ebola
Hakuna tiba inayojulikana kutibu ugonjwa huu lakini baadhi ya watu walioambukizwa virusi vya Ebola wamepata nafuu baada ya kupewa dawa ya Zmapp iliyo katika majaribio.
Hata hivyo dawa hiyo imeadimika kwa sasa.

Pia Jumapili, mfanyakazi wa afya wa Uingereza aliambukizwa ugonjwa wa Ebola nchini Sierra Leone na kurejeshwa Uingereza akisafirishwa na ndege ya jeshi la Uingereza, RAF.
Ni mgonjwa wa kwanza Mwingereza kuthibitishwa kuambukizwa virusi vya Ebola wakati wa mlipuko wa sasa wa ugonjwa huo.

Marekani imetuma vifaa vya tiba kusaidia kupambana na mlipuko wa Ebola nchini Liberia.
Watu kadha wamekufa katika kipindi cha mwezi uliopita baada ya kuugua homa isiyojulikana katika jimbo la Equateur katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Jumapili, Waziri wa Afya wa DR Congo Felix Kabange Numbi amesema watu wawili kati ya wanane waliopimwa ugonjwa Ebola wamethibitika kuambukizwa ugonjwa huo.
Amesema kuwa eneo la karantini litawekwa katika eneo la kipenyo cha kilomita za mraba 100 katika eneo la Boende ambao wagonjwa wamegundulika.
Amesema huu ni mlipuko wa saba wa ugonjwa wa Ebola nchini DR Congo.
Virusi vya ugonjwa wa Ebola kwa mara ya kwanza viligundulika nchini humo mwaka 1976 karibu na Mto Ebola.
Bwana Numbi amesema vipimo zaidi vinafanyika.

Kituo cha wagonjwa wa Ebola nchini Sierra Leone moja ya nchi zilizoathirika kwa ugonjwa huo Afrika Magharibi
Jumamosi, bunge la Sierra Leone lilipitisha sheria mpya kuwa ni kosa la jinai kuwaficha wagonjwa wa Ebola.
Tayari watu zaidi wamekufa katika mlipuko huu wa Ebola kuliko milipuko mingine iliyowahi kutokea. Kama sheria hiyo itaidhinishwa na rais, wale wanaokamatwa kwa kuwaficha wagonjwa watakabiliwa na adhabu ya kifungo jela cha kufikia miaka miwili.
Hatua hii imekuja baada ya Ivory Coast kufunga mipaka yake ya nchi ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Ebola nchini humo.
Nchi hiyo tayari imepiga marufuku safari za ndege kwenda na kutoka Sierra Leone, Liberia na Guinea.
Gabon, Senegal, Cameroon na Afrika Kusini zimechukua hatua kama hizo.
Shirika la Afya Duniani linasema upigaji marufuku safari za ndege hakusaidii, na kinachotakiwa ni madaktari zaidi na maafisa kusaidia kuwafuatilia walioambukizwa Ebola, ikiwa ni pamoja na kuwa na maabara zaidi za kuhama.
Wiki iliyopita, madaktari wawili wa Marekani waliruhusiwa kutoka hospitalini nchini Liberia baada ya kupewa dawa ya ZMapp drug, wakati ambapo madaktari watatu wa Liberia pia wanaendelea vema.
Ugonjwa wa Ebola unaenezwa kati ya binadamu kwa kugusana moja kwa moja na majimaji ya mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo. Ni moja kati ya magonjwa hatari kuliko yote duniani, ambapo asilimia 90 ya watu wanaoambukizwa ugonjwa wa Ebola hufariki dunia.

0 comments:

Post a Comment