Serikali ya jiji, mjini Seoul, Korea Kusini, imeripotiwa kuruhusu wafanyakazi kulala mchana kazini ili kuongeza ufanisi, hasa katika miezi ya majira ya joto.
Kuanzia Agosti 1, wafanyakazi wa serikali ya jiji la Seoul watakuwa na ruhusa ya kuamua kulala kwa saa moja kati ya saa saba mchana na saa kumi na mbili jioni, ili mradi walipie muda huo, ama kwa kuanza kazi mapema au kuchelewa kutoka.
Gazeti la Korea Times limesema: "Wafanyakazi wanaweza kutumia vyumba vya mikutano na sehemu nyingine kupumzika". Msemaji wa jiji amesema: "Serikali ya jiji itatumia fedha zaidi mwaka ujao kujenga sehemu zaidi za kupumzikia wafanyakazi."
Haifahamiki watu wangapi watatumia nafasi hiyo kwa sababu watatakiwa kulipia muda wa saa moja waliolala. Kwa sasa wengi hutumia muda wao wa chakula cha mchana kupumzika.
Kwa mujibu wa gazeti la Korea Observer, iwapo mtu atataka kulala, atatakiwa kumfahamisha mkuu wake wa kazi mapema, ili aanze kazi saa mbili asubuhi, au aondoke saa moja usiku, kwa sababu wafanyakazi wa serikali hiyo huanza kazi saa tatu asubuhi na kumaliza saa kumi na mbili jioni.
0 comments:
Post a Comment