KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Hispania, Xavi anatarajia kutangaza
uamuzi wake wa kuondoka Barcelona Alhamisi hii wakati akijiandaa
kuhamia katika klabu ya Al Sadd ya Qatar.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 amekuwa akiitumikia
Barcelona kipindi chote na kuisaidia kushinda mataji 23 lakini
anataka kuamua kuondoka baada ya muda mwingi msimu huu
akiutumia akiwa benchi.
Xavi ambaye alikaribia kwenda Al Sadd kiangazi mwaka jana kabla
ya kushawishiwa kubakia Barcelona na meneja Luis Enrique,
anatarajiwa kukutana na wanahabari wiki hii kufafanua uamuzi wake
huku akitarajiwa kuaga Camp Nou katika mchezo wa La Liga dhidi ya
Deportivo La Coruna.
Rais wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amemuelezea Xavi kama
kiungo bora kabisa kuwahi kutokea katika historia ya klabu hiyo.
Xavi anaweza kuongeza medali zingine mbili kati ya nyingi alizonazo
kabla ya kuondoka, wakati Barcelona itakapokwaana na Athletic
Bilbao katika mchezo wa Kombe la Mfalme baadae mwezi huu kabla
ya kukabiliana na Juventus katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya
Juni 6.
0 comments:
Post a Comment