Wale waliotazama Kikao cha Bunge cha jana,
watakuwa walishuhudia jinsi wabunge wa CCM,
Waziri Lukuvi na Spika walivyokuwa
wakiwabembeleza wabunge wa UKAWA wasitoke
nje. Kwa nini?
Kamati ya PAC chini ya Zito, ndiyo iliyokuwa
imetoa taarifa za mwanzo kabisa kwa mataifa
wahisani kwa bajeti ya Tanzania kuwa vigogo wa
serikali walikuwa wamechota pesa toka akaunti
ya Escrow. Ikumbukwe kwamba kamati ya PAC
katika mfumo wa kibunge katika mataifa yote,
ina uzito wa juu zaidi kuliko kamati zote za
Bunge. Mataifa wahisani, kwa kuzingatia kauli ya
PAC, walisimamisha usaidizi katika bajeti ya
Tanzania na kusema kuwa katika corruption
wana 'zero tolerance'.
Aliyekwenda kuibua hoja hii Bungeni ni Kafulila,
mbunge wa upinzani, huku serikali ikijitetea
kuwa hakuna ufisadi.
Taarifa ya CAG na TAKUKURU na PAC, wote
wameeleza uchafu mkubwa katika malipo
yaliyofanywa kwa PAP:
1) PAP si mmiliki halali wa IPTL
2) Akaunti ilikuwa inamilikiwa na TANESCO na
IPTL lakini pesa amelipwa PAP
3) Pesa imetolewa kwenye akaunti ya Escrow na
PAP, na kulipwa kwa Rugemarila, kabla ya hata
huo ununuzi fake wa IPTL kukamilika. Hii ni
kama mtu aliyelipwa fidia ya uharibifu wa gari
na bima kabla ya ajali kutokea
4) Mauzo fake ya hisa za 70% yana thamani
ndogo kuliko ya 30%
5) Mbinu zilifanyika kukwepa kodi mbalimbali
na nyingine kulipwa kiwango cha chini kabisa
(chini ya 10% ya ile iliyostahili)
6) Miamala ilifanyika kwa viwango
visivyokubalika na BOT na kukiuka mkataba
tulioridhia wa anti money laundering
Hatua za kuchukua baada ya haya yote
zinastahili zimridhishe kila mhisani wa Tanzania.
Kuridhika kwa mataifa haya kuna sehemu mbili.
Ya kwanza ni lazima kuonekane kuridhika kwa
vyombo vya ndani ya nchi hasa PAC na vyama
vya upinzani vilivyoibua kashfa hii. Ya pili ni
kuonekana dhahiri kwa kila mhisani kuwa hatua
kali zimechukuliwa.
Kikwete na CCM wanalijua hilo. Wanafahamu
kuwa wahisani hawawaamini, ndiyo maana
wanataka UKAWA washiriki mpaka mwisho ili
ionekane kuwa vyombo vyote vya ndani, pamoja
na vyama vya upinzani wameridhika kwa
maamuzi yaliyofanywa. CCM na Kikwete,
wanafahamu kuwa wahisani katika ufisadi huu
wanawaamini wapinzani zaidi kuliko serikali,
Rais Kikwete na CCM. Kuondoka kwa wabunge
wa UKAWA bungeni, na kuazimia hatua hafifu
kutazidi kumdidimiza Rais, serikali na CCM.
Lakini pia kuna wananchi wanaoona
kinachoendelea.
Athari ya UKAWA Kutoshiriki Maamuzi
Endapo UKAWA watatoka, CCM na serikali
kuweza kuaminika na wahisani itabidi RAIS
achukue hatua kali sana, zaidi ya maazimio ya
Bunge ili wahisani waweze kuamini mfumo wa
utawala wa Tanzania. Rais asipofanya hivyo,
hakuna hata dola moja itakayokuja Tanzania
kuinusuru bajeti ya Kikwete. Lakini ni kutokana
na ufisadi huu, mataifa ya Ulaya na America,
yamemwondolea hadhi na heshima Rais
aliyokuwa akijitahidi kuijenga. Ni Wachina pekee
yao ndiyo wanaoonekana kuwa naye.
Serikali Haina Chaguo Jingine
Kwa sasa serikali haina fedha, na haina fedha ya
kigeni. Uwezo wa ugharamiaji wa huduma za
ndani haupo, miradi ya maendeleo imesimama,
uchaguzi mkuu unakuja, hali ya kisiasa ya CCM
kwa sasa ni mbaya zaidi kuliko miaka ya nyuma
na uelewa wa wananchi unazidi kuongezeka. Kwa
hali hiyo ya serikali, ndiyo maana serikali
inalazimika kuridhia chochote kutoka kwa
wahisani na wapinzani wake UKAWA.
UKAWA wana Turufu
Kwa sababu nilizozitaja hapo juu, UKAWA
wakitaka hata PINDA atoke, atatoka tu, wakitaka
waziri yeyote atoke atatoka tu. Lakini naamini
UKAWA hawatatumia turufu hiyo kuwaadhibu
wasiohusika.
Mbowe na Zito Wanasiasa Werevu
Wapo ambao hawaelewi werevu wa Zito kuridhia
mapendekezo ya Chenge. Wabunge wa CCM na
Spika bila kujua, wakakubali kuwa wote
waliotajwa, azimio la Bunge liwe kama lile la
Maswi, wakapiga makofi na kukubali. Azimio lile
lilikuwa linamweka na Pinda katika kundi la
kuchukuliwa hatua na Rais. Hivyo mzigo wote
ungerushwa kwa Rais, na kama Rais
asingechukua hatua, kila mmoja na wahisani
wangejua kuwa tatizo ni Rais. Ole Sendeka
akashtuka, na ndiyo Makinda akafunguka macho
kujua hatari ya pendekezo la Zito. Wabunge wa
CCM waliposhtuka, Mbowe na wabunge wote wa
UKAWA wakagomea maazimio mepesi na kutaka
kutoka nje ili ijulikane kuwa maazimio mepesi
yametolewa na wabunge wa CCM tu.
Hawakutaka Escrow Ijadiliwe bali Walilazimika
Kujadiliwa kashfa hii hakukutokana na dhamira
njema ya Rais, Serikali, Spika au CCM bali
walilazimika. Na ninahisi Rais alilazimisha
ijadiliwe baada ya maji kufika shingoni.
Kujadiliwa kwa ripoti hii ni sehumu ya jitihada
ya kuinasua serikali na Rais katika ukata mkubwa
wa pesa na kuporomoka kwa CCM.
Hakika hata leo kutakua na jitihada kubwa sana
za kumshawishi Mbowe wabunge wa UKAWA
wasisusie. Na hapo ndipo nafasi ya UKAWA ilipo
katika kutoa masharti kwa wabunge wa CCM,
serikali na Spika. Katika hatua hii na mazingira
yaliyopo, wabunge wa UKAWA ni wengi kuliko
wale wa CCM maana ndiyo wenye turufu. Bahati
mbaya ni wabunge wa wachache sana wa CCM
wanaoujua ukweli huu.
0 comments:
Post a Comment