Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na
wengine wengi kujeruhiwa katika mapigano
katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya.
Polisi walipambana na vijana walioingia
katika Msikiti wa Swafaa eneo la Kisauni na
mpaka sasa zaidi ya vijana 400
wanashikiliwa tangu kuanza kwa msako
huo, mapema wiki hii.
Msikiti huo ulifungwa jana baada ya polisi
kuuvamia Jumatano, ambamo walipata
magruneti, mabomu ya petroli na silaha
nyingine. Hali ya wasi wasi bado imetanda
katika mji huo wa pwani. Serikali
imekwishafunga misikiti minne ambayo
wanasema ina uhusiano wa watu wenye
misimamo mikali ya imani ya kidini.
Awali polisi mjini Mombasa pwani ya Kenya
walisema wamepata silaha nyingine zaidi
yakiwemo mabomu katika msikiti wa tatu
ambao ulifanyiwa upekuzi
Msako huo katika msikiti wa Swafaa mtaani
Kisauni unakuja baada ya msako mwingine wa
Jumatatu ambapo polisi pia walipata silaha
ndani ya msikiti ambao wanasema hutumika
kutoa mafunzo yenye itikadi kali.
Mtaa wa Kisauni ndiko vijana waliokuwa
wamejihami kuwadunga visu watu wanne na
kuwaua. Pia waliwashambulia kwa silaha
nyingine.
Waziri wa usalama wa ndani, Joseph Ole Lenku
anasema kuwa msako huo ulifanywa katika
misikiti ambayo hutumiwa na watu wanaoeneza
itikadi kali za kiisilamu kwa vijana ambao
inadaiwa wanajiunga na kundi la wapiganaji wa
kiisilamu la Al Shabaab nchini Somalia.
Viongozi wa kiisilamu wamelaani misako hiyo
katika Misikiti wakisema kuwa itachochea zaidi
vijana kuendeleza itikadi kali za kidini.
Chanzo:BBC
0 comments:
Post a Comment