Facebook

Friday, 21 November 2014

Ukawa wafichua njama za kuizima IPTL bungeni

Dodoma. Wakati kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikianza kupitia ripoti ya IPTL kuhusu uchunguzi wa ufisadi katika Akaunti ya Tegeta Escrow, wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umedai kwamba kuna mikakati imeandaliwa kuzima ripoti hiyo kusomwa na kujadiliwa bungeni.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema jana kwamba moja ya mikakati hiyo ni madai ya kuwapo barua ya Mahakama kuzuia mjadala huo akisema mkakati huo unatokana na ukubwa wa kashfa na jinsi inavyowahusisha viongozi waandamizi serikalini.
Mbatia aliyeambatana na kundi kubwa la wabunge kutoka Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, alisema: “Iko mikakati na mbinu za kila aina kulihujumu Bunge lisisimamie fedha za walipakodi, ndiyo maana kuna danadana na tuna taarifa za kuwapo barua kutoka mahakamani kuzuia jambo hilo lisijadiliwe bungeni kwa madai eti kuna kesi.
“Mahakama haiwezi kuingilia shughuli za Bunge, inatia wasiwasi kwa kuwa Ofisi ya Bunge nayo imekuwa na danadana kila siku kwa kubadilisha badilisha ratiba wakati sisi tunataka hawa waliohusika kwenye kashfa hii wachukuliwe hatua.”
Pia, alisema kuna taarifa kwamba Serikali inadai haina fedha, ikitaka kufupisha Bunge na suala hilo lisijadiliwe sasa hivi.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Mnyaa alisema: “Serikali inategesha tegesha tu mambo bungeni na ndiyo maana leo (jana) wameahirisha Bunge hadi kesho (leo) bila sababu za msingi, wanafinya muda wa sisi kujadili sakata hili,” alisema Mnyaa.
Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alisema escrow ni kama ilivyokuwa kashfa ya Richmond ambayo iliwang’oa wahusika wakuu bungeni, hivyo haiwezekani isijadiliwe bungeni kwa madai kwamba Mahakama imezuia...
“Hakuna utaratibu kama huo wa Mahakama kuelekeza Bunge kitu gani kifanyike na gani kisifanyike pia hata Katiba hairuhusu hilo.”
Lissu alishangazwa na Naibu Spika, Job Ndugai kuahirisha Bunge jana hadi leo kwa madai kuwa yeye (Lissu) alikuwa hajakamilisha taarifa ya upinzani kwenye muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2014 akidai kuwa huo ni upotezaji wa muda.
“Nilimwomba Naibu Spika kuwa aahirishe muswada huo hadi kesho kwa kuwa ulikuwa umepangwa tarehe 25 lakini ghafla ukabadilishwa na mimi sikuwapo kwa muda wote huo. Sikuomba aahirishe Bunge nilimwomba aahirishe muswada tu,” alisema Lissu.
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema naye amesikia kuwapo barua ya Mahakama kuzuia mjadala huo na kusema kama ni kweli, halitakuwa sahihi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika Operesheni Delete CCM mjini Dodoma jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema si Waziri Mkuu wala Jaji Mkuu anayeweza kuuzima mjadala wa escrow bungeni.


Alisema kashfa hiyo ambayo chama chake kina nyaraka zake na ripoti za uchunguzi wa escrow na Takukuru, lilianzia bungeni na lazima lijadiliwe na kumalizikia bungeni.
Ndugai ajibu hoja
Akizungumzia madai hayo, Ndugai alisema hajui kama kuna barua kutoka mahakamani kuzuia mjadala wa escrow bungeni na suala hilo litawasilishwa na PAC bungeni Novemba 27 kama ilivyopangwa.
“Waiamini kamati, kwanza hawa wa upinzani ni yao (kamati) haiongozwi na CCM, mimi naamini kamati itafanya kazi nzuri. Sidhani kama kanuni zinaruhusu kugawa ripoti hiyo kwa kuwa ni siri, kanuni hairuhusu.”
Rejea
Ripoti ya Tegeta Escrow inatokana na uchunguzi maalumu wa Sh306 milioni zilizochotwa katika akaunti ya escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Fedha hizo zilitokana na gharama za uwekezaji zilizokuwa zinalipwa na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina ya wabia hao.
Tanesco ililalamika kuwa ilikuwa inailipa zaidi IPTL kinyume na gharama halisi za uwekezaji, hivyo kuamuliwa na Mahakama kuwa fedha hizo ziwekwe katika escrow hadi upatikane ufumbuzi wa mgogoro huo lakini zikachukuliwa kabla kesi kuamuliwa.

Chanzo:MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment