Facebook

Wednesday, 10 December 2014

SIASA YA TANZANIA:-"RAFIKI WA MWIZI NAYE NI MWIZI"


             
Maisha ya siasa hayana rafiki wa kudumu wala adui wa kudumu.Maisha ya kisiasa yamezungukwa na maslahi.Utashi binafsi na matamanio ya kiutawala huzunguka wanasiasa wengi duniani.Wengine wana dhamira ya dhati na wengine ni "wapigaji" tu."Wapigaji" hawa ndio wale ambao kila skendo ya ufisadi lazima wawepo iwe wao kushiriki moja kwa moja au watu wao kushiriki moja kwa moja kupitia nguvu yao kisiasa.

Sakata la Escrow ni mwanzo wa siasa mpya kuelekea 2015.Kazi nzuri ya David Kafulila na Mwami Zitto Kabwe imejidhihirisha katika vikao vya bunge lililoisha wiki iliyopita.Hawa ni vijana kutoka mkoa wa Kigoma uliopo kanda ya Magharibi.Mwami Zitto akiwa ni mbunge kwa awamu mbili akiwakilisha Kigoma Kaskazini huku David Kafulila akiwa ni mbunge kwa awamu moja akiwakilisha Kigoma Kusini.

Hawa ni marafiki wa siku nyingi.Tangu wote wakiwa Chadema kabla ya Kafulila kuhamia NCCR Mageuzi baada ya kufitiniwa Chadema kwa kosa la kumnadi Mwami Zitto kurithi nafasi ya mwenyekiti Freeman Mbowe.Hata mgogoro wa kiuongozi kati ya Mbatia na Kafulila ulihusishwa na mkakati wa Mwami Zitto kujiunga na NCCR Mageuzi ili aukwae uenyekiti.

Mgogoro huu ulipelekea Kafulila asimamishwe uanachama na kukimbilia mahakamani kuweka pingamizi lililopelekea kuhudumu kama mbunge wa mahakama kabla ya mgogoro wake na Mbatia kusuluhishwa na yeye kurudishiwa uanachama wake.Kilichomtokea Kafulila ndicho kilichomtokea Mwami Zitto Kabwe pale Chadema.

Mwami Zitto aliitwa mnafiki,msaliti,mroho wa madaraka,mbakaji wa demokrasia ndani ya chama na mla rushwa pia kibaraka wa CCM.Urafiki wake na viongozi wa CCM unampa wakati mgumu kisiasa.Ila katika sakata la Escrow ajabu hadi wale waliomuita kibaraka wa CCM walijiunga naye na kumuunga mkono.Je nao waitwe vibaraka wa CCM!?

Siasa kweli haina rafiki wa kudumu au adui wa kudumu."Tumbili" na "Kibaraka" ndio vinara wa siasa za upinzani baada ya kuibua sakata la Escrow bungeni.Hata waliokuwa hawawapendi walijiunga nao.Hawakuwa na namna.Ukimya wao ungewahukumu 2015 majimboni mwao.Mbowe alimhitaji Zitto na Mbatia alimhitaji Kafulila.Mmoja wa rafiki zangu ambaye ni mwanachama wa Chadema ila mfuasi kindakindaki wa Mwami Zitto aliandika katika mitandao "Chadema bring back our Zitto" yaani Chadema turudishieni Zitto wetu.

Hii ni ishara kwamba Mwami Zitto na Kafulila ni nembo ya vyama watokavyo.Hawa ndio nyota wa mchezo kwasasa.Baya lolote dhidi yao ni maafa kwa vyama vyao.Ipo haja ya Chadema kuketi na kumaliza mgogoro wao na Mwami Zitto Kabwe.Huyu ndio kijana aliyeipa jina Chadema.Tangu sakata la Buzwagi,mabilioni ya Uswisi hadi Escrow.Mwami Zitto na Kafulila wanafanya siasa ya kisomi.Wanasoma sana na kuandika.Wanahoji kila lenye kuleta utata kwa maslahi ya taifa.PAC ni kati ya kamati bora za bunge kuwahi kutokea nchini.

"Kombinesheni" ya Deo Haule Filikunjombe na Mwami Zitto Kabwe katika PAC ni alama ya mwisho wa ufisadi nchini.Ukibaraka wa Mwami Zitto unafutwa na nyayo anazokanyaga PAC.Nyayo hizi zinawabomoa wabaya wake kisiasa.Hadi leo umekosekana ushahidi wa kumtia hatiani Mwami Zitto Kabwe.Siku chache kabla ya kusomwa kwa ripoti ya PAC bungeni kuhusu Escrow,Mbowe alifanya mkutano wa hadhara mkoani Kigoma na kumshambulia Mwami Zitto.Ila juzi wakakutana bungeni,Mbowe akaona umuhimu wa kumuunga mkono Mwami Zitto kutaka pesa ya umma irudishwe na wahusika wawajibishwe na kwa mara ya kwanza Mwami Zitto akashiriki kikao cha Ukawa.

Kinachotokea kwa Mwami Zitto na kilichotokea kwa David Kafulila natabiri kitatokea pia CCM.Ila kwa CCM nazungumzia mgogoro wa urais 2015.Hadi sasa kati ya wanaotajwa ni watatu tu ndani ya CCM wanaonekana wana misuli ya kupambana kisiasa kuwania tiketi ya kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang'anyiro cha urais.Hawa ni Edward Ngoyai Lowassa,Mizengo Kayanza Peter Pinda na Bernard Kamillius Membe.

Lowassa ni waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya ufisadi wa mradi wa kufua umeme wa Richmond mwaka 2008.Mizengo Pinda ni waziri mkuu aliyemrithi Lowassa,naye amenusurika katika sakata la Escrow.Ila kama ilivyo kwa Lowassa na Richmond,Pinda naye ana doa tayari.Amebaki Membe peke yake.Akiwa hana doa.Ndani ya CCM sasa anaonekana ana uwezo wa kumrithi rais Kikwete.Wakati sakata la Escrow linarindima nchini wapinzani wa Membe walizusha katika mitandao kwamba Membe anahusika.Ripoti ya CAG na taarifa ya kamati ya PAC vikamsafisha kwa kutotaja mahali popote uhusika wa Membe au uhusika wa rafiki wa Membe.

Waingereza wana msemo wao usemao "tell me your friend and I will tell you your character" yaani nitajie rafiki yako nami nitakwambia tabia yako ikoje.Hii nukuu ina maana kubwa sana katika maisha ya sasa sio tu ya kisiasa.Ukiwa na urafiki na wahuni nawe utaonekana mhuni.Escrow inahusisha baadhi ya marafiki na watu wa karibu wa baadhi ya wanaotajwa kati ya Pinda na Lowassa.
Nani asiyejua kama Chenge ni rafiki wa karibu wa Lowassa? Leo hii kila baya linaloigharimu nchi lina mkono wa Chenge.Je anatumwa au kutumiwa na Lowassa? Isije ikawa anatumika kutafuta hela ya kampeni.Lowassa anaponzwa na marafiki wanaomzunguka.Marafiki wa Lowassa wanakigharimu chama na serikali.Hata kama tuko nao CCM basi mamlaka husika ziwashughulikie.Ccm sio kituo cha malezi ya wachafu.Nahofia wengine wanataka waingie madarakani ili kuficha uovu wao na wanaowazunguka.

Kwa namna mambo yanavyoenda naona kabisa anguko la Lowassa na Pinda katika mpambano wa ndani ya CCM.Moyo wangu unaniambia Membe anatufaa.Huku mitaani wananchi wamebadilika.Wanataka kiongozi anayeikataa rushwa bila kukwepesha maneno.Tangu sakata la Escrow liibuke kati ya Lowassa,Pinda na Membe ni Membe pekee aliyelikemea waziwazi mbele ya waandishi wa habari na wanazuoni.Mwenye ushahidi kuwa Lowassa au Pinda kusimama mbele ya kada yoyote ya jamii nje ya bunge na kukemea ufisadi wa Escrow anipinge kwa makala kama nilivyoandika mimi.

Pinda aliibariki Escrow kwa kusema haikuwa pesa ya umma.Lowassa aliibariki Richmond kwa kuitetea ipate tenda ya kufua umeme Tanzania ilhali akijua fika haina uwezo huo.Ripoti ya kamati teule ya Mwakyembe ikawaumbua wahusika.Tena wote wakiwa ni maswahiba wa Lowassa tuliozoea kuwaona na kusikia wakishiriki katika wizi wa mali ya umma kama vile Karamagi na Rostam Aziz.Nashawishika kuamini kwamba tabu,mateso na umasikini wa watanzania unahusika moja kwa moja na matendo ya hawa wanaotuhumiwa katika ufisadi mbalimbali nchini kama vile Escrow,Buzwagi,mabilioni ya Uswisi na Richmond.

Utajiri wa nchi hii upo mikononi mwa watu hawa wachache.Wanafaidi wao na watoto wao.Hatuna dawa hospitali,hatunywi maji safi na salama,hatuna umeme wa uhakika hadi vijijini,elimu ni duni,hakuna ajira yote kwasababu yao.Wanamfanya rais wetu awe kama yatima.Aliwaamini wakamwangusha na bado mirija waliyojijengea ya kufisadi nchi haijakatika.Hawa wanapaswa kuangushwa 2015 ndani ya CCM na katika majimbo yao ya uchaguzi.Na hili litakuwa zuri sana kama watapandishwa kizimbani kwa makosa ya jinai,itasaidia kuzuiwa kugombea hadi kesi zao za msingi mahakamani zimalizike.Nchi haitaki mtenda jinai.

Kwa nilichoandika hapa naamini nimewakera watu.Nimekera wapambe wao.Nimekera wasaka tonge kwao.Ila msimamo wa nilichoandika haubadiliki.Hawa tuwashughulikie tu ndani na nje ya chama.Tuwaulize, wamesahau nini serikalini kwa miaka yote ya wizi wao?Mwenye akili atang'amua mapema na kujiondoa katika makundi na mitandao yao.Nawaona baadhi wanawaza kujiunga na Membe.Wamegundua walipo sio mahali salama kwa uhai wa taifa letu na maisha yao kisiasa.Swali;je dhambi ya kumsemea uongo na kumfitini Membe wameitubu au wataitubu?Maana Membe pamoja na ukimya wake katika mbio za urais bado anasakamwa.Membe hajaoteshwa ila zengwe dhidi yake ni kubwa.

Nimshauri Membe asiwakubali marafiki wa aina ya Chenge au Karamagi katika kambi yake.Membe asitishwe na utafiti wa Twaweza.Utafiti wa Twaweza umewapigia mbiu wenye doa.Sisi wapigakura tunampigia mbiu yeye kati ya wote wanaotajwa.Nawaona mahasimu wa Membe wakijaribu kutaka kumuunga mkono ila tu awe makini nao.Samahani kwa niliowaudhi ila Membe hana makandokando,akioteshwa atatufaa.Yaliyomtokea 2012 akigombea Nec yanawarudi wanaomchukia.Kama yaliyowatokea Mwami Zitto Kabwe na Kafulila kuungwa mkono na mahasimu wao ndani ya vyama vyao katika sakata la Escrow ndicho kitakachotokea katika kuwania urais kwa Membe.Wabaya watajirudi ila tu awe nao makini.

Imeandaliwa na Hussein Bashe.

0 comments:

Post a Comment