Rais Uhuru Kenyatta amemwachisha kazi
waziri wa usalama Joseph Ole Lenku na
kumpendekeza waziri mpya wa usalama
Joseph Nkaiseri kuchukua nafasi hio.
Wakati huohuo mkuu wa polisi nchini Kenya
inspekta generali David Kimaiyo amejiuzulu
kutokana na shinikizo dhidi yake afanye hivyo
kwa kushindwa kukabiliana na utovu wa
usalama nchini.
Rais Kenyatta alisema kuwa baada ya
mazungumzo na Bwana Kimaiyo alikubali
'kustaafu' mapema kutoka kwa majukumu yake
kwa sababu za kibinafsi.
Rais alitoa tangazo hilo wakati akihutubia taifa
kufuatia shambulizi la hapo jana dhidi ya
wachimba migodi 36 waliouawa na Al Shabaab
mjini Mandera Kaskazini ya Kenya.
Rais pia alitangaza kuwa amekubali ombi la
Generali wa polisi David Kimaiyo kuachia
wadhifa wake.
Kimaiyo na Ole Lenku wamekuwa wakikabiliwa
na shinikizo za kuachia ngazi kufuatia kukithiri
kwa utovu wa usalama nchini.
Hatua ya kuwatimua kutoka katika nyadhifa
zao wawili hao bila shaka litakuwa jambo la
kuridhisha kwa wakenya wengi ambao
wamekuwa wakilalamikia utovu wa usalama na
kuwataka waondoshwe ofisini.
Uteuzi wa Joseph Nkaisery kama waziri mpya
wa usalama ni jambo jipya kwani atakuwa
mwanasiasa wa kwanza kutoka kwa upinzani
kuwa ndani ya serikali.
Alipokuwa anahutubia nchi,Rais Kenyatta
aliwasihi wabunge kuongeza mda wa vikao vyao
vya leo ili kumhoji na kumkagua Nkaisery
aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya waziri mpya wa
usalama na maswala ya ndani ili
wamuidhinishe.
0 comments:
Post a Comment