Tuesday, 24 February 2015
TARIME WALAANI MAUWAJI YA ALBINO. WAITAKA SERIKALI KUOMBA HIFADHI NJE YA NCHI ILI KUWANUSURU ALBINO.
Wakazi wa Tarime mkoani Mara wamelaani vikali mauaji yanayofanyika dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi na kuyaita ya kinyama na ya makusudi. Hayo yamefanyika kupitia jukwaa huru la wanatarime ambalo msingi mkuu wa malengo yake ni kujadili na kuchukuwa hatua stahiki, kwa ustawi wa Tarime na Tanzania kwa ujumla. Jukwaa hilo ambalo limekuwa likifanya majadiliano yake katika moja ya kundi maarufu lijukanalo kama 'Jambo Tarime', limekuwa likifanya hivyo mara kadhaa kuhusu mauwaji yanoyofanyika Tarime kwa kile walichodai kuwa, mauwaji yote dhidi ya binadamu yanapaswa kupingwa vikali kwakuwa ni uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu. Wakiongea na BantuTz.com kwa niaba ya jukwaa hilo, viongozi wa jukwaa hilo ambao ni Bob Chacha Wangwe na Julius Matiko walikuwa na hay:-
Nikimnukuu Bob Chacha wangwe amesema;
" Tunalaani vikali mauji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi na, ni kwasababu hiyo tunaitaka serekali kuchukuwa hatua za haraka ikiwa ni pamoja na kuwatafutia hifadhi nje ya nchi kwakuwa ni dhahiri kuwa, wauwaji hawa wa binadamu wameishinda serikali"
"Tumeshuhudia hatua za haraka zikichukuliwa dhidi ya watu wanaosadikiwa kuwa magaidi kule Amboni, tumeshuhudia oparasheni za makusudi zikianzishwa kwa kutumia majeshi yote ili kuwalinda tembo wetu, kwanini hili la mauwaji ya binadamu wenzetu hayo hayafanyiki?. Hata vyombo vya dola na serikali vikionesha kushindwa kukabiliana na mtandao huo, sisi kama jamii hatupaswi kukata tamaa na kuruhusu mauwaji hayo kuendelea, ni lazima tuchukuwe hatua za kuwanusuru wenzetu ikiwa ni pamoja na kuibua mtandao wa wahusika wa mauwaji hayo".
Aliongeza kijana huyo.
Naye Julius Matiko amesema "binadamu wote wana haki ya kuishi na ni wajibu wa serikali na jamii kuhakikisha wanatoa na kulinda haki hiyo kwa hali na mali, ameongeza kuwa inasikitisha kuona taifa letu linageuka na kuwa na sura ya kutisha kimataifa kwa watu kuua watu wengine kwa imani potofu wakati huo kukiwa hakuna juhudi za dhati za serikali na vyombo vya dola katika kutokomeza uovu huo ambao umevuka mipaka ya kikatili. Ameongeza kuwa, kwa mwenwendo unaoonyeshwa na serikali katika kushughilikia tatizo , anaamini kuna uhusika wa watu wenye ushawishi kwenye vyombo vya dola na serikali."
Katika kujaribu kutoa mbinu ya kutokomeza tatizo hilo, ndg Julius amependekeza serikali kufuta vibali vya waganga wa jadi wanaopiga ramli na uchunguzi wa kina ufanyike kuwabaini wahusika na baadae hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa uharaka maalumu..pia amependekeza adhabu ya kifo itekelezwe kwa wale wataobainika kuhusika ikiwa ni pande Tatu ambazo ni waganga, wauaji na watu wanaowatuma.
Wangwe kwa upande wake aliongeza kuwa"Mtandao huu wa mauwaji una ratibiwa na makundi makuu mawili ambayo ni waganga wa kienyeji pamoja na wateja wao. Tunawaomba watanzania tushirikiane kwa pamoja katika hili bila kuchoka hata kama zipo dalili za watawala kuwa sehemu ya wateja hao. Ni jambo la kushangaza kuona serikali ikishindwa kuwabana watu hawa waharibifu licha ya kuwa wanafahamika. Kwanini waganga wasipewe conditions ( mashart) za kuhakikisha hawawatumi wateja wao kufanya dhambi hiyo?''. Pia aliongeza kwa kusema serikali inapaswa kurekebisha vyombo vinavyotoa haki kuhakikisha kesi za namna hii zinachukuliwa kwa uzito unaostahili bila kuchukuwa muda mrefu.
Jukwaa hilo ambalo limetangaza pamoja na mambo mengine, kuwa balozi na mlinzi dhidi ya mauwaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na haki za binadamu kwa ujumla, limetoa wito kwa umma kushirikiana nao katika vita hiyo ya kuwatetea ndugu zetu walemavu ambao hawana hatia na hawastahili kuteswa au kunyimwa amani kwa sababu ya ulemavu ambao hawakujitakia. Waliomba pia kila mtu kuwa mlinzi na kutoa taarifa polisi pindi wanapobaini au kuhisi wahusika wa mauaji hayo.
Pia jukwa hilo limeitaka serikali kupitia wizara ya jinsia, watoto na makundi maalumu, na asasi zisizo za kiserikali pamoja na makundi mbalimbali katika jamii, kuendelea kuwaelimisha wananchi kuachana mara moja na imani potofu zinazo hatarisha maisha ya watanzania wenzetu.
Sambamba na hayo, pia wameishauri serikali kuwajengea uwezo wananchi hususan vijana kwakuwa vitendo hivi vina changiwa pia na umaskini.
Endelea kutembelea www.bantutz.com kwa habari na makala mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment