Facebook

Monday, 23 February 2015

Yanga yazidi kutakata Mbeya, Simba Hoi Shinyanga

Timu ya Yanga imejibebea point nyingine tatu katika mkoa wa Mbeya baada ya leo kuichapa timu ngumu ya Mbeya City jumla ya mabao 3-1 katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara.


Mabao ya Yanga yamefungwa na Simon Msuva dakika ya 18, Mrisho Ngassa dakika ya 59 na Amis Tambwe dakika ya 78 wakati la kufutia machozi likifungwa na Peter Mapunda dakika ya 69.
Kwa matokeo hayo, Yanga imeweza kufikia lengo lake la kuchukua point 6 katika michezo miwili katika uwanja huo wa Sokoine jijini Mbeya baada ya Alhamis kuichapa Prisons bao 3-0, na kufikisha point 31 zinazoifanya izidi kujikita kileleni.
Mbeya City imebaki na point zake 17 na kushushwa hadi nafasi ya 12.
Wakati Yanga ikizidi kuchana anga, Simba leo imeangukia pua na kuchinjwa na wapiga debe wa Stand United ya Shinyanga katika dimba la Kambarage mjini Shinyanga kwa kupigwa bao 1-0 lililopatikana dakika ya 11 ya mchezo.
Katika dakika ya 90 ya mchezo huo, mchezaji Yasin Mustapha wa Stand United alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia vurugu mchezaji wa Simba Abdi Banda, na baadaye dakika 7 kuongezwa ambazo hata hivyo hazikuweza kuibeba Simba na mpaka mwisho wa mchezo Stand Unite 1-0 Simba.
Simba imebaki na Point zake 20 katika nafasi ya 4 wakati Stand ikipanda hadi nafasi ya 11 ikifikisha point 18.

Katika mchezo huu, Golikipa Ivo Mapunda wa Simba alionekana kushikwa na hasira dhidi ya wachezaji wenzake kiasi cha kuwakaripia mara kwa mara, na ilifikia hatua akajianzia menyewe mpira na kuingia nao katikati ya uwanja kwa lengo la kwenda kufunga mwenyewe.
Baadhi ya vigogo Simba waliokuwepo uwanjani wakishuhudia Simba yao ikipigwa na 'Wapiga Debe' wa Stand ni pamoja na Rais wa Simba Evans Aveva, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zakaria Hanspope, Kassim Dewji na msululu wa mashabiki kutoka Dar es salaam.
Majira ya asubuhi, shabiki mmoja wa Simba alikamatwa uwanjani kwa madai ya kufanya vitendo vya kishirikina.
Azam ambayo kabla ya mchezo wa leo ina point 26 katika nafasi ya Pili, inashuka katika dimba la Azam Complex leo saa 2 usiku kuikabili Prisons kutoka Mbeya.

0 comments:

Post a Comment