Facebook

Friday, 14 November 2014

Ndege nyingine ya kijeshi yaanguka Nigeria.

Helikopta ya kijeshi ya Nigeria imeanguka
katika eneo la kaskazini mashariki mwa
nchi hiyo , ikiwa ni helikopta ya pili kupata
ajali kwa muda wa chini ya wiki mbili .

Ajali ya hivi karibuni imetokea viungani mwa
mji wa Yola, mji mkuu wa jimbo la Adamawa
ambako kwa sasa jeshi linahangaika kukabiliana
na uasi wa wanamgambo wa Jihad.

Kuna taarifa kutoka jimbo hilo kuwa wapiganaji
wa Boko Haram wamekuwa wakiwasukuma
wanajeshi nje ya mji muhimu uliopo karibu na
mpaka wa Cameroon.

Wanafunzi katika chuo
kikuu cha Modibbo Adama kilichopo katika mji
wa Yola wanasema walisikia Helikopta
ikianguka karibu na chuo chao .

Baada ya kuanguka ikafuatiwa na mfulurizo wa
milipuko , kwani inaaminiwa kuwa ilikuwa
inasafirisha silaha na zana nyingine za kijeshi
kwa wanajeshi wanaopigana Boko Haram.
Haijawa wazi ikiwa mtu yeyote aliekuwa ndani
ya ndege hiyo amenusurika na kifo.

Baada ya kusikia kelele , baadhi ya wanafunzi
walianza kukimbia wakihofia kuwa wapiganaji
wa jihad walikuwa wakiwashambulia Hii ni
helikopta ya pili ya kijeshi kuanguka katika mji
wa Yola wiki hii.
Wakati huo huo katika eneo la kaskazini kuna
taarifa kuwa mji wa Mubi hauko tena mikononi
mwa Boko Haram baada ya askari na vikosi
vya usalama vya eneo hilo, wakiwemo
wawindaji kuurejesha tena.

Lakini katika sehemu hii ya kaskazini ya jimbo
la Adamawa bado hali ni mbaya na watu
wamekuwa wakiukimbia mji huo ambao
makundi ya Jihad yamekuwa yakijaribu kuuteka.

0 comments:

Post a Comment