Facebook

Sunday 20 April 2014

Nahodha wa meli iliyozama Korea kusini atiwa mbaroni leo hii..............fuatilia hapa.............


 
Nahodha wa kivuko cha Korea Kusini kilichozama na kusababisha watu zaidi ya 300 kutojulikana walipo amekamatwa Jumamosi (19.04.2014) kwa tuhuma za uzembe na kuwatelekeza watu waliokuwa kwenye shida ya kuhitaji msaada. Wapelelezi wamemkamata Lee Joon -Seok na wafanyakazi wenzake wawili mapema leo asubuhi na wote watatu wameshutumiwa kwa kuwatelekeza mamia ya abiria waliokuwa wamenasa ndani ya chombo hicho na kuhangaika wenyewe kujiokowa. Mahakama imesema imeamuru kukamatwa kwao ili kuzuwiya watuhumiwa hao kukimbia au kuharibu ushahidi.

Nahodha huyo mwenye umri wa miaka 68 yuko chini ya uchunguzi kwa kuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuitelekeza meli hiyo wakati abiria wake wakiwa bado wako hatarini.Lee amefunguliwa mashtaka ya uzembe na kushindwa kuhakikisha usalama wa abiria kinyume na sheria za bahari.Abiria waliambiwa kupitia vipaza sauti kwamba wabakie hapo walipo licha ya kuwa meli hiyo ilikuwa ikizama upande mmoja.

Nahodha atetea uamuzi wake

Watu 32 imethibitishwa kuwa wamekufa katika janga hilo na wengine 270 hawajulikani walipo wengi wao ni watoto wakiwa katikasafari ya shule ya upili.


"Naomba radhi kwa wananchi wa Korea Kusini kwa kusababisha janga hili na nainamisha chini kichwa changu kuomba radhi familia za wahanga" Lee amewaambia waandishi wa habari wakati akiondoka katika mahakama ya Wilaya ya Gwangiu Tawi la Mokpo kuelekea gerezani leo asubuhi. Lakini ametetea uamuzi wake ulioshutumiwa vikali wa kusubiri dakika 30 kabla ya kuamuru kuchukuliwa kwa hatua za kuondolewa kwa abiria.

"Wakati huo mawimbi yalikuwa makali sana, hali ya bahari ilikuwa ya baridi,na nilifikiri kwamba iwapo watu wataondoka kwenye kivuko hicho bila tafakuri inayofaa na ikiwa hawakuvaa majeketi ya uokozi na hata ingelikuwa wamevaa, wangelisombelewa mbali na maji na kukabiliwa na matatizo mengine magumu" Lee amesema na kuongeza kwamba meli za uokozi zilikuwa bado hazikuwasili na pia kulikuwa hakuna meli zozote zile za uvuvi au mashua nyengine karibu wakati huo.

Watu wengi wangeliweza kuokoka

Wataalamu wamesema watu wengi zaidi wangeliweza kunusurika ingelikuwa wameondoka kwenda vituo vya uokozi kabla ya meli hiyo kuegemea sana upande mmoja na maji kuanza kujaa ndani.

Msaidizi wake wa tatu mwenye umri wa miaka 26 ambaye alikuwa na uzoefu wa miezi sita katu hakuwahi kabla kuongoza meli hiyo kwenye njia hiyo na ndie aliekuwa kwenye usukani wakati meli hiyo Sewol ilipozama.


Kwa mujibu wa sheria Lee alikuwa alitakiwa awe kwenye sitaha ya meli ambapo nahodha hutowa amri zake ili kusaidiana na wenzake wakati meli ikipita kwenye maeneo ya bahari chafu.

Mwendesha mashtaka mwandamizi Yang Jung-jin amewaambia waandishi wa habari nahodha huyo alikimbia kabla ya abiria.Ukanda wa video uliorushwa na shirika la habari la Yonhap umemuonyesha Lee akiwa miongoni mwa watu wa kwanza kuwasili ufukweni kwa kutumia boti ya uokozi.

Yang amesema wafanyakazi hao wenzake wawili waliokamatwa walishindwa kupunguza kasi ya mwendo wakati kivuko hicho kikiwa karibu na visiwa na wameshindwa kuchukuwa hatua zinazohitajika kuokowa maisha.


Kulikuwa na abiria 476 na mabaharia kwenye meli hiyo ya tani 6,825 wakiwemo wanafunzi 320 na walimu 15 kutoka Shule ya Upili ya Danwon huko Ansan karibu na mji mkuu wa Seoul wakati ilipoanza kupinduka na kuzama ikiwa safarini kutoka Incheon kuelekea kisiwa cha kitalii cha Jeju kilioko kusini.

Afisa wa ulinzi wa mwambao Ko Myung-seok amesema meli 176 na ndege 28 leo zimewekwa kufanya msako kwenye eneo karibu na ilikozama meli hiyo na kwamba zaidi ya wapiga mbizi 650 wanajaribu kulifikia eneo la ndani ya meli hiyo iliozama Jumatano.

0 comments:

Post a Comment