Huyu ni kijana mwenye uwezo mkubwa,BantuTz imeona sio mbaya kukuletea makala kuhusu kijana huyu ambaye kwa namna moja au nyingine anaweza akawa mfano wa kuigwa na vijana wengine.
Jambo moja ambalo wanafunzi
waliosoma naye nchini Tanzania
hawabishani kuhusu Malima ni ukweli
kwamba alikuwa ni mwanafunzi
mwenye akili nyingi darasani.
Shafii Dauda ambaye alikuwa
mwanafunzi wa kidato cha kwanza
katika Shule ya Sekondari Azania jijini
Dar es Salaam, anamkumbuka
Asanterabi kama mwanafunzi mwenye
akili aliyefanya vizuri sana katika
masomo yake ya kumaliza kidato cha
nne.
Shafii, ambaye sasa ni miongoni mwa
watangazaji na wachambuzi maarufu
wa mchezo wa soka hapa nchini
alikuwa kidato cha kwanza wakati
Malima alikuwa kidato cha nne.
Akili ile ya Malima imemfikisha
nchini Marekani ambako sasa
amefanya ugunduzi wa kidude chenye
saizi ya pini ndogo (milimita 0.250)
kinachoweza kubaini magonjwa ya
kuambukiza, kansa na moyo katika
hatua ya awali kabisa.
Ugunduzi huu, utakapofika mwisho
wake, unaweza kuokoa maisha ya
watu wengi duniani.
Fikiria tu
kwamba unakuwa na kifaa ambacho
mojawapo ya magonjwa hayo
yakikuanza unaubaini mapema na
kwenda kutibiwa.
Mamilioni ya watu wataokolewa
maisha yao na kijana huyu wa
Kitanzania.
“Siku zote nimekuwa na ndoto za
kugundua kitu ambacho kitaweza
kuokoa maisha ya watu. Baba yangu
alifariki kwa ugonjwa wa moyo
ambao ungegundulika mapema kama
kungekuwa na kifaa kama hiki.
“Kwa sasa sitaweza kuokoa maisha ya
baba yangu lakini ninaweza kuokoa
maisha ya wazazi au watoto wa watu
wengine kutokana na ugunduzi huu
nilioufanya. Nafurahi kwamba ndoto
yangu imetimia.
“Kansa, baadhi ya magonjwa ya
kuambukizwa na magonjwa ya moyo
huwa yanachelewa sana kugundulika.
Watu wengi hupoteza maisha, na kwa
nchi zilizoendelea hutumia pesa
nyingi sana kuwatibu waathirika.
“Kifaa nilichogundua ni kidude cha
ukubwa wa pini (0.250mm)
kinachoweza kupima na kugundua
hayo magonjwa mapema. Ili, yaweze
kutibika kirahisi, kuokoa maisha na
kupunguza gharama,” anasema
Asanterabi katika mazungumzo yake
na Admin wa BantuTz yaliyofanyika kwa njia
ya mtandao juzi,Jumamosi.
Asanterabi ni mtoto wa aliyepata
kuwa waziri wa fedha wa Tanzania,
Profesa Kighoma Ali Malima,
aliyefariki dunia Agosti 6, 1995 jijini
London, Uingereza, katika mojawapo
ya vifo vya kushtusha katika historia
ya Tanzania.
Kifaa alichokigundia kijana huyu wa
Kitanzania kinafahamika kwa jina
la Biolom na ugunduzi huu aliufanya
akishirikiana na wanafunzi wenzake
wawili wa Chuo Kikuu cha
Northeastern kilichopo Boston; Cihan
Yilmaz na Jaydev Upponi.
Pamoja na udogo wake, kipini hicho
kina jumla ya maeneo manne –yote
yenye kazi maalumu, na ubunifu huo
tayari umetambuliwa na Serikali ya
Marekani.
Katika mazungumzo yake na vyombo
vya habari vya Marekani, Asanterabi
alipata kusema kwamba vifaa vingi
vya kisasa hubaini magonjwa; kwa
mfano kansa, katika wakati ambapo
ni vigumu mtu kupata tiba na
kupona.
“Kazi yetu hii itakapokamilika,
tutaweza kubaini magonjwa haraka
zaidi na mapema zaidi na hivyo watu
watapata tiba mapema na kuokoa
maisha.
“Nchini kwangu (Tanzania),
akinamama wengi hufariki dunia kwa
sababu ya kuugua ugonjwa wa kansa
ya kizazi, kifaa hiki kitaweza kusaidia
watu wengi kupona kutoka katika
matatizo yao,” alisema.
Kidude hicho ni kidogo sana kwa
umbo na namuuliza kama wameamua
iwapo mtu anaweza kukinunua na
kubaki nacho nyumbani akijitazama
mwenyewe au ni lazima aende
hospitali.
“Dhamira yetu hapo ni kipimo
kitumike mtu akienda hospitali au
kliniki (for annual check-up). Lakini
japokuwa kinafanya kazi, kupata
ruhusa kwa kukiingiza kama pini ni
vigumu. Tunafanya vipimo (test) kwa
kupima damu iliyotoka kwa
mgonjwa,” anasema.
Asanterabi ni zao la mfumo wa
masomo wa kawaida uliokuwepo
hapa nchini miaka michache iliyopita
(kabla ya ujio wa hizi za kata na
‘academy’).
Alisoma katika Shule ya Sekondari ya
Tambaza jijini Dar es Salaam kwa
mwaka mmoja kabla ya kuhamia
Azania.
Miaka 20 iliyopita, hizi zilikuwa ni
shule zilizokuwa zikichukua watoto
waliofaulu vizuri kimasomo miongoni
mwa wanafunzi wa shule za msingi za
Mkoa wa Dar es Salaam.
“Tambaza nilisoma mwaka mmoja tu
lakini kutokana na fujo zilizokuwapo
nikahamishwa na wazazi na ndipo
nikaenda Azania nilikosoma mpaka
kumaliza kidato cha nne. Nashukuru
kwamba nilifaulu vizuri kwa kupata
daraja la kwanza. Kimsingi, nilipata
alama A katika masomo yangu yote,”
anasema.
Pamoja na muda wote alioutumia
Marekani na umaarufu ambao
ameupata kama mmoja wa vijana
wenye bongo zinazochemka nchini
humo, Asanterabi bado hajasahau
maisha ya hapa nchini na, hususan,
maisha ya shule.
Kimsingi, Asanterabi anasikitishwa
sana na matokeo mabovu ambayo
baadhi ya shule alizosoma katika
miaka ya nyuma zimekuwa zikiyapata
katika miaka ya karibuni.
“Kwa kweli nakumbuka sana walimu
wangu. Pale Tambaza, kwa mfano,
namkumbuka sana mwalimu mmoja
alikuwa anaitwa Mama Msuya, huyu
nadhani ndiye alikuwa mwalimu bora
kuliko wote pale. Huyu alikuwa
anafundisha Jiografia.
“Katika shule ya Azania, namkumbuka
sana Mama Shija ambaye naye
alikuwa akitufundisha somo la Kemia.
Mzizima namkumbuka sana mwalimu
mmoja alikuwa anaitwa Thind - best
mathematician ever (mwana hisabati
bora kuliko wote niliowahi
kufundishwa nao).
“Elimu ni sehemu nyingine ambao
inanisisimua mno. Nimefuatilia katika
tovuti ya Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi ( moe.org.tz )
kuwa mwaka 2011, karibu asilimia
50 ya wanafunzi walipata alama
sifuri. Tambaza, Forodhani, Kibasila
na Azania zilikuwa na watu wenye
akili kuliko wote, pengine Tanzania
nzima.
“Niko sasa nafanya kazi na vichwa
vya bongo huku Marekani tuone
tunaweza kufanya nini kutoa
mchango kwa "online video
learning" (mafunzo kwa njia ya
mtandao maana wengi wetu tulisoma
bure tu na huo utakuwa sehemu ya
mchango wetu kwa Taifa,” anasema.
Kutokana na ubunifu huo alioufanya
na wenzake hao, Malima sasa
anatakiwa kuanzisha kampuni
ambayo itafanya biashara ya ubunifu
huo utakaoleta mapinduzi katika
sekta ya afya duniani kote.
Haya ni mabadiliko makubwa katika
maisha ya Asanterabi ambaye aliwahi
kunukuliwa na vyombo vya habari
vya Marekani akisema kwamba siasa
iko kwenye damu ya familia yao.
Baba yake alikuwa mwanasiasa na
msomi maarufu nchini na kaka wa
Asanterabi, Adam, sasa ni Naibu
Waziri wa Fedha katika serikali ya
Rais Jakaya Kikwete. Pia ndiye
Mbunge wa Jimbo la Mkuranga
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Kusema kweli mimi sijawahi kujiona
kama mjasiriamali (mfanyabiashara).
Watu wengi walijua kwamba
nitakapokuwa mkubwa nitafuata tu
nyayo za wazee wangu. Lakini leo
niko hapa.
“Kwenye maisha yangu, sikutaraji
kwamba ipo siku nitakuja kufanya
ubunifu kama huu. Baada ya kufika
hapa nilipofika, sasa naamini
kwamba naweza kupiga hatua zaidi,”
anasema.
Ingawa fedha si msukumo mkubwa
katika maisha ya Asanterabi,
ugunduzi huu unaweza kumfanya
kuwa mmoja wa Watanzania matajiri
endapo kidude hiki kitaanza kuuzwa.
Hesabu zake ziko hivi.
“Tunafikiri kitakapokuwa tayari,
kidude kimoja kinaweza kuuzwa kwa
wastani wa dola moja hivi ya
Marekani (Shilingi 1650) kama
tukiweza kufanya uzalishaji mkubwa.
“Gharama ya kupimwa inaweza
kugharimu kiasi cha kati ya dola
10-15. Mahospitali huwa wanachaji
hela nyingi mno kama daktari ndio
atafanya vipimo na maamuzi. Ila
kama ni nesi gharama si kubwa,”
anasema.
Katika dunia yenye watu zaidi ya
bilioni sita, uwezekano wa kuuza pini
hizo milioni mia moja kwa mwaka ni
mkubwa na kwa kiasi hicho pekee,
mauzo ya zaidi ya dola milioni 100
kwa mwaka (zaidi ya shilingi bilioni
165) yanawezekana.
Asanterabi na wenzake watakuwa na
mgawo wao hapo na ifahamike kwa
sababu ya sheria kali za hatimiliki
nchini Marekani, hizi ni fedha
ambazo familia ya wagunduzi
watakula hadi kwa wajukuu, vitukuu
na kuendelea.
Safari ya Asanterabi kutoka Tanzania
kwenda Marekani haikuwa rahisa
namna hiyo. Ikumbukwe kwamba
alifiwa na baba yake wakati ndiyo
kwanza akiwa na umri wa miaka 15
tu.
Ni msiba ambao nusura ubadili
kabisa maisha ya kijana huyu ambaye
baadhi ya wanafunzi waliowahi
kusoma naye wanamtambua kwa jina
la “Mzaramo wa Chole.”
Chole ni miongoni mwa mitaa
maarufu ya eneo la Oysterbay jijini
Dar es Salaam ambako Asanterabi
alikulia. Pengine, jina hilo linatokana
na ukweli kwamba kuna watu
wachache wa kabila la Wazaramo
analotoka Malima wanaoishi huko.
Majina ya namna hii hayakuwa na
maana ya ubaguzi wa kikabila lakini
ni sehemu ya utani wa kikabila
uliokuwa Tanzania wakati huu.
Utafiti na ubunifu huu wa Asanterabi
si habari kubwa hapa Tanzania pekee
kwani inaonekana kwamba hata
Marekani nako ameanza kutambulika.
Juni mwaka huu, wakati wa sherehe
za maadhimisho ya Wiki ya Afrika
katika Jimbo la Massachussets uliko
mji wa Boston, Gavana wa Jimbo
hilo, Deval Patrick, alimpa Asanterabi
tuzo maalumu ya Ujasiriamali
akimpongeza kwa ubunifu wake huo
utakaosababisha nafuu kwa maisha ya
wanadamu na pia ukuaji wa uchumi
wa eneo hilo.
“Si kwamba ugunduzi huu utabadili
maisha ya wengi na uchumi kwa
wakazi wa Marekani pekee, lakini
ugunduzi huu utasaidia sana kuokoa
maisha ya mamilioni ya wananchi
katika nchi anakotoka Malima ya
Tanzania,” alisema Gavana huyo.
Miaka michache iliyopita, Asanterabi
alikuwa akijipanga kuwa mmoja wa
waajiriwa katika mojawapo ya
kampuni kubwa duniani ya Toshiba,
lakini sasa ugunduzi huu umemfanya
kujiandaa kuwa mmoja wa viongozi
wa kampuni muhimu hapa duniani.
Pamoja na umbali mkubwa uliopo
sasa, baadhi ya watu wanaomfahamu
Asanterabi wanamkumbuka kama
kijana mpole ambaye hakuharibiwa
na ukubwa wa jina la baba yake.
“Mzaramo wa Chole alikuwa mpole
sana kipindi kile anasoma Azania na
kwa kweli hakuwa na mambo mengi
kama walivyo watoto wengi wa
wakubwa,” anasema Mintanga Malulu
aliyesoma katika shule hiyo wakati
mmoja na Asanterabi.
Jambo zuri kuhusu Asanterabi ni
kwamba ni mzalendo na anayependa
nchi yake. Katika mazungumzo yake
Pia alisema kwamba kwa
namna yoyote ile ugunduzi wake huo
utaifaidisha Tanzania.
Tayari Tume ya Sayansi na Teknolojia
Tanzania (Costech) imetangaza
kuvutiwa na mafanikio ya Asanterabi
katika Nyanja hiyo ya sayansi.
Taarifa iliyotolewa na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo,
Dk. Flora Tibazarwa, inasema ingawa
utafiti huo bado haujafikia katika
hatua ya mwisho, matumaini ni
makubwa.
“Tuna taarifa kuhusu ugunduzi wa
Dk. Malima lakini hatuwezi kusema
chochote kwa sasa kwa vile bado uko
katika hatua za awali na haujapita
katika vipimo vyote. Jambo zuri ni
kwamba dalili za kufanikiwa ni
kubwa,” ilisema taarifa hiyo.
Ni safari ndefu, ndefu sana kutoka
Tanzania hadi Marekani. Lakini, kama
mwisho wake ni kama ule wa
Asanterabi, safari inakuwa njema.
Wakati tukiagana baada ya kumaliza
mazungumzo yetu, bado alionyesha
kusikitishwa na matokeo katika shule
za sekondari maarufu; Hivi, kuna nini
kinatokea huko kwa Azania na
Tambaza?
Sikuwa na majibu. Labda nitapata
kama nitafanya utafiti. Labda, itabidi
Asanterabi agundue kidude kingine
kitakachotoa majibu kuhusu kushuka
kwa elimu hapa nchini.
Swali moja kubwa ambalo nimejiuliza
baada ya makala hii ni moja tu; Hivi kweli
Taifa hili litakuja kutoa akina
Asanterabi wengine katika miaka 20
ijayo katika mfumo wetu
Endelea kutembelea www.bantutz.com
Imeandaliwa na Katemi Methsela.
0 comments:
Post a Comment