Facebook

Friday, 20 February 2015

Oparesheni ya kuwasaka wauaji Morogoro yaanza



Jeshi la polisi mkoa wa Morogoro limeanza kufanya oparesheni ya kuwatafuta  watuhumiwa waliohusika na mauaji ya  watu  watatu  wakiwemo wakulima wawili na mfugaji mmoja, wilayani Kilosa

 Jeshi la polisi mkoa wa Morogoro limeanza kufanya oparesheni ya kuwatafuta  watuhumiwa waliohusika na mauaji ya  watu  watatu  wakiwemo wakulima wawili na mfugaji mmoja,  kufuatia mapigano yaliyozuka kati  ya wakulima na wafugaji  katika bonde la matembele linalounganisha kijiji cha Mabwegere na Mbigiri wilayani kilosa mkoani Morogoro.

Mkuu wa wilaya ya Kilosa Elis Tarimo akizungumzia  tukio hilo wakati alipotembelea majeruhi  katika  hospitali  ya mission St Joseph  Dumila  amesema  mauaji hayo hayatavumilika na jeshi la polisi litahakikisha linawakamata waliohusika na tukio hilo.
Tarimo amewataja waliofariki dunia  kuwa ni Joseph Peter (26) mkulima, Rajabu Selemani (55) mkulima na Kaduru Kashu (30) mfugaji na wengine wamelazwa hospitalini hapo huku mmoja  akihamishiwa katika hospital ya mkoa wa Morogoro.

Kufuatia tukio hilo mkuu wa wilaya ya Kilosa Elias Tarimo ametupia lawama  Wizara ya  Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuchelewa  kuleta wasuluhishi wa mgogoro huo kama serikali ilivyoahidi kwa lengo  la kuhakiki upya  mipaka ya vijiji  ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji, iliyodumu kwa muda mrefu.

Nao majeruhi waliolazwa  katika hospitali ya Mission  Joseph  Dumila  wamelalamikia  serikali kushindwa kumaliza tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji ambapo wameelezea mapigano yalivyo tokea nae muuguzi wa zamu  Melania Shayo amesema wakulima wawili walifariki dunia wakati wakipatiwa matibu  na  kukiri kupokea maiti moja ya mfugaji  aliyeuwawa wakati wa mapigano hayo.

Mapigano haya yamekuja siku chache baada ya nyumba 41  kuchomwa moto zikiwemo za  wakulima na wafugaji kufutia mgogoro wa ardhi katika kijiji cha mabwegere wilayani kilosa, ambapo mkuu wa wilaya aliwakutanisha wakulima na wafugaji kwa lengo la kumaliza mgogoro huo lakini hata hivyo mkutano huo  uligubigwa na mivutano  na wafugaji kuondoka kabla ya mkutano kumalizika..

0 comments:

Post a Comment