Facebook

Sunday 4 October 2015

NA AYOS MATA MAESTRO:-KUELEKEA DIMBA LA EMIRATES (ARSENAL VS MANCHESTER UNITED)

Na: Ayoub Hinjo
Arsenal dhidi ya Manchester United ni mechi yenye hisia kali na msisimko usiolezeka. Ni mechi ya kihistoria sababu hizi ni timu mbili kubwa na zina mashabiki wengi duniani kote. Ni wapinzani kweli kweli iwe ndani au nje ya uwanja,mafanikio yao ni kielelezo tosha kuonyesha hawa ni wapinzani wakubwa. Mambo yafuatayo yanaweza kuleta taswira ya mchezo huu mkali.

ARSENAL

1: SAFU YA ULINZI

Safu ya ulinzi ya Arsenal ina watu makini wa kazi ambao wamekosa mseto mzuri ndani ya safu hiyo. Kukosekana kwa Konsielny ni pigo kubwa kwa timu hiyo sababu ni beki tegemezi ambaye anajituma na kujitolea kwa ajili ya timu,pindi inapokuwa na hali ngumu. Konsielny na Paulista wanatengeneza mseto mzuri ambao utajenga ukuta mgumu wa kati wa timu hiyo. Kukosena kwa Konsielny kunatoa nafasi kwa beki mzoefu na mkongwe Per Metersacker ambaye kwa mechi za karibuni alikuwa anakaa benchi kutokana na majeraha madogo madogo. Urejeo wa Metersacker kunaleta imani kubwa kwenye ulinzi sababu ni beki mwenye uwezo wa kusukuma timu kwenda mbele kwa pasi zenye macho na zenye madhara,lakini shida inaweza kuja kwao kama safu ya ushambuliaji ya wapinzani itatoa presha kubwa na kuwaweka kwenye pilikapilka muda wote sababu wote sio wazuri sana kwenye kufanya marking za haraka kwenye nafasi muhimu. 

Ugumu na ubishi alionao Paulista ni kielelezo tosha kuwa atafanya kazi kubwa kwenye safu hiyo na kazi ya Metersacker itakuwa kufukia mashimo ambayo Paulista atakuwa akiyatengeneza na kuziba kabisa mianya ambayo mipira itakuwa ikipitishwa.

2: SAFU YA KIUNGO

Mara nyingi kwenye timu ya Arsenal safu ya kiungo huwa na ubora mkubwa kuliko wapinzani. Conquelin na Cazorla wamejenga mseto mzuri ambayo umeleta hatamu nzuri kwenye timu na uelewano wao wa kuzuia na kupandisha timu umekuwa mchango mkubwa kwenye timu hiyo kupata matokeo chanya mara nyingi.

Bila kusahau mchango wa Aaron Ramsey ambaye amekuwa shujaa wa timu miaka ya karibuni. Ramsey ni kiungo ambaye anaweza kubadilika muda wowote kutokana na mfumo au kasi ya timu yake au wapinzani. Uwezo wake mkubwa wa kufunga umetokana na kasi yake ya kusogea eneo la mwisho la kisanduku cha adui.

3: SAFU YA MASHAMBULIZI

Alexis Sanchez na Theo Walcott wanatoa mchango mkubwa kwenye safu hiyo wakisaidiana na Giroud na Ozil. Muunganiko wao umekuwa na madhara kwenye safu ya ulinzi kutokana na kasi na uwezo binafsi wa kuweza kutengeneza mashambulizi ambayo wamekuwa wakiyatengeneza. Sanchez hakufunga mechi 6 wala kutoa pasi ya goli kwenye mechi zilizopita,lakini mechi ya 7 amefunga magoli matatu ambayo leo yanaweza kumletea morali ya kupambana na kuwa na hamu ya kuendelea kufunga pia Walcott amekuwa mwiba kwa mabeki hasa baada ya kutumika kama mshambuliaji wa kati kwa sasa.

Tatizo ambalo linatengenezwa na safu ya ushambuliaji ya Arsenal ni kushindwa kutumia nafasi ambazo wanakuwa wanazitengeneza. Nafasi zinatengenezwa nyingi lakini umakini wao umekuwa mdogo kwenye kuzitumia vyema nafasi hizo.

MANCHESTER UNITED

1: SAFU YA ULINZI

Mseto ambao umetengenezwa na Smalling na Blind umekuwa imara kadri siku zinavyokwenda. Uwezo wa kuzuia hasa Smalling amepevuka kiakili na anafanya kazi vyema kila siku inayoitwa leo. Blind mara nyingi amekuwa akitumika kama beki wa pembeni au kiungo mkabaji,lakini uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi umemweka sambamba na Smalling kati kati ambao wametengeneza mseto mzuri. Uwezo wa Blind ni kupiga pasi na kuhold wapinzani washindwe kusogelea lango la timu.

Safu ya ulinzi ya pembeni ni bora lakini shida ni pale Valencia anapotumika kama beki wa pembeni,uwezo finyu wa kuzuia umekuwa unakaribisha mashambulizi mara kwa mara kwenye sanduku la timu yake na kuwa weka kwenye mashaka makubwa wenzake.

2: SAFU YA KIUNGO

Machaguo mengi ya wachezaji yanaleta ushindani kwenye timu. Schweisteiger, Carrick,Herrera na Schneiderlin kila mmoja ana sifa ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza. Uwezo wa kuzuia,kushambulia na kutengeneza nafasi za mashambulizi hufanywa na safu hiyo ambayo imekuwa na madhara sana kwa wapinzani.

3: SAFU YA MASHAMBULIZI

Martial,Martial,Martial ni kinda mwenye kipaji ambaye amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu. Uwezo wa kufunga magoli na kutengeneza nafasi za magoli ni uwezo mzuri na ameonyesha mwanga wa kuwa tegemezi wa timu miaka kadhaa ijayo. Rooney bado hayupo kwenye kiwango bora lakini rekodi ambayo amekuwa nayo dhidi ya Arsenal inaweza kumtia hamasa ya kuonesha uwezo wake wa siku zote anapokutana nao. Rooney ndiye mchezaji wa Manchester United ambaye amefunga magoli mengi dhidi ya Arsenal kwenye ligi,magoli 9 na amefunga magoli 12 kwenye michuano yote aliyocheza dhidi yao. Rekodi aliyonayo inaweza kumuweka kwenye kilele chake. Mata ni mchezaji muhimu kwenye timu,pasi za magoli na uwezo wa kufunga vimemuweka kwenye chati ya ubora sasa ni ufunguo wa Manchester United kwenye mashambulizi. Memphis bado ana mengi ya kujifunza lakini kocha anamjengea imani ya kumwamini kwenye kila mchezo na kumpa nafasi aoneshe alichonacho ni upcoming nzuri na aangaliwe kwa jicho la tatu kwenye mchezo huo.

Bado tatizo ambalo United wanalo ndilo linalowasumbua Arsenal pia. Nafasi ambazo zinatengenezwa na timu ni nyingi lakini zimekuwa hazitumiki vyema.

HITIMISHO:

Arsene Wenger na Louis van Gaal ni makocha wazoefu na wenye mbinu mbalimbali ambazo zinaweza kuleta alama muhimu kwenye timu.

Arsenal imekuwa timu ngumu hasa msimu uliopita imekuwa inajiamini inapocheza na timu kubwa na kupata matokeo wanayotaka. Miaka kadhaa iliyopita ili kuwa timu ambayo inafungwa magoli mengi kila walipocheza na timu kubwa.

Timu inatakayo tumia nafasi vizuri ina asilimia kubwa ya kushinda.

Imeandaliwa na..........
(Ayo's Mata Maestro) E-mail: hinjo38@gmail.com

0 comments:

Post a Comment