“Rais Kikwete naye alikuwa mwanajeshi, sasa kuna ubaya gani kama mwanajeshi akitawala nchi. Kuna ubaya gani mwanajeshi mwenye akili akitawala nchi yetu. Mbona Komba (Kapteni John Komba), aliwahi kuwa mwanajeshi na sasa ni Mbunge wa Mbinga Magharibi. Jeshi ni la wananchi na hao wanajeshi wanaowasema wengine huwa tunakutana nao klabu za muziki.” Joseph Mbilinyi
Siku chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi kudai kuwa iwapo mfumo wa serikali tatu utapita, jeshi litachukua nchi, wanazuoni wametafsiri kauli hiyo kuwa ni ya kuwajengea hofu wananchi.
Jumapili Lukuvi, akiwa katika Kanisa la Methodist,
Jimbo la Dodoma alikokuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri Mkuu,
alisema muundo huo utasababisha nchi kutawaliwa na jeshi kwa kuwa
Serikali ya Muungano haitakuwa na fedha za kulipa mishahara wanajeshi.
Lakini mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Mohammed Bakari amesema kauli hiyo
ilitolewa katika jukwaa lisilo sahihi hususan kwa kiongozi kama Lukuvi.
“Kila kauli ina mahala pake. Haikutakiwa kwa mtu
mwenye madaraka kama yule kuzungumzia mambo nyeti kama hayo kanisani,”
alisema Dk Bakari.
“Licha ya kwamba kauli yake si mpya ilishasemwa na
Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete, lakini ilibidi ayaseme hayo
ndani ya vikao vyao na si kanisani.”
Alisema pamoja na kwamba kiongozi huyo alitoa
maoni yake binafsi, ilitakiwa aangalie kwanza kauli yake kabla ya
kuitoa. “Unapokuwa na nafasi ya juu ya uongozi, uhuru wako wa kutoa
maoni binafsi unapungua. Kwa hiyo kupitia nafasi hiyo itabidi uzingatie
masuala ya kuzungumza ukiwa raia, pia kiongozi,” alisema.
Mwanasheria Harold Sungusia alisema watu wanaodai
serikali mbili wamepungukiwa na hoja na ndiyo maana wanaanzisha masuala
mengine yasiyo na tija. “Nimepitia sheria zote nikagundua kuwa mtu
anayetetea hoja ya serikali mbili anakosa hoja za msingi ukizingatia
tayari muundo huo wa Muungano umedumu kwa miaka 50.”
Hata hivyo, mhadhiri wa Siasa wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema Watanzania hawatakiwi
kuacha kufuata hoja za msingi na kutishika na propaganda. “Hizo ni
propaganda kwa sababu hakuna utafiti uliofanywa na kugundua kuwa
serikali tatu zitaleta vurugu.”
Mkazi wa Mbagala Mtongani, Isaiah Solomon alisema
alichosema Lukuvi kinaweza kuwatisha raia hususan wale walio na uelewa
mdogo juu ya masuala ya siasa.
“Si jambo jema kusemea mambo hayo kanisani. Pia
alizungumzia kuhusu kugharimia jeshi, sifikiri kama ni wanajeshi pekee
wanaoweza kuleta madhara iwapo fedha za kuwalipa zikiwa pungufu; wapo
wafanyakazi wengine watakaoleta balaa,” alisema Solomon.
Mwenyekiti wa chama cha UDP Mkoa wa Dar es Salaam,
Joackim Mwakitinga alisema woga wa wanasiasa wanaotaka serikali mbili
ndiyo unaofanya watoe kauli za kuogofya wananchi.
“Naona ni woga tu wa wanasiasa wanaotaka kuleta mambo ambayo hayapo katika hoja za muundo wa Muungano,” alisema.
0 comments:
Post a Comment