Facebook

Friday, 18 April 2014

Makala Ya Michezo:Mseminari Wa Kale Anayehubiri Injili Kwenye Soka




           Katika maisha yangu sijawai ona watu wenye imani kali kama wahubiri
dini.Mapadri ,masheikh,wachungaji,  hawa watu wana imani kali sana na dini zao.Imani zao zimejengwa
kwa kusikia mafundisho ya vitabu vitakatifu.Hata biblia imenena kuwa “imani huja kwa kusikia ,tena
kwa kusikia neno la Mungu”.Qurani kurugo ya shekh, na Biblia kuwadi wa Mchungaji (Padre).Ili shekh
uitwe shekh lazima uwe una Imani thabiti ya dini ya kiislamu ilojengwa kwa misingi ya Qurani.Na
mchungaji vivyo hivyo,Lazima awe amejazwa neno la Imani kupitia misingi thabiti ya Biblia.Lakini
hakuna shekh aliekua shekh bila kupitia Mafundisho thabiti ya Dini ya kiislam,na ili uwe Padre
lazima upitie Seminari.

Achana na Seminari magamaga za siku hizi,Kila mtu akijenga shule anaiita
seminari.Matokeo yake wanatuzalishia magigisi na magobo.Seminari zilikua zamani bwana,Mtu
akitoka seminari hata bila kukwambia utamjua tu.Tabia hata hekima yake itaongea tu.Wachungaji
na Mapadre waliosoma seminari za Kale walifundwa wakafundika, walikanywa wakakanyika.Hawa
watu ni ngumu kuwatenganisha mbali na imani yao,Hawa watu huwezi kuwabadilisha kwenye kile
wanachokiamini.Mchungaji na Padre walishafundishwa,wakasikia pia wakasoma kuwa Isaka ni mzaliwa wa
kwanza halali wa ibrahim,Hasilani huwezi kumbadilisha na kumwambia Ismail ndie mzaliwa wa kwanza
halali wa ibrahim.Kesha ukeshavyo,hubiri uhubirivyo hawezi kubadili msimamo wake hasilani.

   Mpige mawe kama stephano,muwekee kisu shingoni bado atachukua mbundugo na kuendelea na Imani yake.
Mchungaji anaamini akimuombea kiwete atatembea tena,akimuombea kipofu ataona tena,kiziwi pia
atasikia tena.Muda mwingine kipofu huwa aamini kua siku moja akiombewa ataona,ila mchungaji ana
imani asilimia zote kua kipofu lazima atapokea uponyaji.Hata akimuombea mara ya kwanza kipofu
asione ila bado atakua na imani ipo siku kipofu huyo ataona tena kwa kua alishawai ombea vipofu
wengine wakaona tena.Huo ndo ujasili wa mchungaji,hiyo ndo imani ya mchungaji.

October 22 1949 mjini Strasbourg alizaliwa muinjilisti wa soka.Mwenye imani kali kama
Ibrahim.Huyu ni mtoto wa mzee Alphonce,aliyekua mfanya biashara maarufu wa vipuri mjini
Strasbourg.Alitumia muda mwingi kuangalia mpira akiwa bar.Hakika soka ilikua ndani ya damu
yake.Alitumia mbinu alizoziona bar na kuziamishia kwenye timu yake ya kijiji.Tangu kijana alipenda kazi
ya ukocha kuliko kucheza mpira.Mda mwingi alikua akipanga kikosi kwenye timu yake ya kijiji amayo
baba yake alikua akifundisha.

Maisha yake ya soka kama mchezaji yalianzia kwenye timu ya kijiji cha
Duttlenheim,kijiji ambacho alikulia mseminari huyu.Hakuna aliyemjua muinjilisti huyu kwenye maisha
yake ya uchezaji.Alitundika daruga akiwa na timu ya RC Strasbourg na kufungua ukurasa mpya katika
ngazi ya ukocha.Maisha yake kama kocha yalianza mwaka 1981 mara alipohitimu shahada yake ya
biashara na kukabidhiwa mikoba kama kocha wa timu ya vijana katika timu ya RC Strasbourg.Mwaka
1983 akateuliwa kua kocha wa vijana wa timu ya Cannes kabla ya kutimkia katika klabu ya Nancy 
Lorraine mwaka mmoja baadae,mwaka 1987 klabu ya Nancy ikashuka daraja.Wengi walifikiri huo ndo
utakua mwisho wa mseminari huyu katika maisha yake kama kocha,La hasha huo ndo ulikua mwanzo
wa nyota yake kuangaza.Mnamo mwaka 1987 klabu ya Monaco ikampa ajira ya kua kocha wa timu
hiyo,uteuzi huo ulileta maswali mengi sana,hakuna aliyeamini klabu kubwa kama Monaco itamteua
kocha alioyeishusha timu daraja.”Hakika huyu ni mwana wa Mungu”,ni mmoja wa watu wenye bahati
katika sayari yetu.

Msimu wake wa kwanza akiwa na Monaco akaiwezesha klabu hiyo kuwa bingwa
wa ligi kuu ya ufaransa,pia mwaka 1991 aliiwezesha Monaco kua bingwa wa kombe la ufaransa.Katika
kipindi chake kama kocha wa Monaco alipata kuwasajili wachezaji kama Glenn Hoddle na George Weah ambae baadhi ya watu walikejeli usajili wake lakini mwamba huo wa Afrika miaka kadhaa mbele
ukaibuka kua mchezaji pekee bora duniani kuwai kutokea kwenye Dunia yetu ya tatu.Huo ndo ujasiri
wa mseminari huyu ulipoanzia.Mwaka 1994 alishindwa kukubaliana na uongozi kuhusu mkataba wake
na klabu ya Monaco.Kumbuka klabu ya Monaco ilimzuia kwenda kufundisha katika klabu ya Bayern
munich mwaka huo huo.Huo ndo ulikua mwisho wake wa huduma kama kocha kwa klabu ya Monaco na
ufaransa kwa ujumla.Ailitimkia kwenye klabu ya Nagoya grampus kabla ya kupigiwa pande na rafiki yake
David dein kuinoa klabu ya arsenal mwaka 1996.Timu zote alizofundisha awali zilikua shule hapa ndipo
alipoanza rasmi kazi yake ya uinjilisti.
Utamwambia nini huyu mtu akuelewe wakati washabiki wa arsenal hawakumuelewa alipotumia
pesa kumnunua Dennis bergkamp.

Wengi walilalamika pesa zilizotumiwa kumnunua mdachi huyo.Ni
yeye pekee aliyeamini begkamp ana thamani hiyo. Baadae kidogo bergkamp akawaonesha wenger
alikua sahihi kuliko wadau na mashabiki.Unamkumbuka Anelka? Wakati anasajiliwa kinda huyu kila
mtu alimnyooshea kidole.Magazeti yote yakamuadaa na kuona kama amefanya kituko cha usajili.

Ila mzee huyu na imani kama ya abrahamu akamuamini anelka, anelka nae akampa kocha wake kile
alichokiona kutoka kwake .Mashabiki na wadau wakabaki midomo wazi,huku vyombo vya habari
vikiwa vimepigwa bao la pili na mfaransa huyu.Robbin va persie aliandamwa na majeruhi,mashabiki
wengi sana walipendekeza auzwe hasa pale Juventus walipotuma ofa.Lakini muinjilisti huyu akamkumbatia
kilema wake huku akiamini ipo siku kilema wake atatembea tena.Aliamini ipo siku RVP atakua
gumzo katika ligi ya uingereza.ndivyo ilivyotokea ,washabiki walotaka auzwe wakasahau wakaanza
kumshangilia.

 Aaron  Ramsey,huyu mpiganaji wa kiingereza, wenyewe humuita Rambow, ni mchezaji
bora wa arsenal mwaka 2013,licha ya kupata majeruhi bado anatarajiwa kua mchezaji bora wa arsenal
mwaka 2014.Huyu ni muingereza haswa,hujitoa asilimia mia ndani ya uwanja,hutoa kila kitu kwa ajili
ya timu yake.Kila mshabiki wa arsenal anampenda rambow,ila bila imani ya kocha wake huyu ramsey
asingekuwa mchezaji wa arsenal kwa sasa.Huyu mtoto wa mzee aliphonce ana imani kama ya David
Oyedepo,aliamin ipo siku ramsey atakua nyota.Lakini mashabiki wa arsenal waliona Ramsey ni kama
mgonjwa wa ukimwi,hawakuamini kama atapona siku moja.Ni yeye tu aliyemuamini
Huyu mzee wetu kuna mambo matatu ameamua kuyafumbia macho.Hayo ndo
yalioifanya arsenal ikose ubingwa kwa miaka nane na huu unaenda mwaka wa tisa bado anafanya
makosa yale yale yatakayomfanya atoke kapa tena. 

Kosa la kwanza ni kufumbia macho nguvu ya pesa ya Chelsea na Man city.
Bado anaiishi jana yake leo,Anaamini soka la karne ya 20 ni sawa na soka la karne hii.Katika utawala wake
alikua akishindana na Manchester united pekee.Manchester United ikitereza arsenal ilikua haifanyi
makosa.Tangu utawala wa Chelsea na Man city uanze Arsenal wametwaa taji moja tu.Arsenal ya sasa
inahitaji kutumia mabavu ya pesa ili kushindana na Chelsea na Manchester City.Huwezi kuchukua kombe
wakati unawategemea sanogo na Giroud na huku mwenzako ana Dzeko na Jovetic katika benchi la
wachezaji wa akiba. 

Pili ni Kuendelea kukumbatia wachezaji wasiompa matokeo.Tunajua kama wewe ni baba
wa imani kwenye soka ila kwanini usijifunze kwa yaliyokupata awali.Richard Wright,Denilson,Andre
santos,Francis Jeffers,Igors stepanovs,Sebastian Squillaci hawa ni miongoni wa wachezaji
mizigo aliowaamini na kuwapa nafasi.Licha ya kuwaamini na kuwangangania bado hawakumpa
matokeo,mwisho wa siku wachezaji hao wakaitia hasara klabu.Ila bado hajakoma tu,bado anaamini kwa
giroud,akimuangalia giroud anamuona henry ndani yake,imani yake ndio inamuongoza hivo.

Kosa lake kubwa na la mwisho kushindwa kufanya mabadiliko na marekebisho kwa kila sekta katika timu kwa msimu.
Kuna msimu arsenal inakua na beki nzuri na viungo wazuri lakini
inakosa mmaliziaji mzuri(mfano msimu huu),kuna msimu inakua na beki mbovu ila wanapata viungo
wazuri na washambuliaji wazuri,pia kuna msimu wanakua na beki imara na washambuliaji maridadi
lakini viungo wanarega.Wakati akiendelea kumsubiri RVP Cesc Fabregas alikua akiibeba timu licha
ya kuongozwa na safu nyepesi ya ushambuliaji iliyokua ikiongozwa na Adebayor.Mungu si Athuman
Robbin van persie akarejea lakini msimu unaofuata tangu Rvp arejee akamuuza cesc fabregas.Kiungo
cha arsenal kikarega,Akaanza kumuamini Ramsey huku Thomas rocisky akirejea taratibu kuziba pengo la
fabregas kipindi hiko Rvp anaibeba timu,Lakini msimu unaofuata akamuuza rvp ambaye alikua mmoja
wa washambuliaji hatari Duniani na kumnunua Olivier giroud kama mbadala wake,mpaka wa leo giroud
viatu vya rvp havimtoshi.pata picha arsenal ya leo ingekua na RVP na Samir Nasri,ungekua unahitaji
nini kwenye Dunia ya soka.Arsenal ilikua inahitaji mtu kama suarez ili avae viatu vya RVP,keshokutwa
atatafuta mshambuliaji mkali huku akisahau Rocisky na Cazorla umri unawatupa mkono.huyu kila msimu
anakomaa kuimarisha sekta moja au mbili tu.Kwake siku zinaganda,miaka haiendi.Huyu ndie Baba wa
imani,mimi napenda kumuita muinjilisti,Huyu ndie ARSENE WENGER,mwenye roho ya kiseminari,imani
ya kichungaji, hua akubali kupingwa kutoka kwenye kile anachokiamini, hua apangi kushindwa, ila
anashindwa kupanga.
               Imeandaliwa na……….   
                                               Allen kaijage
                                            (Middle Ya Juu)

0 comments:

Post a Comment