Facebook

Friday 23 January 2015

WAHAFAMU BINADAMU WENYE UWEZO WA KUTUMIA MIGUU AU MIKONO YOTE (KUSHOTO NA KULIA) KWA UFASAHA ZAIDI)-AMBIDEXTERITY



  


Duniani kuna viumbe vya aina mbalimbali ambavyo wengi wetu tunaamini Mwenyezi Mungu aliviumba kwa ustadi wa hali ya juu sana lakini wapo wale wanaoamini viumbe hivi vilitokea tu kwa nguvu isiyojulikana lakini mwisho wa siku tunarudi pale pale kwamba Kuna nguvu ya ziada ambayo wengi tunaamini Mwenyezi Mungu aliviumba.Kuna viumbe vya ajabu sana vilivyoko baharini na nchi kavu ama hakika ukistajaabu ya Musa utayaona ya firauni.Mabaharia na wavuvi wamepata wasaa wa kushuhudia vitu vya ajabu sana ambavyo kwa hali ya kawaida huwezi kuamini.Vivyo hivyo hata nchi kavu kuna baadhi ya sehemu duniani kuna viumbe vya ajabu na vya kustaajabisha.
 
Mfano mzuri ni Misitu ya Amazon iliyoko bara la Amerika ya Kusini hususan nchi ya Brazil kuna nyoka wakubwa na wanene kuliko wote duniani wanaojulikana kama Anaconda, ukirudi Tanzania sehemu moja inaitwa Kihansi mkoani Morogoro kuna Vyura wa ajabu ambao wao huzaa kama binadamu tofauti na vyura wengine duniani.
 Sokwe mtu wanaopatikana hifadhi ya Gombe-Kigoma pekee dunia nzima.Mnyama mkubwa duniani ambaye anaweza kutengeneza kisiwa cha muda mfupi ndani ya maji anaitwa nyangumi, ama hakika shughuli ya uumbaji ilikuwa ya kipekee sana.

Katika uumbaji mwenyezi Mungu aliumba viumbe mbalimbali kisha akavipa uhai na kila kiumbe kina umuhimu wake hapa duniani.Lakini katika uumbaji huo Mwenyezi Mungu alitumia maarifa zaidi katika kumuumba mwanadamu kwani alimpa utashi na kasha akampa mamlaka ya kuvitawala vitu na viumbe vyote vilivyoko duniani.

Ama hakika binadamu ni kiumbe cha kipekee sana.Lakini miongoni mwa wanadamu kuna mfanano na utofauti katika baadhi ya mambo moja wapo ni vipawa, Mwenyezi Mungu amemjaalia kila mwanadamu kipawa chake.Tumezoea kuona binadamu anayeweza kutumia mkono mmoja wapo kati ya mkono wa kulia au wa kushoto kwa ufsaha zaidi vivyo hvyo hata katika miguu. 

Leo ningependa nikuongezee maarifa na uweze kuwatambua baadhi ya binadamu wenye uwezo wa kutumia miguu au mikono yote kwa pamoja,yaani mkono wa upande wa kushoto na mkono wa upande wa kulia au mguu wa upande wa kulia na wa kushoto kwa ufasaha zaidi. Ama hakika Mungu ni wa ajabu sana.Kwa lugha ya kigeni na kitaalamu zaidi wanajulikana kama “Ambidexterity”

Binadamu waliozaliwa na uwezo huo wa kutumia viungo hivyo kwa ufasaha zaidi ni wachache sana, kwa dunia ya leo takwimu zinaonyesha kati ya watu 1000 unaweza kumkuta binadamu aliyezaliwa na uwezo huo mmoja.

Kwa ulimwengu sasa “Ambidexterity” wengi ni wale walizaliwa na uwezo wa kutumia mkono au mguu wa kushoto kisha wakajifunza kutumia viungo vya upande wa kulia, kisha wanamudu kutumia viungo hivyo kwa ufasaha zaidi.Mara nyingi inawezekana binadamu huyo akaanza kujifunza kutumia viungo vya upande wa kulia akiwa mdogo, shule ambapo mkono wa upande wa kulia unapendekezwa zaidi katika matumizi, kwa mfano mototo anapozaliwa akiwa anatumia mkono wa kushoto katika kula chakula, moja kwa moja wazazi wa huyo mototo watamlazimisha kutumia mkono wa kulia.

Vilevile binadamu anayetumia mkono wa kushoto anaweza kujifunza kutumia mkono wa kulia kutokana matumizi ya vitu mfano mkasi, opena na vingine vingi ambavyo vinaleta ugumu katika kuvitumia kwa mkono wa kushoto moja kwa moja inapelekea kujifunza kutumia mkono wa kulia.

Vilevile binadamu wanaotumia mkono wa upande wa kulia wanaweza kubadilika na kisha kutumia mikono yote au mkono wa kushoto kutokana na sababu mbalimbali kama vile ajali, aghalabu anaweza kubadilika na kuanza kutumia mikono yote kutokana na ufanyaji wa shughuli mbalimbali ambazo zinahitaji ubunifu wa ziada hasa katika shughuli zinazokuwa na uhitaji wa kutumia mikono yote miwili kwa mfano wale wanaotumia vifaa kama computer katika “TYPING” hali kadhalika katika kuogelea, upasuaji, kupiga gitaa, upiganaji wa ngumi yaani ‘boxing’ mchezo wa baseball, mpira wa miguu n.k

HAWA NI BAADHI YA NYOTA MBALIMBALI DUNIANI WENYE UWEZO WA KUTUMIA MIKONO AU MIGUU YOTE KWA UFASAHA.

MCHEZO WA RUGBY
Jonathan Edwards, huyu ni mchezaji wa mchezo wa rugby anasifika sana kwa kuupiga mpira wa rugby kwa kutumia miguu yote miwili, hakika ni jambo la kustaajabisha sana.

MCHEZO WA KIKAPU ‘BASKETBALL’
Katika mchezo wa mpira wa kikapu huko marekani uitwao NBA kuna nyota mbalimbali waliojaaliwa kipawa cha kutumia mikono yote miwili kwa ufasaha zaidi, anapotumia mkono wa kushoto na kulia huwezi kuona tofauti.Kawaida ni kwamba wanapotoa pasi fupi fupi wachezaji wa mchezo huo hupendelea kutumia mkono ambao ni dhaifu yaani ambao hautumii mara kwa mara.
 
 Lakini imekuwa tofauti zaidi kwa baadhi ya wachezaji kama Kobe Bryant, Kyrie Irving, Carlos Boozer, David Lee, John Wall, Derrick Rose, Andrew Bogut na Michael Beasley hawa wanavipawa vya ajabu sana, ukipata wasaa wa kuangalia mchezo huo utastajaabu namna wanavyoweza kutumia mikono yote miwili kwa ufasaha zaidi.

Lakini cha kustaajibisha zaidi ni mchezaji anayeitwa Bogut yeye anamudu zaidi kutoa pasi ndefu na kutumbukiza mpira katika kikapu kwa kutumia mkono ambao ni dhaifu kwake, mkono wa kushoto kuliko mkono wa kulia ambao ndio anaoutumia mara kwa mara.Kuna ndugu wawili Marc na Pau Gasol wanauwezo wa kutumia mikono yote kwa ufasaha zaidi.

Bob Cousy,lijendari wa timu ya kikapu Boston Celtics ililazimika atumie mkono wa kushoto baada ya kuumia mkono wa kulia alipokuwa shule baadae akawa anatumia mikono yote miwili.Mchezaji wa kati wa LA Clippers, DeAndre Jordan anatumia mkono wa kushoto katika kushuti lakini anaruka juu na kurusha mpira kwa kutumia mkono wa kulia.

MCHEZO WA MASUMBWI ‘BOXING’
Katika mchezo wa masumbwi tumeweza kuwashuhudia mabondia mbalimbali mashuhuri ulimwenguni mfano Jimmy Floyd Myweather Jr na Mike Tyson ni mashuhuri zaidi katika kurusha ngumi kwa kutumia mikono yote lakini mikono yao ya upande wa kushoto ndiyo yenye nguvu zaidi na akibahatika kukupiga ngumi kwa kutumia mkono wa kushoto pambano linaweza kumalizika mapema.
 
Vivyo hivyo kwa mabondia wengine kama Mohamed Ali, Evander wanauwezo mkubwa sana wa kutumia mikono yao kwa ufasaha lakini mkono wa kulia ndiyo wenye nguvu zaidi.Ukiachana na mabondia hao kuna bondia aitwae Manny Pacquiao huyu ndiye bondia pekee mwenye uweze wa ajabu na tofauti zaidi na mabondia wengine kutokana na umahiri mkubwa alionao wa kurusha makombora ya ngumi kwa kutumia mikono yote miwili kwa ufasaha zaidi.Huwezi kuiona tofauti anapokuwa anarusha ngumi kama mabondia wengine kitu amabcho kinamsaidia kupata ushindi mapema zaidi katika mapambano yake mbalimbali.

UCHORAJI
Kuna makala nilishawahi kuandika iliyokuwa inamhusu Leonardo Da Vinci, huyu ni miongoni mwa wanadamu wachache waliojaaliwa kuwa na akili ya ajabu na uwezo mkubwa sana.Naweza kujumuisha vitu vyote kwa kumuita ‘Genius’ kwa lugha ya kimombo.Aliishi katika karne ya 17.Alikuwa ni mchoraji, mbunifu na mhandisi mkubwa aliywahi kutokea duniani.
Alichora michoro mbalimbali ya majengo na kupanga miji mbalimbali mikubwa duniani kama vile Madrid, Paris, Venice, Lambardy-Italia, Fiorentina, Lens, Nice, Istanbul ama hakika hakuna mhandisi wa majengo yeyote Yule asiyemjua Da Vinci.Leonardo Da Vinci alijaaliwa kipawa cha kuchora kwa kutumia mikono yote miwili.Falsafa zake zinatumika hadi leo hii.
 
Lakini cha kuvutia zaidi ni mchoraji mwingine anayefuata nyayo za Da Vinci aitwae Gur Keren amabaye anaweza kuchora kwa kutumia mikono yote miwili hadi miguu kwa ufasaha zaidi.Ukimfuatilia Gur Keren utashangaa namna anavyoweza kutumia miguu yake yote miwili katika uchoraji.

MCHEZO WA SOKA ‘KANDANDA’
Tukiangazia katika mchezo unopendwa zaidi duniani, ukiwa umejikusanyia mashabiki katika pande mbalimbali za dunia mpira wa miguu huku wengine wakiuita soka au Kandanda .Tumeweza kushuhudia vipaji mbalimbali, vizazi mbalimbali vikija na kupotea kisha kuibuka kizazi kingine.Tumeweza kuona magwiji wa soka Ulimwenguni kama Pele, Garrincha,Maradona,Gaza, Roger Milla, Platini,George Weah,Zinedine Zidane Zizzou, Buckenber, Ronaldo,Patrick Kluivet,Ronaldinho,Rooney, Robert Pires, Zola,Silva,Fabregas,Rosicky, Bergkamp, Di Mateo, Carlos,Deco, Van Persie, Falcao, Hazard, Eto’o,Drogba,YayaToure,Paul Scholes, Lionel Messi, Mbwana Samata ‘SamaGoal’ ,Iniesta,Arjen Robben,Kevin Strootman, Xavi, Pirlo,Santi Carzola na wengine wengi wameweza kuuchezea mpira vile wanavyotakana kufanya chochote kilecwanachopenda uwanjani.

Lakini wachezaji wengi wamekuwa wakitumia zaidi mguu mmoja wapo kati ya kusho au kulia na wengi wanaweza kutumia mguu mmoja wapo kwa ufasaha zaidi na mwingine sio kwa ufasaha zaidi.
Lakini kuna baadhi ya wachezaji wamezaliwa wakitumia mguu mmoja wapo ama wa kushoto au wa kulia na kisha wakajifunza kutumia  mguu ambao walikuwa hawautumii kwa ufasaha zaidi.Wachezaji hawa wanakuwa na uwezo mkubwa uwanjani katika utoaji wa pasina kufunga magoli na vile vile wanakuwa na uwezo wa kucheza nafasi na pande mbalimbali uwanjani.

Wachezaji kama Cristiano Ronaldo, Wesley Sneijder,Xavi,Iniesta,Fabrigas, David Villa, Hernanes, Zinedine Zidane,Ross Barkley, Marek Hamšík, Adel Taarabt, Jack Rodwell, Adam Lallana and Radamel Falcao wanachukuliwa kama ‘ambidextrous’ kutokana na uwezo mkubwa walionao wawapo uwanjani katika utumiaji wa miguu yao.Hawa wamezaliwa wakitumia mguu wa kulia kwa ufasaha zaidi na kisha wakajifunza kutumia mguu wa kushoto.Wako wengi lakini hawa ni baadhi yao.

Ukiacha na wachezaji hawa ambao wamejifunza kutumia miguu dhaifu lakini kuna baadhi ya wachezaji wamezaliwa wakiwa na uwezo wa kutumia miguu yote kwa ufasaha zaidi, anapopiga mpira kwa kutumia mguu wa kulia na mguu wa kushoto huwezi kuona tofauti Andreas Brehme, Shinji Kagawa, Paolo Maldini and Pavel Nedvěd,Toni Kroos, Adriano Correia na Julian Draxler.

Lakini ukiachana na hawa wote mchezaji ambaye ananistaajabisha zaidi ni Mhispaniola anayekipiga katika klabu ya Arsenal Santi Carzola huyu ndiye mchezaji pekee mwenye uwezo wa kutoa pasi,kupiga mashuti ya umbali mrefu na kufunga magoli katika sehemu yoyote ile ya uwanja kwa kutumia miguu yote 100%.Unapomuangalia Santi Carzola lazma uvutiwe na staili anayocheza ,anakuwa ni hatari na mwiba mkali anapolikaribia lango la mpinzani.Arsene Wenger kocha wa Arsenal amekuwa akimpanga nafasi yapembeni katika mechi mbalimbali lakini alimtumia katika sehemu ya kiungo cha kati amahakika aliweza kutumia vyema uwezo aliokuwa nao na kuinyanyasa timu pinzani vilivyo. 

Ama hakika ukianza kuitadhimini kazi ya uumbaji ya Mwenyezi Mungu lazma upige goti kumsujudu na kumshukuru.Ninashukuru sana kuwa miongoni mwa ‘ambidextrous’ katika matumizi ya mikono.Mungu amevigawanya vipaji kwa watu mbalimbali,unaweza ukawa na kipaji Fulani usikigundue  changamoto inabaki kwako kufanya kila njia ukigundue kipaji chako.


Imeandaliwa na.....
                               Katemi Mugisha Methsela
                               (C.E.O BantuTz.com)
                                  +255 785 442 107
                                  +255 716 418 657
                              

0 comments:

Post a Comment