Facebook

Wednesday 30 July 2014

Askofu: Chikawe huna ubavu wa kulifuta kanisa langu.


Askofu Kiongozi wa Kanisa la
Moravian nchini, Alinikisa Cheyo amesema
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe
hana ubavu wa kulifuta kanisa lake.


Cheyo alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku
moja baada ya Waziri Chikawe kutishia
kulifuta kanisa hilo na madhehebu mengine
yatakayoendekeza migogoro.


Akizungumza Dar es Salaam kwenye
maombezi ya kuliombea Taifa yaliyoandaliwa
na Jumuiya ya Karismatiki Katoliki Jimbo Kuu
la Dar es Salaam juzi, Chikawe alisema Kanisa
la Moravian lina migogoro inayosababisha
hata waumini wake wapigane hadharani
wakati wa ibada.


“Ninawataka viongozi wa kanisa hili kumaliza
tofauti zao kupitia mabaraza yao ya ndani
badala ya kufikishana katika vituo vya polisi,
vinginevyo nitachukua hatua ya kulifuta kwa
kuwa yanahatarisha amani ya nchi,’’
alinukuliwa akisema Chikawe.


Kutokana na kauli hiyo, Askofu Kiongozi huyo
alijibu jana akisema: “Waziri hana uwezo wa
kufuta kanisa kwani ni la Mungu, lakini
migogoro itamalizwa na sisi wenyewe.”
Kwa kipindi kirefu kanisa hilo limekuwa na
migogoro maeneo ya Tabata na
Mwananyamala, Dar es Salaam na Jimbo la
Kusini Mbeya.


Hivi karibuni, wachungaji na waumini wa
kanisa hilo katika Jimbo la Mbeya walifunga
lango kuu la kuingia makao yake makuu na
kusababisha polisi na Mkuu wa Wilaya ya
Mbeya, Dk Norman Sigala kuingilia kati.


Kutokana na mgogoro huo, Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya wilaya hiyo, ilifanya kikao cha
dharura na halmashauri ya kanisa hilo na
ilidokezwa kwamba walifikia mwafaka mzuri.
Hata hivyo, baada ya siku mbili kanisa hilo
liliwasimamisha kazi wachungaji watano
ambao nao kupitia kwa wakili walitoa siku
saba kwa makamu mwenyekiti aliyeandika
barua kuwarudisha kazini haraka.

0 comments:

Post a Comment