Facebook

Wednesday 23 July 2014

Van Gaal atakavyopata kikosi cha kwanza

 
MANCHESTER United wanapiga tizi la nguvu nchini Marekani walikokwenda kujiandaa kwa msimu mpya wa Ligi Kuu England. Jumatano hii watacheza mechi ya kirafiki dhidi ya LA Galaxy na kuwapima nyota wake wapya Ander Herrera na Luke Shaw, huku kwenye benchi pia wakiwa na kocha mpya, Louis van Gaal.

Kwenye mazoezi ya Jumamosi, hali ya mambo ilionekana kuwa shwari wakati kocha Van Gaal alikuwa akitaniana na wachezaji wake akiwamo Wayne Rooney, ambaye alionekana kuwa na furaha kubwa kwa kuwa chini ya kocha huyo.

Van Gaal ana kazi ya kuiongoza Man United kuhakikisha inafanya vizuri kwenye Ligi Kuu England msimu ujao na kuonyesha kwamba hakubahatisha wakati kikosi chake cha Uholanzi kilichoshika nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka huu.

Wakati kikosi chake kikiwa hakina mastaa wengi baada ya Robin van Persie, Arjen Robben, Nigel de Jong na Wesley Sneijder kuwa pekee ndiyo wachezaji waliokuwa na majina kwenye timu hiyo, Van Gaal bado aliendelea kupata matokeo mazuri kutoka kwa nyota wake waliopo kwenye timu.

Van Gaal sasa amekabidhiwa kikosi ambacho msimu uliopita kwenye Ligi Kuu England kilimaliza kwenye nafasi ya saba. Mdachi hiyo atakuwa na shughuli pevu ya kupambana kwelikweli kupata matokeo chanya kutoka kwa wachezaji ambao kocha aliyemtangulia David Moyes alionekana kushindwa kuwatumia.

Kwenye Kombe la Dunia 2014, Van Gaal alibadili fomesheni katika kila mechi kulingana na mpinzani wake jambo ambalo alifanikiwa kupata matokeo. 

Jambo hilo pia anatarajiwa kulifanya atakapokuwa na kikosi cha Man United ili kuvuna matokeo mazuri.

Msimu uliopita, Moyes alichagua vikosi vya kwanza tofauti katika kila mechi aliyoiongoza timu hiyo kama kocha. Swali lililopo kwa sasa je, Van Gaal atatumia fomesheni gani au mtindo gani kwenye Ligi Kuu England msimu ujao atakapokuwa na kikosi cha Man United?

Kushambulia

Kocha Moyes alitaabika sana kuwatumia wachezaji wake wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka la kushambulia. Alikuwa na wachezaji wengi kwenye kikosi chake, lakini alishindwa jinsi gani awatumie.

Kama Van Gaal atatumia fomesheni ya 4-2-3-1, ambapo Juan Mata, Shinji Kagawa na Wayne Rooney kwa pamoja nyuma ya straika Robin van Persie, Man United watakuwa matata sana na kuisambaratisha ngome yoyote watakayokumbana nayo.

Kutokana na kikosi alichonacho kwa sasa kwa kuwatumia nyota hao wanne kwenye ushambuliaji, atahitaji kuwa na wakali wawili watakaocheza kama viungo wakabaji.

Mmoja wa nyota hao ni Ander Herrera na mwingine anaweza kuwa Michael Carrick, Marouane Fellaini, Darren Fletcher au Tom Cleverley. Hawa watakuwa na kazi moja tu ya kuwalinda mabeki wa kati na kunyang’anya mipira kabla ya kuwapa washambuliaji wafanye mambo yao.


Wakali wanne watakaounda safu ya ulinzi wanaotajwa kuwa watakuwa chaguo la kwanza la kocha huyo ni Shaw upande wa kushoto, Rafael Da Silva upande wa kulia, Jonny Evans na Phil Jones watakuwa katikati.
Golini atakuwa David de Gea. Kwenye kushambulia, Shaw na Rafael watatumika zaidi pembeni hasa kutokana na mtindo wa kocha huyo kupenda kutumia wachezaji wa pembeni.
Kulinda
Van Gaal amekuwa na kawaida ya kucheza soka la kujilinda wakati mwingine. Anafanya hivyo anapocheza na timu ambayo anadhani ni tishio sana na ina safu nzuri ya ushambuliaji.
Anapocheza mfumo wa kujilinda zaidi, mara nyingi pembeni amekuwa hatumii mabeki, anatumia mawinga wenye uwezo wa kukaba na kushambulia. Klabuni Man United anao wawili, Antonio Valencia anaweza kucheza kulia na Danny Welbeck upande wa kushoto.
Wachezaji hao wawili watasimama kwenye mstari sawa na viungo wa kati, huku Rooney akitumika kama kiunganishi wa mipira kutoka kwenye sehemu ya kiungo na kwenye safu ya ushambuliaji ambapo Van Persie atakuwa na kazi hiyo.
Mfumo wa kumtumia Rooney kama kiunganishi wa safu ya kiungo na ushambuliaji ulitumika pia na Moyes kitu ambacho mashabiki wa timu hiyo hawatapenda sana kitokee msimu huu.
Makinda
Vyovyote atakavyofanya kocha Van Gaal kama ataamua kutumia fomesheni kongwe za 4-4-2 au 4-3-3, atakuwa na nafasi kubwa ya kutumia wachezaji makinda kwenye kikosi chake.
Adnan Januzaj alicheza vizuri msimu uliopita chini ya Moyes anaweza kupata nafasi kwenye winga iwe kulia au kushoto. Kinda huyo ana uwezo pia wa kucheza nyuma ya mshambuliaji wa kati.
Tom Lawrence, ambaye alicheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha wakubwa wakati timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Ryan Giggs. Anaweza kucheza winga.
Kikosi hicho kina makinda wengine pia kama Ben Pearson anayemudu kucheza kiungo, wakati kwenye safu ya ushambuliaji kuna kinda anaitwa James Wilson mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao. Msimu uliopita alicheza mechi moja ya Ligi Kuu England, lakini alifunga mabao mawili.

Usajili
Mashabiki wa Man United wanaishi kwa ndoto. Wanataka kocha Van Gaal afanye usajili wa maana.
Wangependa kuwa na Arjen Robben kwenye kikosi chao, lakini hilo haliwezi kutimia baada ya Mdachi huyo kugoma kung’oka Bayern Munich. Kama wangempata Robben hata kama wangecheza 4-4-2 au 4-3-3 bado mchezaji huyo angecheza pembeni na Man United ingekuwa tishio sana kama Van Persie akiwa mshambuliaji wa kati.
Wengine anaowataka Van Gaal klabuni hapo ili kuifanya Man United kuwa tishio ni viungo wa kati, Bastian Schweinsteiger na Arturo Vidal.
Pia, anataka beki wa kati na Mats Hummels na Thomas Vermaelen wanapigiwa hesabu za kutua klabuni hapo.
Kupitia vitu hivyo vinne vitasaidia Van Gaal kupata aina ya kikosi cha kwanza na mfumo ambao atatumia kukijenga kikosi matata cha Man United msimu ujao.

Imeandaliwa na.....
                               Katemi P.Methsela

0 comments:

Post a Comment