Wednesday, 2 July 2014
Cameroon kuchunguza tuhuma za upangaji wa Matokeo.
Maafisa wa Cameroon wanafanyia uchunguzi madai kuwa wachezaji wao saba walihusika na upangaji matokeo katika michuano ya Kombe la Dunia nchini Brazil. Kamati ya maadili ya shirikisho la kandanda la Cameroon litatazama tuhumza juu ya "udanganyifu" uliofanywa na "matunda saba yaliyoharibika" katika mechi zao tatu za makundi.
Tuhuma hizo zimeandikwa kwenye gazeti moja la Ujerumani -Der Spiegel - na kumkariri mpanga matokeo aliyewahi kukutwa na hatia kutoka Singapore. Cameroon ilipoteza mechi zake zote katika Kundi A, ikiwemo kufungwa 4-0 na Croatia.
Alex Song alipewa kadi nyekundu kwa kumfanyia madhambi Mario Mandzukic katika mchezo huo, huku Benoit Assou- Ekotto na Benjamin Moukandjo wakifarakana pia.
Tuhuma za upangaji matokeo zimetolewa na mtu anayehusika na upangaji matokeo kinyume cha sheria- Wilson Raj Perumal, ambaye alikamatwa na polisi wa Finland mwezi Aprili baada ya kutolewa amri ya kimataifa ya kumkamata.
Katika mahojiano na gazeti la Der Spiegel, Wilson Raj Perumal aliweza kutabiri matokeo kati ya Cameroon na Croatia na pia kubashiri mchezaji kupewa kadi nyekundu.
Taarifa kutoka chama cha soka cha Cameroon imesema "Tuhuma za hivi karibuni za udanganyifu kuhusiana na Cameroon katika Kombe la Dunia Brazil 2014, katika mechi zake tatu za awali, hasa kati ya Cameroon dhidi ya Croatia, pamoja na uwezekano wa 'kuwepo kwa matunda saba yaliyoharibika ndani ya timu yetu ya taifa' hakuakisi misingi ya utawala wetu, sambamba na sheria za Fifa na taifa letu."
0 comments:
Post a Comment