Facebook

Tuesday 28 April 2015

Madereva wa mabasi ya abiria wapanga kugoma tena.

Siku 17 baada ya madereva wa mabasi mchini kugoma na kutikisa
nchi , Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani ( Taboa)
kimetangaza mgomo mwingine nchi nzima . Mgomo wa Aprili 9 ,
mwaka huu uliodumu kuanzia alfajiri hadi saa 7 :00 mchana
ulitikisa nchi na kuwaathiri abiria wengi waliokuwa wanasafiri
kwenda maeneo mbalimbali ya nchi . Jana Taboa walitangaza
kusitisha utoaji huduma kuanzia kesho ikiwa ni hatua ya kupinga
nauli mpya za mabasi zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa
Usafiri wa Nchi Kavu na Majini ( Sumatra) . Kufuatia hali hiyo ,
Taboa kimewataka mawakala kutokatisha tiketi kuanzia leo kwa
abiria hadi hapo Sumatra itakapotoa taarifa za kuruhusu nauli
ya zamani ziendelee kutumika . Katibu Mkuu wa Taboa, Enea
Mrutu , alitoa taarifa hiyo jana wakati akitoa majumuisho ya
mkutano mkuu wa dharura uliojumuisha wadau wa usafirishaji.
Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu tatu ambazo ni ajali za
barabarani, nauli mpya zilizotangazwa na Sumatra , madaraja ya
mabasi, mgomo wa madereva na vituo vya kubadilishia madereva
wanaokwenda umbali mrefu . Mrutu akisoma maazimio hayo baada
ya kumalizika kwa majadiliano hayo , alisema sababu iliyotolewa
na Sumatra kushusha nauli kutokana na bei ya mafuta kushuka
siyo kigezo muhimu bali ni shinikizo kutoka kwa wanasiasa . “ Kesho
kutwa ( kesho ) hakuna gari ambalo litatoka kituo cha mabasi
Ubungo kwenda mkoani na kama tutapigwa mabomu tupigwe, ila
msimamo wetu uko pale pale wa kutotoa magari hadi Sumatra
watakapotoa tamko la kutaka nauli za awali ziendelee kutumika, ”
alisema . Kuhusu ajali, alisema kutokana na kukithiri kwa ajali za
mabasi, wanakubaliana na utaratibu uliowekwa na serikali wa
madereva kubadilishana wanaokwenda masafa marefu katika
vituo ambavyo vitatengwa ili kupunguza ajali hizo . KILOMITA 80
KWA SAA Mrutu aliagiza madereva wote watumie mwendo wa
kilomita 80 kwa saa na wazingatie sheria za usalama barabarani
na watakaokiuka sheria hizo wachukuliwe hatua kwa mujibu wa
sheria. Alisema kuanzia Mei mosi , mwaka huu wataanza kutumia
vituo maalum vya kubadilishia madereva kwenye mabasi ya
masafa marefu kwa muda wa miezi mitatu kwa majaribio . Vituo
hivyo ni Singida mjini , kwa mabasi ya Dar es Salaam kwenda
Mwanza , Bukoba , Kahama ; na kituo cha Morogoro kwa mabasi
yanayokwenda mikoa ya nyanda za juu kusini . Uamuzi huo
umechukuliwa kutokana na mapendekezo ya Jeshi la Polisi kikosi
cha usalama barabarani , kubainisha kuwa chanzo cha ajali kwa
mabasi yaendeyo masafa marefu ni uchovu wa madereva . Mrutu
aliwataka wamiliki wa mabasi kuhakikisha madereva wao
wanazingatia taratibu na sheria zilizowekwa na Jeshi la Polisi
pamoja na Sumatra ili utoaji wa huduma uweze kwenda vizuri.
Alisema madereva ambao wameanza tabia ya kuwachafua
wamiliki wa mabasi kwamba wamekuwa wakielekezwa kwenda
mwendo wa kasi ili kuwahi abiria watawachukulia hatua
kwasababu suala hilo siyo la kweli .

“ Mimi ninunue gari la
mamilioni halafu nimlazimishe dereva aende mwendo kasi ni kitu
ambacho hakiniingii akilini inamaana sina uchungu na gari yangu ,”
alisema Mrutu Alisema mwendokasi wa kilomita 80 kwa saa , uwepo
wa vituo vya kubadilisha madereva wa mwendo mrefu na kukoma
kwa urasimu miongoni mwa askari polisi kuwa suluhisho la ajali za
barabarani nchini . Mrutu alisema katika utafiti wao wamebaini
kuwa chanzo kimojawapo kinachosababisha kutokea kwa ajali
nchini ni ubovu wa miundombinu ya barabara . Kwa upande wake ,
Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji wa maadili iliyopewa jukumu
la kuchunguza tatizo la ajali nchini , Abdulrazack Kimaro , alisema
ajali za barabarani zinasababishwa na mwendokasi.

Alisema
katika uchunguzi wao wamebaini hakuna hata dereva mmoja
anayezingatia sheria za usalama za barabrani ingawa Sumatra na
askari wa kikosi cha usalama barabarani wanakuwapo bali
kinachofanyika ni kumalizana kwa kupeana ‘ kitu kidogo’ .
Abdulrazack alisema wao kama wamiliki wa mabasi hawako tayari
kuendekeza madereva wanaokwenda kinyume cha sheria, hivyo
kila mmiliki kwa muda wake atoe somo kwa dereva wake juu ya
makubaliano hayo ili kudhibiti ajali.

Alisema madereva
wanatakiwa kusimamiwa kikamilifu kwenye utendaji wao na
kwamba kila mmiliki anapaswa kuwasilisha majina ya dereva wake
na vyeti , leseni kwa Taboa ili kuthibitisha ufanisi wake kwa kazi
anayoifanya. Naye Katibu wa Wamiliki wa Mabasi Mkoani Kigoma
( Kiboa ) , Hussein Kalyango , alisema serikali inatakiwa kuyafanyia
marekebisho baadhi ya mambo yakiwamo kanuni za usafirishaji
zinazomkandamiza mmiliki zaidi huku zikimwacha dereva nje ya
lawama mfano chanzo cha ajali . Kalyango alisema utaratibu wa
sheria za Sumatra zinamlenga mmiliki wa basi kwa utovu wowote
wa basi ambao anaufanya dereva . “ Tunaiomba Sumatra ibadilishe
sheria makosa anayofanya dereva adhibitiwe dereva na hata
kuchukuliwa sheria za zaidi na tunatakiwa kushirikiana Sumatra,
polisi na sisi kumaliza ajali hizi za barabarani ,” alisema .
CHANZO:NIPASHE

0 comments:

Post a Comment