Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
NAHODHA wa Burundi, Didier Kavumbangu
amesaini Mkataba wa miaka miwili na mabingwa
wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Azam FC mchana wa leo, BIN ZUBEIRY imeipata
hiyo.
Kavumbangu aliyemaliza Mkataba wake wa
miaka miwili Yanga SC, ameamua kusaini Azam
FC baada ya kuona klabu yake haina
mawasiliano naye licha ya kumaliza Mkataba
wake.
“Mimi ni mchezaji, kazi yangu ni mpira.
Nimemaliza mkataba Yanga, lakini viongozi
hawaniambii kitu, nimepata ofa nzuri Azam
nikaamua kusaini,” amesema Kavumbangu
akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya kusaini
Mkataba huo ambao unamfanya alipwe vizuri
kuliko alivyokuwa analipwa Jangwani.
Pamoja na hayo, Kavumbangu ameishukuru
Yanga SC na mashabiki kwa miaka miwili
aliyoichezea timu hiyo na anasema itabakia
kwenye kumbukumbu zake kwa ameshinda nayo
mataji.
Mshambuliaji huyo mrefu mwenye nguvu
amesema sasa akili yake anaipeleka kwa mwajiri
wake mpya, Azam FC ambako pia amepania
kwenda kushinda mataji na kuiwezesha timu hiyo
ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na
familia yake kufanya vizuri kwenye michuano ya
Afrika.
“Mimi sasa ni mchezaji wa Azam, nafurahi
kujiunga na klabu hii kubwa. Kawaida yangu
huwa nashabikia klabu nayochezea, sasa mimi ni
mshabiki namba moja wa Azam,”amesema.
Kavumbangu alitua Yanga mwaka 2013 akitokea
Atletico ya Burundi na katika mechi misimu
miwili ya kuichezea klabu hiyo, amefunga mabao
31 katika mechi 63 za mashindano yote, moja tu
la penalti.
Maisha mapya; Kavumbangu akitia dole gomba
Mkataba wa Azam leo
Tukutane Chamazi; Kavumbangu anahamisha
virago vyake kutoka Jangwnai hadi Chamazi
0 comments:
Post a Comment