MENEJA
wa England, Roy Hodgson, tayari anajua ni Wachezaji gani 23 atakuwa nao
huko Brazil kwenye Fainali za Kombe la Dunia zinazoanza Juni 12 na
hatarubuniwa na fomu ya Mchezaji yeyote kwenye Mechi hizi za mwisho za
Ligi Kuu England.
Akihojiwa na Wanahabari, Hodgson amesema
tayari ana mipango thabiti kabla hajatangaza Kikosi chake cha Wachezaji
23 hapo Mei 13 na uchaguzi wake huo wa Wachezaji unazingatia fomu ya
Mchezaji ya Miezi kadhaa na hata Miaka.
Amesema: “Hakuna kitu kitakachotokea
Gemu hizi 4 za mwisho na Mchezaji kung’ara na kunibadilisha mimi.
Siwapimi Wachezaji kwa hali zao za Dakika za mwisho kwenye Mechi 2 au 3!
Napima Wachezaji kwa zaidi ya Miaka miwili. Na kama yuko mpya kaibuka
basi nampima kwa Miezi kadhaa. Siwezi kufanya uamuzi kwa kutazama Wiki
iliyopita tu na hii ni mbaya sana kupima vipaji!”
Aliongeza: “Nilishakuwa na fikra za wazi
nini nataka kufanya na Kikosi hiki kwa muda mrefu sana. Hivi sasa najua
wazi nini nataka kufanya na hii Timu.”
Hodgson ndie Meneja wa kwanza wa
Kiingereza kuiongoza England kwenye Fainali ya Kombe la Dunia kwa Miaka
16 baada kuongozwa na Wageni kina Sven-Göran Eriksson, kutoka Sweden,
kwenye Fainali za Kombe la Dunia Mwaka 2006 na kutolewa Robo Fainali, na
kisha Fabio Capello wa Italy kwenye Fainali za Mwaka 2010 na kubwagwa
nje Raundi ya Pili.
England, ambao wako Kundi D huko Brazil,
wataanza Kampeni yao dhidi ya Italy hapo Juni 14 Mjini Manaus na
kufuatia Mechi dhidi ya Uruguay na Costa Rica.
0 comments:
Post a Comment